Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema, Washington imealika jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF kuanza mazungumzo yatakayosimamiwa na Marekani kuanzia tarehe 14 Agosti.
Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Daglo, ambaye amekuwa vitani na jeshi linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan kwa karibu mwaka mmoja, ameukaribisha mwaliko wa Blinken na kwamba upande wake utashiriki mazungumzo hayo.
Soma pia: Marekani yatoa nyongeza ya mamilioni ya dola kuisaidia Sudan
Blinken amesema mazungumzo nchini Uswisi yanalenga kufikia usitishaji wa ghasia nchini kote, kuwezesha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa wanaohitaji, na kuandaa utaratibu thabiti wa ufuatiliaji na uhakiki ili kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano.
Juhudi za upatanishi
Hata hivyo mazungumzo ya awali ya mjini Jeddah, Saudi Arabia, yalishindwa kusitisha mapigano ambayo yamesababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao, na kusababisha onyo ya tahadhari ya kuibuka kwa baa la njaa na kuacha maeneo ya mji mkuu Khartoum kuwa magofu.
Juhudi za upatanishi zilizofuata, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Afrika, zimeshindwa kuzileta pamoja pande zinazozozana katika chumba kimoja cha mazungumzo, huku wataalam wakisema vikosi vyote vinashindana kuidhibiti Sudan.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja, vita vya kikatili vimeendelea katika nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika kati ya jeshi la kawaida chini ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na RSF inayoongozwa na naibu wake wa zamani Daglo.
Mzozo huo umesababisha makumi ya maelfu ya vifo na kuhamisha zaidi ya watu milioni 10, ikiwa ni pamoja na milioni mbili ambao wamekimbia kuvuka mipaka, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Mazungumzo hayo ya Uswisi yatakayosimamiwa na Marekani yataongozwa kwa pamoja na Saudia na yatajumuisha wajumbe kutoka Umoja wa Afrika, Umoja wa Falme za Kiarabu, na Umoja wa Mataifa kama waangalizi.
Hali yazidi kuwa ngumu
Huku haya yakijiri msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, ameonya kwamba takriban watu milioni 26 wanakabiliwa na njaa nchini Sudan.
“Ugumu wa maisha unazidi kuwa mbaya msimu wa mvua unapoanza. Kivuko cha mpaka cha Tine – ambacho kinatumika kusafirisha bidhaa kutoka Chad hadi eneo la Darfur nchini Sudan – kwa sasa hakipitiki kutokana na mvua kubwa na mafuriko. Njia nyingi katika sehemu ya kusini ya Sudan pia hazifikiki.”
Kulingana na Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), ufadhili wa ziada unahitajika nchini Sudan.
//AFP