KUTOKA MAHAKAMANI: Aenda jela miaka minne kwa kumuua baba yake bila kukusudia

Arusha. Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Musoma imemhukumu kifungo cha miaka minne na miezi 10 jela, Mabula Mathias, mkazi wa Kiji cha Kasuguti Wilaya ya Bunda mkoani Mara baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua baba yake mzazi, Mathias Mashauri bila kukusudia.

Julai 5, 2024 Mathias alisomewa mashtaka hayo 2 na alikiri na akatiwa hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Akitoa hukumu hiyo, jana Jumanne Julai 23, 2024, Jaji Kamazima Kafanabo aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, amesema kwa mazingira ya kesi hiyo, pamoja na kukiri kwa mshtakiwa kutenda kosa, Mahakama imeona anastahili kupunguziwa adhabu.

Hivyo, Mahakama inamuhukumu Mathias kwenda jela kutumikia kifungo hicho cha miaka minne na miezi 10 kutokana na kosa hilo.

Akichambua mwenendo wa shauri hilo, Jaji huyo alieleza Aprili 14, 2022 katika Kijiji cha Kasuguti, baba yake Mathias akiwa amelala, mtuhumiwa alitoka nje ya nyumba waliyokuwa wamelala na kusukuma ukuta wa nyumba hiyo.

Amesema ukuta uliokuwa umedhoofishwa na mvua kubwa iliyonyesha, ulimwangukia Mashauri na kumsababishia majeraha makubwa na kutokwa na damu nyingi, kisha kifo chake.

Jaji alieleza kwa mujibu wa ripoti ya daktari, baada ya kuangukiwa na ukuta huo, marehemu alipata, majeraha yanayodaiwa kutokea zaidi kichwani na kusababisha kupoteza damu nyingi na hatimaye kifo chake.

“Mahakama hii pia inazingatia kuwa mshtakiwa alitoweka na kujificha kuanzia Aprili 4, 2022 hadi Mei 14, 2023 alipokamatwa na ndugu zake. Hii ina maana kuwa mamlaka husika zilitumia muda mwingi na rasilimali nyingine katika upelelezi hadi mtuhumiwa alipokamatwa,” amesema.

Mahakama imezingatia kuwa mshtakiwa alikiri kosa la kuua bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, hivyo aliokoa muda na rasilimali kwa upande wa mashtaka na mahakama.

Pia alieleza kuwa katika kesi hiyo, rekodi zinaonyesha mshtakiwa alikiri polisi wakati akihojiwa Mei 14, 2023 kuwa alitenda kosa hilo na alikiri tena Mei 22, 2023 mbele ya mlinzi wa amani.

“Pia imeelezwa kuwa mshtakiwa alikuwa rumande tangu siku alipokamatwa Mei 14, 2023 hadi Julai 19, 2024 ambayo ni zaidi ya miezi 14,” amesema Jaji.

Jaji Kamazima amesema kama ilivyoainishwa na sheria kuhusu adhabu ya kutenda kosa la kuua bila kukusudia, kifungu cha 198 cha Kanuni ya Adhabu kinatoa adhabu ya juu zaidi ya kifungo cha maisha jela, ila adhabu ya chini kabisa haijasemwa, inategemea busara ya mahakama.

Ameeleza mahakama baada ya kuzingatia sababu ikiwemo mshtakiwa kukiri kutenda kosa hilo akihojiwa polisi na pia mahakamani baada ya kusomewa maelezo ya awali, mahakama inampunguzia adhabu.

Jaji ameeleza kwa kuzingatia masuala mengine ikiwemo hoja za ungamo, mahakama hiyo ilimpunguzia adhabu na kwa kuzingatia alikaa mahabusu zaidi ya mwaka mmoja, imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka minne na miezi 10.

Hivyo, amesema: “Kutokana na mshtakiwa huyo kukiri kutenda kosa hilo alipokamatwa na kuhojiwa na polisi, mbele ya mlinzi wa amani na mahakamani wakati shauri likisikilizwa, mahakama inamhukumu mtuhumiwa kutumikia kifungo cha miaka minne na miezi 10 jela.”

Related Posts