Utouh: Uwaziri unasahaulisha majukumu ya ubunge majimboni

Dar es Salaam. Kigezo kinachotaka mtu anayeteuliwa kuwa waziri lazima awe mbunge kimetajwa kusababisha mawaziri wengi kusahau wajibu wao wa kutumikia muhimili wa Bunge, badala yake wanaitumikia Serikali pekee.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu Ludovick Utouh, kigezo hicho kinamlazimu mtu mmoja kuwajibika kwa mihimili miwili, yaani Serikali na Bunge, jambo ambalo linakuwa si rahisi.

Utoh ambaye pia ni mkurugenzi wa Taasisi ya Wajibu, ameyasema hayo leo Jumatano, Julai 24, 2024 katika mahojiano yake na kipindi cha redio Clouds Fm.

Iwapo mbunge ameteuliwa kuwa waziri, amesema anajikuta katika mkanganyiko wa kutumikia mihimili miwili – Bunge na Serikali, huku akiwajibika kwa waliomchagua na aliyemteuwa.

Na kwa sababu marupurupu ya uwaziri ni mengi kwa mujibu wa Utoh, mara nyingi mawaziri wanajikuta wakisahau wajibu wao wa kuzitumikia nafasi zilizowapa kigezo cha kuwa mawaziri.

“Unapokuwa waziri kuna marupurupu ya uwaziri na ambayo yako vizuri zaidi kuliko mtu kuwa mbunge wa kawaida, na kibinadamu penye masilahi wakati mwingine panakupa kujisahau.

“Unapochaguliwa kuwa mbunge unatumikia muhimili wa Bunge, lakini unapoteuliwa kuwa waziri unafanya kazi ya muhimili wa Serikali, mara nyingi kuna kujisahau ukasahau huu muhimili ambao umekufanya uwe waziri,” amesema.

Utouh amesema kuliwahi kuwepo fikra za kufanyika mabadiliko kwenye eneo hilo, hiyo ilikuwa ndani ya rasimu ya mabadiliko ya Katiba wakati wa mchakato wa mchakato ulioongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Katika mapendekezo hayo, amesema wananchi walitaka kuondolewa ulazima wa kuwa mbunge kama kigezo cha kuteuliwa kuwa waziri.

Pendekezo hilo lilienda sambamba na kile alichoeleza, kama kungetokea ulazima wa mbunge kuteuliwa kuwa waziri, alipaswa aachie nafasi moja ili atumikie uteuzi kwa ufanisi.

Hata hivyo, baada ya Bunge Maalumu la Katiba, ibara ya 116 (1) (d) iliendelea kusisitiza kuwa mtu anayeteuliwwa kuwa waziri au naibu waziri lazima awe “ni mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.”

Akisisitiza kuhusu ufanisi, Utouh amsema: “Inapokuja kwenye ufanisi, lazima utaingiliwa kidogo kwa sababu majukumu ya uwaziri ni mazito na kazi za muda wote, kama ilivyo kwenye uwakilishi, lakini tunakwenda kwa mfumo uliopo kwenye Katiba.”

Hata hivyo, amesema kwa kuwa utaratibu uliopo sasa unataka hivyo, mawaziri waliopo wanapaswa kuwatumia vema wasaidizi wao kuwawakilisha majimboni.

Related Posts