Maelfu ya polisi kuwalinda Waisrael kwenye Olimpiki – DW – 24.07.2024

Katika hatua nyingine, polisi  wamemkamata mtu mmoja raia wa Urusi wakimtuhumu kwa kupanga kuvuruga michezo hiyo, hii ikiwa ni kulingana na ofisi ya mwendesha mashitaka, siku moja kabla ya michezo hiyo ya Olimpiki kuanza rasmi. 

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin amesema pamoja na mechi hiyo kati ya Israel dhidi ya Mali, katika uwanja wa Parc des Princes mjini Paris, mechi nyingine zitakazopewa kipaumbele cha usalama ni kati ya Ukraine na Iraq, itakayochezwa huko Lyon, kusinimashariki mwa Ufaransa.

Soma pia:Wanamichezo wakimbizi walenga kutimiza ndoto zao Paris 

Amekiambia kituo cha televisheni cha BFM na Radio RMC kwamba licha ya mechi zote kupangiwa ulinzi, lakini mechi hizi mbili zitazingatiwa kwa kiwango cha kupambana na ugaidi. Ameongeza kuwa uwanja huo utazungukwa na maelfu ya polisi hii leo watakaohakikisha ulinzi, hii leo, kila siku na kila wakati katika michezo hii ya Olimpiki.

“Ujumbe wa Israel ndio haswa utapewa ulinzi. Nilichukua uamuzi huu wiki mbili zilizopita kwa sababu tangu michezo ya Olimpiki ya Munich, ambako baadhi ya wanariadha  waliuawa, tumekuwa tunaichukulia kama suala nyeti, na hasa kutokana na hali ya kisiasa ulimwenguni inayowasababishia vitisho,” alisema Darmanin.

Ufaransa | Olimpiki 2024 | Michezo ya Olimpiki, Paris
Maafisa wa polisi wakifanya doria katika mtaa wa Place du Trocaderomjini Paris wakati jiji hilo likisubiri kuanza kwa michezo ya Olimpiki huku kukiwa na kitisho cha usalamaPicha: Takuya Matsumoto/AP Photo/picture alliance

Kundi la wanaharakati wa Ufaransa la Europalestine lililo nyuma ya maandamano ya hivi karibuni nchini humo, limeliambia gazeti la Guardian kwamba lilikuwa limeandaa maandamano ya amani ndani ya uwanja huo ya kupinga mauaji ya halaiki huko Ukanda wa Gaza.

Raia wa Urusi akamatwa kwa kutishia usalama

Katika hatua nyingine, polisi nchini humo wamemkamata raia mmoja wa Urusi anayedaiwa kujaribu kuvuruga michezo ya Olimpiki. Raia huyo wa miaka 40 alikamatwa jana Jumanne baada ya polisi kupekua nyumba yake kufuatia ombi la Waziri Darmanin na kukuta vidhibiti “vilivyowatia mashaka kwamba huenda ananuia kuvuruga michezo hiyo.” Mtu huyo amewekwa mahabusu na anaweza kufungwa hadi miaka 30 ikiwa atakutwa na makosa.

Uhusiano baina ya Ufaransa na Urusi umekuwa umeingia doa kwa miezi kadhaa wakati Rais Macron, anapoonekana kuwa mpinzani mkubwa wa uvamizi wa Urusi, huku akiiunga mkono pakubwa Ukraine.

Janga la UVIKO-19 nalo limeanza kuiandama michezo hiyo, baada ya wachezaji watano wa kikosi cha mpira wa majini cha Australia kuambukizwa virusi vya corona. Mkuu wa kikosi hicho Anna Meares amesema wachezaji hao wametengwa na wataweza kuanza tena mazoezi watakapopata nafuu.

Mbali na hayo yote, Rais Macron amedokeza juu ya uwepo wa msanii wa kimataifa Celine Dion katika sherehe za ufunguzi wa Olimpiki siku ya Ijumaa. Ameiambia Televisheni ya France 2 kwamba itakuwa ni habari njema sana ikiwa mwimbaji huyo maarufu kabisa duniani atakuwepo kwenye sherehe hizo. Fununu zinahanikiza kwamba Celine tayari yupo nchini humo.

Related Posts