Umeme jua unavyoweza kuleta kicheko kwa wakulima

Mbeya. Matumizi ya teknolojia ya umeme jua maarufu katika kilimo, imetajwa kuwa suluhisho katika uzalishaji wa tija, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukwepa gharama kubwa za uendeshaji.

Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini imekuwa kinara katika shughuli za kilimo ikitajwa kutoa mchango mkubwa wa chakula kitaifa na kimataifa haswa kwa nchi za ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Pamoja na mchango huo, wakulima wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali zikiwamo athari za mabadiliko ya tabianchi zinazowakosesha uzalishaji wenye tija.

Pia, gharama za uendeshaji haswa kwa kutumia mashine za mafuta katika uwagiliaji zimekuwa zikitajwa kuwagharimu fedha nyingi wakulima wengi wenye kipato cha chini na kushindwa kufikia malengo.

Katika kuondoakana na changamoto hizo, kwa sasa mkoani baadhi ya wakulima wameanza matumizi ya umeme wa sola kama mbadala wa kukabiliana na changamoto shambani.

Mmoja wa wakulima, Wilson Kihwele amesema kabla ya kuanza matumizi ya umeme jua alikuwa akitumia kati ya Sh840,000 hadi Sh900,000 kwa ununuzi wa mafuta, jambo ambalo sasa limeisha.

Amesema pamoja na kwamba ni muda mfupi ameanza kutumia teknolojia hiyo, matarajio yake ni kuzalisha kwa wingi na kwa tija kwa kuwa ameanza kuyaona matokeo kwenye kupunguza gharama.

“Mkulima yeyote hasa kwenye kilimo cha mbogamboga kazi kubwa iko kwenye umwagiliaji, wakati natumia mashine gharama zilikuwa juu na ninalazimika kutumia hadi Sh900, 000 kwa mwezi,” anasema na kuongeza:

“Lakini baada ya kufunga mtambo wa sola, nafanya kilimo kwa ufanisi na nimeona dalili nzuri, situmii nguvu, muda wala gharama za mafuta.”

Naye Helward Mbiligwe mkazi wa Mbarali, amesema tangu kuanza kutumia umeme huo kwenye umwagiliaji, ameona nafuu ya kilimo na usumbufu aliokuwa akipata umebaki historia.

Amesema matarajio yake katika kilimo cha nyanya, vitunguu, mihogo, matunda na mboga mboga ni kuzalisha kwa wingi na tija kutokana na mfumo mpya aliofunga.

“Awali, nilikuwa sivuki gunia 10 au 15, lakini mavuno ya hivi karibuni baada ya kuanza kutumia umeme wa sola, yamefika gunia 33 na ninaamini kwa mwenendo huu nitafikia mbali,” amesema Mbuligwe.

Mkulima huyo ameongeza kuwa licha ya gharama za manunuzi ya vifaa kuwa juu, lakini baada ya mtambo kufungwa faida ni kubwa, hahitaji kutumia gharama za ziada zaidi ya maji na jua.

Kwa upande Ismail Mwamafupa, mkulima wilayani Kyela anakiri matumizi ya umeme jua kumbadilishia maisha na mwenendo wa kilimo, akieleza tatizo la mabadiliko ya tabianchi yamepata mwarobaini.

“Kuna muda tulipigwa na kiangazi mazao yalikauka, lakini tangu mwaka jana tunaendesha kilimo chetu kwa raha, sababu sola inahitaji tu jua, nishauri wakulima wengine wahamie kwenye teknolojia hii,” amesema Mwamafupa.

Ameongeza kuwa kilimo cha mazao kama matikiti, ufuta, vitunguu na nyanya huhitaji umwagiliaji, hivyo teknolojia hiyo ni nyenzo mbadala katika kukabiliana na changamoto zake.

Mtaalamu wa kilimo kutoka jijini Mbeya, Adili Panja amesema matumizi ya sola kwa sasa ndio msingi wa kilimo hasa kwa maeneo ya vijijini ambako nishati ya umeme haijafika.

Anasema matumzi ya sola yana faida mbalimbali ikiwamo kukausha viungo kwa asilimia 70 kwa kila kirutubisho kwenye mazao, kwa sababu  hairuhusu kupenya kwa mionzi ya jua.

“Sola hairuhusu mionzi ya jua ukianika karafuu na mdarasini, ukianika juani inaondoa uhalisia hata kibiashara inakuwa ngumu.

“Utafiti unaonyesha asilimia 70-80 ya uanikaji mazao usio sahihi huathiri na hupoteza viinilishe, hivyo umeme wa sola husaidia kulinda mazao na mazingira,” anasema Panja.

Akizungumzia hilo, Profesa Chako Punnoose anasema kama ilivyo kwa dunia kubadilika kidigitali, hata maisha ya mimea nayo hubadilika, hivyo badala ya kutumia zana za kizamani lazima wakulima wabadilike.

“Kama maisha ya mwanadamu yalivyobadilika, mimea nayo inahitaji kwenda na teknolojia mpya, hizi sola ukiwa na uhakika wa maji na jiografia rafiki, kilimo kitapanda,” amesema Punnoose.

Mapinduzi hayo yameiamsha Serikali ikieleza kuungana na wakulima walioanza kuchangamkia matumizi ya teknolojia hiyo, kama anavyoeleza Bernad Libata, ofisa kilimo Mkoa wa Mbeya.

Anasema dunia ya sasa imebadilika na kila kitu kinaenda kidigitali, hivyo badala ya kuendelea na matumizi ya mashine za zamani lazima wakulima wabadilike ili kuzalisha kwa tija.

“Serikali inathamini wadau wa kilimo na tunaungana na waliotangulia kuanza matumizi ya sola katika shughuli hiyo, tunahitaji kuona wengi wakitumia teknolojia hii.

“Kwa sasa mwitikio bado ni mdogo ila tunaamini wengi wataanza matumizi haya baada ya matokeo ya wenzao, tunashughulikia miundombinu kuhakikisha mkulima anazalisha kwa tija na kunufaika,” anasema Libata.

Ofisa mmoja wa kampuni inayojishughulisha na umeme wa sola jijini Mbeya, Simon Kalawa amesema wanalenga kuwafikia zaidi ya wakulima 200 ili kuondokana na changamoto kwenye kilimo.

Related Posts