Dar es Salaam. Licha ya historia nzuri na sifa lukuki za utendaji, alipokuwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), katika wadhifa wa Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania hali imekuwa tofauti.
Huu ndiyo uhalisia wa historia ya Maharage Chande katika kuzitumikia taasisi za umma tangu Septemba 2021 alipotoka sekta binafsi.
Safari ya Chande katika mashirika ya umma ilianza Septemba 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alipomteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco.
Kuingia kwake Tanesco, kulimfanya awe mmoja wa wakurugenzi waliopata kusifiwa na mkuu huyo wa nchi, hasa kwa kile kilichoitwa mageuzi ya kidigitali ndani ya shirika hilo.
“Mwezi uliopita nilishiriki mkutano wa Posta pale Arusha nikakuta maendeleo makubwa kwa upande wa Posta yetu wanakwenda kidigitali na nikajua hayo ndiyo maeneo yako (Chande).
“Kwa hiyo kwa sababu ni maeneo yako na nimemkuta kijana mzuri wa Posta ya kidigitali nikaona ninyi mkiwa pamoja mtafanya kazi nzuri, kwa hiyo nenda kamsaidie mkuze Posta yetu iende kidigitali,” alieleza Rais Samia baada ya kumwapisha Chande katika wadhifa wa Posta Masta Mkuu.
Sifa na matarajio hayo yamefifia Julai 23, 2024, baada ya taarifa ya utenguzi wa Chande katika wadhifa wake pamoja na watendaji wengine katika taasisi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, waliotenguliwa ni Chande, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Peter Ulanga na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba.
Mbali na hao, wengine waliotenguliwa ni, wenyeviti wa bodi za wakurugebzi, Profesa John Nkoma wa UCSAF, Zuhura Muro wa Tanesco na Brigedia Jenerali mstaafu, Yohana Mabongo wa Shirika la Posta Tanzania.
Julai 31, 2023 aliyekuwa Waziri wa Nishati, January Makamba kupitia kongamano la Mwananchi Jukwaa la Fikra kwa ushirikiano na Tanesco, alieleza uteuzi wa Chande na Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco haikuwa rahisi, lakini alijenga hoja kwa Rais Samia na akaeleweka.
Alisema kabla ya uteuzi wa Chande alikuwa na mahojiano naye, alimuuliza akipewa Tanesco ataifanyia nini na majibu yalikuwa ni kuanza na watu (wafanyakazi wa Tanesco) kisha wateja.
Makamba alisema: “Baada ya hapo nilikwenda kumuona Rais (Samia Suluhu Hassan) nikamuambia nadhani tumepata mtu sahihi ambaye atatusaidia,” alieleza.
Ziliposalia siku mbili ili Chande atimize miaka miwili ndani ya shirika hilo, Septemba 23, 2023 Rais Samia alimteuwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL akichukua nafasi ya Peter Ulanga ambaye angepangiwa majukumu mengine.
Kwenye nafasi hiyo, Chande alidumu kwa siku mbili pekee ambapo Septemba 25, 2024 aliteuliwa kuwa Posta Masta Mkuu akichukua nafasi ya Macrice Mbodo ambaye atapangiwa majukumu mengine.
Majukumu ya uongozi wa TTCL yalirejeshwa kwa Peter Ulanga huku Rais Samia akieleza sababu ya panga pangua hiyo ndani ya muda mfupi.
Septemba 26 2023 katika uapisho wa viongozi mbalimbali Ikulu, Dar es Salaam, Rais Samia amesema amegundua kuwa kiongozi huyo alikuwa na biashara ndani ya TTCL.
“Tumekutoa Tanesco na nikachukua uzoefu wako nikaona TTCL ingekufaa zaidi lakini baadaye nikagundua una biashara ndani ya TTCL na kwa sababu kampuni inafanya vizuri.
Ndio maana imemuwezesha kijana (Peter Ulanga- Mkurugenzi Mkuu wa TTCL) kufanya vizuri, nikasema hapana usiende sehemu ambayo una biashara itakuwa conflict of interest nikaona sasa nikupe Posta Masta Mkuu,” amesema Rais Samia.
