Ukiukaji wa sheria unavyoathiri miundombinu ya masoko Dar – 1

Dar es Salaam. Utekelezaji usioridhisha wa sheria za usimamizi wa mazingira na sheria ndogo za masoko katika Mkoa wa Dar es Salaam umesababisha kuibuka kwa masoko yasiyo na viwango, yenye miundombinu mibovu na uchafu uliokithiri unaohatarisha afya za wananchi.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa miezi mitatu kwenye masoko 11, umebaini sheria hazitekelezwi ipasavyo na kusababisha mengi hali yake kuwa mbaya.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 2004, kifungu cha 115 (1), inahitaji mamlaka za serikali za mitaa kufanya uchambuzi, utunzaji na utupaji wa taka kwa njia inayozingatia aina ya taka, kama vile taka za kuoza, plastiki, kioo au chuma. Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa wa kiwango cha chini.

Hata kwa kuzingatia sheria ndogo za halmashauri kuhusu ushuru wa masoko na magulio, ambazo zinahimiza kuboresha miundombinu, usafi na usalama wa masoko, hali haijakidhi viwango vinavyotakiwa. 

Mkoa wa Dar es Salaam una jumla ya masoko 87 yanayosimamiwa na manispaa, lakini kuna masoko 106 kwa jumla ikiwa ni pamoja na madogo na magulio, lakini ni machache tu yapatayo sita yanayofanya vizuri kama vile Kisutu, Magomeni, Tandale, Mbagala, Temeke Sterio na Buguruni, kama yalivyobainishwa na Mohamed Mwekya, mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa masoko.

Kwa mfano, soko kubwa zaidi la Tegeta Nyuki linalohudumia maelfu ya watu katika kata za Wazo, Mabwepande, Bunju na maeneo mengine, lina miundombinu dhaifu ambayo husababisha mafuriko na tope wakati wa mvua. 

Masoko mengine kama Kawe na Ilala Boma, ingawa yana shedi (paa la wazi la kuzia mvua na jua) za kutosha, bado yanakabiliwa na changamoto za ubovu wa miundombinu kama ufinyu wa njia na vibanda vingi vilivyopo ni vya muda.

Suala la usafi nalo limekuwa tatizo katika masoko mengi, na wafanyabiashara wengi wanakiuka sheria kwa kuweka bidhaa chini, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya umma. 

Wakati hali ikionyesha hivyo katika soko la Kawe, mambo ni tofauti kwa Soko la Ilala Boma na uchunguzi unaonyesha soko hilo lina miundombinu ya kutosha, lakini limejaa wafanyabiashara mara tatu zaidi ya idadi iliokusudiwa, kwa mujibu wa Julius Ndele, mchumi katika Manispaa ya Ilala.

Ndele ameiambia Mwananchi kuwa hali hiyo imesababisha matatizo kadhaa katika soko hilo, kama ukosefu wa mifereji ya maji kutokana na njia za kuipitisha kuwa finyu, na vibanda vingi vya muda.

Idadi ya wafanyabiashara katika soko la Ilala Boma inakadiriwa kuwa 2,000 badala ya watu kati ya 600 na 700.

Kuna kizimba cha kuhifadhia taka, kilichopakana na vibanda vya mamalishe na biashara nyingine ndogondogo za vyakula. Hali hii inaelezwa kusababisha harufu mbaya, wadudu, mambo ambayo yana madhara na yanapunguza wateja.

Soko la Buguruni, lenye wafanyabiashara 2,000, lina tatizo la kuwa na njia nyembamba za watu kupita ndani ya soko na wafanyabiashara wengi wamepanga bidhaa zao chini.

Changamoto nyingine ni ufinyu wa barabara hasa kwa kuingiza magari ya mizigo, kama alivyobainisha Katibu wa wafanyabiashara wa soko hilo, Furahisha Kambi.

Amesema licha ya uwepo wa mifereji ya maji inayotiririsha maji na baadhi ya wafanyabiashara wako nje ya sehemu zilizotengwa.

