Kutoka ukondakta hadi kucheza Yanga, JKT Tanzania

HISTORIA ya maisha ya mshambuliaji wa JKT Tanzania, Matheo Antony itakufunza kutoyakatia tamaa maisha, kwani wakati anasajiliwa Yanga msimu wa 2015/16 alikuwa anapiga mishe za ukonda wa daladala.

Kwenye mahojiano yake na Mwanaspoti, amesema mwaka 2014 hadi mwanzoni mwa 2015 wakati anacheza KMKM alipiga sana mishe za ukonda wa daladala, pamoja na hilo amesema haikumzuia kukipigania kipaji chake cha soka.

Mwanaspoti: Ulipangiliaje muda wa mazoezi na kufanya kazi ya ukonda?

Antony: Mazoezini nilikuwa naenda saa 1:00 hadi 4:00 asubuhi, ilikuwa ikifika saa 5:00 naenda kufanya kazi ya ukonda hadi usiku na ilinifunza unyenyekevu wa maisha.

Kazi ya ukonda nilikuwa nafanya siku moja, siku inayofuata napumzika, kuupa mwili nguvu ili kukiwa na mechi niweze kucheza kwa kiwango cha juu.

Mwanaspoti: Kwa siku ulikuwa unapata shilingi ngapi kwenye ukonda?

Antony: Nilikuwa napata Sh20,000 hadi 30,000. Nilikuwa nikichanganya na maokoto kutoka KMKM, angalau nilikuwa naweza kujikimu kimaisha na kuwasaidia wanaonizunguka.

Mwanaspoti: Yanga ilikuonaje?

Antony: Nilionekana kupitia KMKM mwaka 2015, ndio maana nimesema ukonda haukunipumbaza nikiache kipaji changu, baada ya kusajiliwa Yanga ndio ikawa mwisho wa kazi hiyo.

Mwanaspoti: Unapanda daladala na kama ndio ukiwaona makondakta nini kinakujia?

Antony: Nawaheshimu, najua kuna watu wanaowategemea kupitia kile wanachokipata, wakati mwingine nawapa moyo kuwaambia hata mimi nilikuwa nafanya kazi hiyo, pia tunategemeana, konda anakurahisishia kujua gari linakwenda wapi, hivyo apewe heshima.

Mwanaspoti: Yanga ilibadilisha maisha yako?

Antony: Yanga ilibadilisha maisha yangu kwa kiasi kikubwa, pia ilinifungulia njia ndio maana nimecheza timu nyingi za Bara, ila kwamba nimefanya hiki na kile siwezi kuviweka wazi kabisa.

Baada ya kutoka Yanga mwaka 2019 nilikwenda kufanya majaribio na klabu ya FC Lupopo ya DR Congo, nilipoona aliyetupeleka anaanza kuleta janjajanja, nikaamua kurudi Tanzania, maana sipendi udanganyifu kwenye mapambano yangu za kutafuta pesa.

Matheo msimu huu anamiliki mabao manne, aliyofunga akiwa na Mtibwa Sugar, huku timu za Ligi Kuu Bara alizozicheza ni Yanga, Polisi Tanzania, KMC, Mtibwa na sasa JKT Tanzania.

Related Posts