Kitendo hicho, kilimuweka Chande kwenye orodha ya watendaji wakuu wa taasisi za umma waliohudumu kwa muda mfupi katika nafasi zao akiwemo Thobias Richard aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Aprili 4, 2021 na kisha kufutwa kazi siku moja baadaye.
Katika elimu, mwaka 1996 hadi 1999 Chande alipata shahada ya kwanza ya masuala ya umeme na sayansi ya mawasiliano ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Baada ya kumaliza chuo kikuu, mwaka 1999 aliajiriwa chuoni hapo kama meneja msaidizi wa masuala ya ufundi hadi kufikia Machi 2000.
Chande aliondoka kwenye nafasi hiyo na kujiunga na Benki ya Standard Charted kama Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Teknolojia kuanzia Machi 2000 hadi Aprili 2004.
Safari yake haikusishia hapo, mwaka 2004 Kampuni ya simu za mkononi Vodacom PLC ilimuajiri kama mkuu wa kitengo cha teknolojia na habari.
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2008 alikwenda masomoni Afrika Kusini akichukua shahada ya uzamili nafasi ya uongozi katika biashara Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (Universiteit van Suid-Afrika).
Wakati huohuo, mwaka 2007 Kampuni ya simu za mkononi Vodacom PLC ilimpandisha cheo na kuwa msimamizi mtendaji katika idara ya habari na teknolojia hadi 2010 mwaka ambao huduma yake ilikoma.
Baada kumaliza mkataba wake na Vodacom PLC, Benki ya Taifa ya Biashara ABSA/Barclays ilimfungulia milango Chande kwenda kuhudumu kwa nafasi Mkuu wa Uendeshaji kuanzia 2010 hadi 2014.
Utumishi wake katika benki hiyo uliokoma mwaka 2014 na kuingia serikalini, akiajiriwa kwa nafasi Mkurugenzi wa utoaji huduma ofisi ya Rais kuanzia 2010 hadi 2014 alipochia nafasi hiyo.
Huo ndio mwanzo wa kuajiriwa kama Mkurugenzi Mtendaji, Juni 2016 hadi Juni 2018 alihudumu katika Kampuni ya Multichoice Tanzania na baadaye akahudumu nafasi ya juu zaidi kama Mkurugenzi wa Kampuni ya Multichoice Kusini na Magharibi mwa Afrika Juni 2018.
Ulanga alisoma shahada ya kwanza ya uhandisi Chuo Kikuu cha Dar es Salam kuanzia 1992 hadi 1996 na 2004 hadi 2005 alitimkia nchini Australia katika Chuo Kikuu cha Southern Queensland akibobea kwenye usimamizi wa biashara.
Vilevile alipata shahada yake ya pili ya uzamili katika sayansi Chuo Kikuu cha Essex ya nchini Uingereza.
Kwenye utumishi wake serikalini mwaka 1996 hadi 2002 aliajiriwa kama Mhandisi Mkuu, Meneja Ufundi Kampuni ya Mawasiliano Tanzania TTCL.
Pia, mwaka 2002 hadi 2009 aliajiriwa kama Mhandisi Mkuu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na baadaye kuhudumu kama Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuanzia Julai 2009 hadi Juni 2019.
Baada ya hapo, alijiunga na Benki ya Maendeleo Afrika kwa mwaka mmoja akihudumu kama mshauri wa masuala ya uchumi wa kidigitali kuanzia Januari 2020 hadi Desemba 2020 na baadaye kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL. Kwa sasa Ulanga ni Mkurugenzi wa Bodi ya Usajili ya Wahandishi (ERB).
Justina Mashiba ambaye Rais Samia ametengua uteuzi wake Julai 23,2024 akiwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF aliwahi kuwa Mkuu wa ushauri wa masuala ya kisheria Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanzia mwaka Aprili 2001 hadi Aprili 2011.
Julai 2011 hadi Julai 2011 Mashiba alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria Wakala ya Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) na mwaka 2019 hadi Julai 2024 alihudumu kama Ofisa Mtendaji Mkuu UCSAF.