Soko la Temeke Sterio lenyewe lina wafanyabiashara 6,000 na linahudumia masoko mengine ya Temeke na maeneo jirani. Ingawa lina shedi za kutosha, bado wafanyabiashara wengi wamejipanga kwenye maeneo ya wazi au pembezoni mwa barabara za soko, hivyo kusababisha msongamano na kuleta wasiwasi wa usalama.

Kadhalika, Soko la Tazara – Veterinary limekuwa na historia ya kujaa maji, lakini miundombinu yake imeimarika na sasa linawahudumia watu, hasa wanaofanya kazi eneo la viwanda vidogo.

Wafanyabiashara wengi wanaouza matunda na chakula katika soko hilo wanafikia 360 na bado lina maeneo ambayo kipindi cha mvua hutuwamisha maji mengi yanayosababisha adha kubwa kwa wafanyabiashara na wateja.

Soko lingine ni la Mabibo lililopo Manispaa ya Ubungo, lenye wafanyabiashara 2,183, maarufu kwa kuuza ndizi. Miundombinu ya soko hili, kama yalivyo mengine mengi, inakabiliwa na changamoto kuwa na  mifereji dhaifu ambayo haiwaruhusu watumiaji kupita kwa urahisi, hasa wakati wa mvua.

Vilevile, Manispaa ya Kigamboni yenye umri wa miaka saba, ilirithi masoko yake mengi kutoka Wilaya ya Temeke kama anavyoeleza Hassani Pongwa, ofisa biashara wa manispaa hiyo.

Anasema Soko la Kigamboni Ferry lina wafanyabishara 291 na liko kwenye matengenezo.

Soko jingine ni lile la Ungindoni lenye wafanyabishara 112, likiwa dogo kwa mwonekano, pembezoni mwa barabara ya Kibada. Lina shedi moja kubwa inayoingia karibu robo tatu ya wafanyabiashara na vizimba vyake vimejengwa kwa kuacha nafasi za watu kupishana, japo hakuna sakafu chini.

Karibu kabisa na barabara kuu kipo kizimba cha kuhifadhia taka cha kuhamishika. Licha ya kwamba hakuna mazingira hayo hayaruhusu taka kutenganishwa, hakukuwa na taka zilizozagaa.

Mfanyabiashara wa kuku katika soko la Kawe, Michael Mahinya anasema kukosekana kwa paa kunawaathiri sana wakati wa mvua au jua kwa kuwa kuku wanakufa. Kungekua na roofing (paa) ingepunguza hasara,” anasema.

Kauli ya Mahinya inaungwa mkono na Merania Yonas, muuzaji wa samaki kwenye soko hilo, kuwa “eneo ni bovu na wakati wa mvua huwa wanafunga biashara.”

Akifafanua, anasema eneo la wauza samaki limepakana na mfereji mchafu wenye maji yaliyotuama.

Hali wanayokumbana nayo wafanyabiashara na wateja wa Kawe, haina tofauti sana ya ile Tegeta Nyuki, kana inavyothibitishwa na Pastory Antony, mfanyabiashara wa duka.

 “Tunakosa wateja kwa sababu ya miundombinu mibovu. Pia maji hayapatikani kwa urahisi na vyoo ni vichache”.

Mtumiaji wa soko hilo, Bertha Eliya ambaye ni mkazi wa Tegeta anasema, “mimi nafanya manunuzi yangu hapa bidhaa zipo, japo mazingira sio mazuri. Kuna tope na uchafu mwingi. Pia hakuna parking (maegesho) ya magari ni adha kubwa kwetu”.

Licha ya mabadiliko ya miundombunu katika soko la Buguruni, mfanyabiashara Suleiman Mohamed anasema bado kuna changamoto.

“Miaka ya sasa kuna shedi (paa) lakini bado kuna tatizo kubwa la tope. Zamani tulikuwa wachache tulitosha eneo dogo sasa hivi tupo wengi ila miundombinu haijaongezeka,” anasema Mohamed aliyedumu kwenye soko hilo tangu 2003.

Hata hivyo, Shukuru Dikala ambaye ni kiongozi wa wafanyabishara sokoni hapo anasema changamoto ni wafanyabiashara kujaa hadi kwenye njia muhimu za kuingia sokoni.

