TANZANIA NA CZECH MBIONI KUONDOA UTOZAJI WA KODI MARA MBILI

Naibu Katibu Mkuu wa Usimamizi wa Uchumi, Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwamdumbya na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Masuala ya Kodi Kimataifa wa Wizara ya Fedha ya Czech aliyeongoza ujumbe wa Czech Bw. Václav Zíka, wakisaini nyaraka za kukamilisha majadiliano, katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Usimamizi wa Uchumi, Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwamdumbya na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Masuala ya Kodi Kimataifa wa Wizara ya Fedha ya Czech aliyeongoza ujumbe wa Czech Bw. Václav Zíka, wakibadilishana nyaraka za kukamilisha majadiliano, katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Usimamizi wa Uchumi, Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwamdumbya na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Masuala ya Kodi Kimataifa wa Wizara ya Fedha ya Czech aliyeongoza ujumbe wa Czech Bw. Václav Zíka, wakionesha nyaraka za kukamilisha majadiliano, katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Usimamizi wa Uchumi, Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwamdumbya na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Masuala ya Kodi Kimataifa wa Wizara ya Fedha ya Czech aliyeongoza ujumbe wa Czech Bw. Václav Zíka, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukamilika kwa majadiliano ya kuondoa vikwazo vya kikodi katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)

Na. Saidina Msangi, WF, Dar es Salaam

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Czech zimekamilisha majadiliano ya Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili yatakayowezesha wawekezaji na wafanyabiashara watakaofanya shughuli zao kati ya nchi hizi mbili kutozwa kodi katika mapato yao katika nchi moja badala ya kila nchi kutoza kodi ya mapato.

Majadiliano hayo ambayo yamefanyika katika duru ya tatu yalikutanisha pande hizo mbili Tanzania ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwandumbya na Serikali ya Czech ikiongozwa na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Masuala ya Kodi Kimataifa wa Wizara ya Fedha ya Czech, Bw. Václav Zíka, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwandumbya ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania katika majadiliano hayo, amesema kuwa hatua hiyo itavutia mzunguko wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Czech na kufungua fursa mpya za kiuchumi.

‘‘Mkataba huo utakaposainiwa utawezesha wawekezaji na wafanyabiashara watakaofanya shughuli zao kati ya nchi hizi mbili kutozwa kodi katika mapato yao katika nchi moja badala ya kila nchi kutoza kodi mapato ya aina moja na kusababisha changamoto ya utozaji kodi mara mbili (Double Taxation)’’, alifafanua Bw. Mwandumbya.

Naye kiongozi wa ujumbe wa Czech, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Masuala ya Kodi Kimataifa wa Wizara ya Fedha ya Czech Bw. Václav Zíka, alieleza kuwa Serikali ya Czech inatambua umuhimu wa Mkataba huo katika kuibua fursa za ajira, biashara na uwekezaji ambazo zitakuwa endelevu kutokana na kuweka mazingira ya kisera yanayotabirika.

Pamoja na hayo, amefafanua kuwa Mkataba huo utakaposainiwa unatarajiwa kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa nchi hizo mbili kupitia upatikanaji wa taarifa za kikodi na utatuzi wa migogoro ya kikodi.

Kufuatia kukamilika kwa majadiliano hayo, kwa sasa inasubiriwa kukamilika kwa taratibu za ndani za kisheria kwa kila nchi kuwezesha Mkataba huo kusainiwa na hatimaye kuridhiwa ili kuanza kutekelezwa.

Related Posts