Gofu Mombasa yabeba watano Tanzania

WACHEZA gofu wanawake kutoka Tanzania wameanza kujifua kwa ajili ya mashindano ya mchezo huo yatakayochezwa katika viwanja vitano tofauti katika miji ya Mombasa na Malindi nchini Kenya mwanzoni mwa mwezi ujao.

Mashindano hayo yatashirikisha wachezaji watano wa kike kutoka klabu za Arusha Gymkhana, TPDF Lugalo na Kili Golf  ya Arusha, kwa mujibu wa katibu wa Chama cha Gofu kwa Wanawake tanzania (TLGU), Rehema Athumani.

Wachezaji watakaoshiriki mashindano hayo ni pamoja na Vicky Elias ambaye hivi karibuni alishika nafasi ya nane kati ya wachezaji 48 walioshiriki mashindano ya wazi ya Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita.

Wengine ni Yasmin Challi ambaye alishiriki Zambia Open, Loveness Mungure kutoka Kili Golf ya Arusha, Neema Olomi wa Gymkhana (Arusha) na Shaz Myombe (Dar es Salaam).

Rehema alisema mashindano hayo yataanzia katika viwanja vya Vipingo, Mombasa, Agosti 5, mwaka huu na baadaye kuhamia viwanja vya Nyari, Mombasa Club, Leisure Lodge na Malindi.

“Nimepiga zoezi la kutosha kwa kucheza na kufanya vizuri katika mashindano ya Lina PG Tour na Arusha Open. Naamini  mazoezi haya yameniweka vizuri kwa mashindano ya viwanja vingi yatakayofanyika Mombasa na Malindi,” alisema Vicky.

Kwa miaka mingi wachezaji wa kike kutoka Tanzania wamekuwa wakishiriki na kufanya vizuri katika mashidano ya mialiko nchini Kenya.

Madina Iddi wa Arusha ndiye mwenye rekodi ya kufanya vizuri katika mashindano mengi ya nje ya nchi yakiwemo hayo ya Mombasa ambayo mwaka jana alimaliza wa pili.

Yasmin Challi, ambaye mwanzoni mwa mwezi huu alishiriki  mashindano ya wazi ya wanawake nchini Zambia ameahidi kuwawakilisha vyema Watanzania nchini Kenya.

“Naamini sisi sote tutafanya vizuri baada ya mazoezi ya kutosha kupitia mfululizo wa michuano ya Lina PG Tour na mingineyo,” alisema.

Naye Neema pia ana uzoefu wa kutosha wa mashindano ya kimataifa, ambapo ushindi wake mkubwa aliupata katika mashindano ya kimatafa ya wanawake ya Uganda Ladies Open  ambako alishinda 2022.

Related Posts