KIUNGO mpya wa Simba, Jean Ahoua ameanza balaa huko Misri akipiga bao mbili kwenye mchezo wa kwanza wa kirafiki wa wekundu hao, na kocha mmoja Mfaransa akatuma salamu kwa wapinzani.
Kocha Julien Chevalier wa Asec ambaye ni wapinzani wakubwa wa Stella d’Adjame aliyotokea Ahoua ameliambia Mwanaspoti kuwa kiungo huyo jina lake litaimbwa sana na mashabiki wa Simba kutokana na ubora wake.
Chevalier, raia wa Ufaransa, alisema Ahoua ni fundi wa mpira kama alivyo Pacome Zouzoua wa Yanga na kwamba, kuanza kwake kufunga mabao juzi ndiyo moto wake umeanza.
Kocha huyo alisema Simba itanufaika na usajili huo kwa kuwa Ahoua anaweza kucheza nafasi nne za kiungo mshambuliaji akitokea pembeni kote pamoja na namba nane na kumi.
“Jean namjua ni mmoja kati ya wachezaji bora. Hutachoka kumuangalia akiwa na mpira, ni mtu anayeinjoi kuuchezea mpira kwa pasi zake na hata kufunga,” alisema Chevalier.
“Kama amefunga, basi ndio ameanza hivyo. Simba wamepata mchezaji bora sana ambaye atawasaid-ia kwani anaweza kucheza nafasi nyingi za mbele. Unaweza kumtumia kutoka pembeni kokote utaka-potaka, (ama) akatokea katikati ni kiungo wa kisasa sana.
“Napokuwa namuangalia huwa ni kama namuona Zouzoua (Pacome) juu ya ubunifu wao wakiwa na mpira. Kama atafanya kazi na kocha anayependa soka la kushambulia ataisaidia sana Simba.”
Kocha huyo ambaye atakutana na Simba kwenye Kombe la Shirikishp Afrika, alisema Asec ilikuwa na hesabu za kumchukua Ahoua kabla ya wekundu hao kuwahi kumaliza biashara.
“Unajua shida kubwa ligi ya hapa ilichelewa kumalizika nadhani hapo ndipo Simba ilipotuacha, waka-muwahi na kumsajili, lakini ilikuwa tumchukue,” alisema.
“Hatukuwa tumepata mtu sahihi wa kushika nafasi ya Zouzoua tukaona tuje tumchukue Jean, lakini naye tumemkosa. Tutatafuta mwingine.”