Kizmba cha taka zilichoonekana kujaa kwenye soko la Buguruni na kuwalazimu watumiaji kuweka taka pembeni. Nyuma ya kizimba hicho ni biashara ya mama ntilie.

“Njia ile pale imejaa wafanyabiashara na imeongeza adha kwenye kushusha mizigo,” alisema.

Kwenye njia hiyo kuna wafanyabiashara waliojenga vibanda vya muda takriban 20.

“Halmashauri inaangalia mapato tu bila kuangalia ufanisi wa kazi. Pale magari yanalazimika kupita upande mmoja.”

Tatizo jingine linaibuliwa na Kashinde Rajabu, mfanyabiashara soko la Tazara – Veterinary juu ya miundombinu ya maji na vyoo huku Mashaka Juma, mtumiaji soko la Temeke Sterio akisema, “tatizo kubwa hapa ni msongamano wa wafanyabiashara na watu, nyakati za asubuhi inahatarisha usalama, unaweza kuibiwa.”

Mama Lishe kwenye  soko la Kigamboni Feri, Mwamvita Hamisi anasema pamoja na miundombinu kuboreshwa bado wana changamoto ya wateja.

“Wateja ni wachache japo sio kipindi hiki tu, kwa sasa miundombinu mingi ipo vizuri hata maji tuna sehemu ya kumwaga na hayatuami sokoni,” anasema.

ASkizungumzia hali ilivyo kwenye Soko la Mabibo maarufu ‘mahakama ya ndizi’, Ofisa Mfawidhi Biashara na Masoko wa Manispaa ya Ubungo Peter Malaga anasema “halikuwa chini ya manispaa mpaka Machi mwaka huu ndipo limerudishwa.”

Malaga anasema zaidi ya miaka mitano soko lilirudishwa kwa wafanyabiashara na walikuwa wanaliendesha wenyewe.

“Baada ya manispaa kujiridhisha uendeshaji wakehauridhishi licha ya kodi zinazokusanya, Machi mwaka huu soko lilirudishwa kwa manispaa,” anasema.

Ofisa huyo anaongeza kuwa katika kipindi hicho wamelikarabati soko kwa kuongeza shedi kubwa yenye uwezo wa kuchukua zaidi ya wafanyabiashara 300 na kizimba cha pili cha kukusanyia taka.

“Makati uliopo ni kuboresha barabara za ndani ya soko, kuongeza lenye paa na miundombinu ya maji. Katika mwaka ujao wa fedha (2024/25) tumetenga Sh100 milioni kwa ajili masoko yaliyopo kwenye manispaa na Mabibo lipo kwenye mkakati,” anasema.

Akizungumzia soko lililoboreshwa la Mburahati kukosa wafanyabiashara, Malaga anasema tangu wakati wa maboresho ya soko wafanyabiashara walitawanyika maeneo tofauti na wengi hawajarudi.

“Tuna amini watarudi au watakuja wengine kujaza soko kwa sababu kuna miundombinu wezeshi,” alisema.

Kwa upande wa Temeke, Ramadhani Gurumukwa, mkuu wa Idara wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, anakiri changamoto za miundombinu kwenye baadhi ya masoko ya manispaa hiyo, hasa lile la sterio lakini hali hiyo inadhibitiwa.

“Kila mwaka lazima tutenge bajeti ya ukarabati wa miundombinu na ukarabati unatanguliza maeneo korofi kwenye soko. Ukarabati unaofanyika ni wa muda na sio wa kumaliza matatizo ya soko” alisema.

Akitaja maadhi ya maeneo yenye changamoto, anasema kwa soko la Sterio tatizo ni sakafu ambayo husababisha maji kutuama, shedi kwenye maeneo mengi hasa kwenye kitengo cha nyanya, vizimba vya taka na vyoo.

“Haya tunayafahamu ndio maana mwaka uliopita ilitengwa Sh800 milioni kuboresha miundombinu. Sterio imeboreshwa kiasi fulani, Veterinary kama unakumbuka pale kulikua kunajaa maji mvua ikinyesha hata kidogo tu, lakini sasahivi hakuna, anafafanua.

