WAKATI Simba ikizindua wiki ya tamasha la kila mwaka ‘Simba Day’ leo Jumatano katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Morogoro, mashabiki wa timu hiyo wa mkoani Tanga wanatarajia kuchangia damu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Matawi ya Simba Tanga, Edgar Mdime amesema imekuwa ni desturi yao kila mwaka kufanya shughuli za kijamii kila wanapoazimisha wiki hiyo, lakini mwaka huu itakuwa ya tofauti kutokana na namna walivyojipanga kuhamasisha wanachama na mashabiki wa timu hiyo.
Mdime amesema katika kufanikisha hilo tayari wameshafanya hamasa kwa kutembelea matawi yote ya mashabiki na wapenzi wa timu hiyo ambapo kila mmoja ameonekana kuwa tayari kwa ajili ya kujitolea kuwezesha wagonjwa waliopo hospitali wanaohitaji kuongezewa damu.
“Imekuwa ni kawaida yetu kila mwaka kabla ya kuanza kwa msimu kwenye wiki ya Simba Day, sisi mashabiki wa Mkoa wa Tanga tunaungana na wenzetu kufanya shughuli za kijamii na mwaka huu tumejiandaa kuchangia damu kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zetu wagonjwa wenye uhitaji wa kuongezewa damu,” amesema.
“Tumekuwa tukifanya hivi kila mwaka, lakini awamu hii tumeboresha zaidi na watu wamehamasika watajitokeza kwa wingi. Nimefanya ziara ya kutembelea matawi yote yaliyopo hapa Wilaya ya Tanga.
“Tuna matawi 15 ndani ya Jiji la Tanga, bado wapo wenzetu mashabiki na wapenzi wa timu yetu katika wilaya (zingine) tunatarajia kwenda kuwatembelea na kuwafungulia matawi. Mwitikio wa mashabiki ni mkubwa tunaipenda timu yetu.”
Aliongeza kuwa, “baada ya zoezi hilo la uchangiaji wa damu tutakwenda kuungana na mashabiki wenzetu wa kutoka mikoani kushuhudia mubashara kilele cha Simba Day timu yetu ikicheza.
“Tanga tutaondoka kwa pamoja siku moja kabla ya tukio, kila mwanachama na shabiki atachangia nauli ya kwenda na kurudi Sh40,000.”
Edgar aliupongeza uongozi wa timu yao kwa usajili mkubwa wa wachezaji walioufanya katika dirisha hili, akiamini wanakwenda kurudisha heshima iliyopotea kwa misimu mitatu katika Ligi Kuu Bara ambapo wamepoteza ubingwa kwa watani zao, Yanga.
“Tunakwenda kimataifa watu hawataamini kile ambacho tutakwenda kukifanya katika Kombe la Shirikisho (Afrika),” alisema.