Ofisa biashara Manispaa ya Kigamboni Hassani Pongwa anasema masoko mengi ya wilaya hiyo yamerithiwa kutoka manispaa ya Temeke miaka saba iliyopita nab ado ni madogo kwa maeneo na idadi ya wafanyabiashara.

“Masoko mengine ni makubwa lakini bado hakuna wafanyabiashara wengi kwa sababu maeneo mengi ya huku bado yanakua,” alisema akimaanisha kuwa wilaya hiyo bado ni mpya.

Hata hivyo anasema katika mwaka wa fedha uliopita walitenga Sh18 milioni kwa ajili ya ukarabati wa soko la Kigamboni – Ferry ambalo lilikuwa na changamoto za mfumo wa maji na mpaka sasa ukarabati unaendelea.

 “Kwenye masoko mengine na maeneo ya biashara tunaboresha miuondombinu ya barabara na vyoo, lakini kwenye mikakati ya muda mrefu tunaendelea na tathmini ya maeneo kwa kushirikiana na wadau ili tujenge soko kubwa la kisasa kwa manispaa.”

Tegeta Nyuki na Kawe yapo kwenye mikakati ya maboresho, kwa mujibu wa Goodluck Kabage, ofisa masoko Manispaa ya Kinondoni.

“Kwa mfano hilo soko la Tegeta Nyuki na Kawe. Kuna mikakati inafanywa kupitia benki ya dunia, yapate ufadhili na kuyafanya yawe masoko ya kisasa.”

Aliongeza kuwa masoko hayo hayapo kwenye mpango wa awamu ya pili ya Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP II), lakini wamefanya tathmini kwa masoko hayo na wanashirikisha wadau.

“Soko la Tegeta Nyuki tulishaandaa na michoro na wadau walishirikishwa kuliona hilo. Linatarajiwa kujengwa jipya la viwango,” anasema.  

Katika Manispaa ya Ilala, Mchumi Julius Ndele anasema yapo masoko yaliyojengwa na kuboreshwa na mengine yana miundombinu ya kitambo. Akitaja soko la Ilala Boma Ndele alisema limezidiwa na kuna ongezeko kubwa la mahitaji.

Ndele anasema wafanyabiashara waliopo ni mara tatu zaidi ya uwezo wa soko na manispaa inatambua hilo.

“Watu wachache ndio wapo kwenye vizimba na ukiangalia eneo rasmi la soko lina shedi ila kuzunguka eneo hilo kuna vibanda vingi na mwingiliano kwenye nyumba za watu. Pia miundombinu ni ya zamani”.

Katika maeneo mengine alisema, “Yapo maeneo ambayo hayakupangwa lakini yanatumika kama masoko. Mfano eneo la Gongo la Mboto watu wamekusanyika ila hakuna soko”.

Ndele anasema hayo wanayatambua ndio maana manispaa imekamilisha hatua zote muhimu za ujenzi wa masoko mapya.

“Soko la Ilala Boma tumemaliza tathmini na tutajenga soko jingine palepale ambalo litakuwa na ghorofa tano, mbili za chini (maegesho na kuhifadhi mizigo) na nyingine za biashara, litagharimu Sh30 bilioni na ujenzi utaanza mwaka ujao wa fedha.

Ndele aliyasema hayo akionyesha michoro mbalimbali na picha jongefu za soko hili litakavyokuwa. Pia alisema soko la Mchikichini (Karume) litajengwa kwa Sh40 bilioni na Gongo la Mboto ambapo hakuna soko rasmi wamefanya utambuzi wa eneo na litajegwa soko kwa Sh15 bilioni ili kutoa adha kwa watumiaji wa barabara.

Alipoulizwa kuhusu ufanisi wa masoko yanayojengwa kutokuwa na wateja alisema,”Tumefanya upembuzi yakinifu na kujifunza kutoka kwa masoko mengine kama la Job Ndugai na Magomeni na tumejipanga kufanya kitu cha tofauti”.

Itaendelea kesho tukiangazia fursa iliyojificha kwenye taka zilizosheheni kwenye masoko na dampo.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts