Mapya yaibuka kesi ya mirathi ya Hans Poppe

BAADA ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Z. H. Poppe Limited , Caeser Hans Poppe na mwanae Adam Caeser HansPoppe, kujisalimisha wenyewe Mahakama Kuu iliyopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia (IJC), Temeke.

Watoto wa Zacharia Hans Poppe, wamewasilisha maombi katika mahakama hiyo, wakiomba mambo matano likiwemo la wakurugenzi hao kuwasilisha mahakamani hapo, nyaraka mbalimbali za mikopo waliyochukua kwenye taasisi za fedha kupitia kampuni hiyo hadi sasa na mikataba ya kusafirisha mafuta nje ya nchi pamoja na mikataba ya upangishaji wa hoteli ya Zacharia Hans Poppe iliyopo Iringa.

Watoto hao, Angel, Abel ambao ni wasimamizi wa mirathi, katika kesi ya mirathi ya Zacharia HansPoppe namba 177/2022, iliyopo Mahakamani hapo.

Shauri hilo linalosilikizwa na Jaji Glady’s Nancy Barthy, liliitwa kwa ajili ya Mahakama hiyo kujua iwapo amri iliyotoa ya kukamatwa Caeser Adam  kama imefanyiwa kazi.

Hatua hiyo inatokana na mahakama hiyo, kutoa hati ya kukamatwa kwa Caeser na Adam na kupelekwa hapo ili washtakiwe kwa kosa la kuidharau na kushindwa kufika mahakamani hapo Julai 5, 2024

Caeser, mdogo wa Zacharia Hans Poppe aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, alitakiwa afike mahakamani hapo siku hiyo, lakini hakufanya hivyo na ndipo mahakama hiyo ilipotumia mamlala yake.

Wakurugenzi hao walitakiwa kufika mahakamani hapo, ili watoe taarifa za mapato na matumizi pamoja na orodha ya mali alizoacha marehemu ambazo wanazisimamia wao kupitia kampuni za Zacharia, lakini hawakutokea siku hiyo

Hata hivyo, mapema leo, Caeser na Adam kupitia wakili wao kutoka kampuni ya Tan Law Africa, Peter Kibatala akisaidiana na Alphonce Nachipiangu, Gloria Ulomi, Rebecca Lyaka na Omari Msemo anayemwakilisha mleta maombi namba moja katika shauri hilo la mirathi (Aldo Hans Poppe) aliomba mahakama hiyo iondoe amri iliyokuwa imetoa mwanzoni mwa mwezi huu ya kuwakamata na isitekeleze amri iliyokuwa imeelekeza ya kuwashtakiwa kwa sababu wamefika mahakamani hapo wenyewe bila kukamatwa.

Jaji Barthy alikubaliana na ombi la Kibatala na kuondoa amri ilizokuwa imezitoa na kisha kuelekeza tarehe itakayopangwa na mahakama hiyo wakurugenzi hao na pamoja na wasimamizi wa mirathi siku hiyo wafike mahakamani hapo, bila kukosa.

“Naelekeza, wakurungenzi hawa na wasimamizi wa Mirathi tarehe itakayopangwa na mahakama hii wanatakiwa wafike bila kukosa” amesema Jaji Barthy.

Baada ya Jaji Barthy kutoa maelekezo hayo, alimpa nafasi mawakili wa waleta maombi katika shauri hilo, ambao ni Emmanuel Msengezi na Regina Helman kutoa taarifa ya shauri hilo la mirathi.

Wakili Msengezi alianza kwa kukumbushia ombi walilowasilisha tarahe iliyopita la kutaka Wakurugenzi hao waleta taarifa za fedha pamoja na orodha ya mali zilizopo katika kampuni hizo.

“Kwa niaba ya msimamizi wa mirathi namba mbili na tatu( Angel na Abel) ambao ni watoto  wa marehemu  Zacharia Hans Poppe, naomba nieleze kuwa Zacharia alikuwa anamiliki asilimia 90 za hisa katika kampuni ya Z.H.Poppe, hivyo watoto hao wanataki wateuliwe kuwa wasimamizi katika kampuni hiyo” amedai wakili huyo na kuongeza;

“Mheshimiwa Jaji, tarehe iliyopita tulileta maombi mahakamani hapa na katika maombi yetu ya msingi, tunaomba wasimamizi hawa waweze kuteuliwa ili waweze kuingia kama wakurugenzi wa kampuni ili waweze kusimamia maslahi ya kampuni na hisa zilizopo.”

Msengezi amedai kwa bahati mbaya Mkurugenzi aliyopo katika kampuni hiyo (Caesar) hakuwahi kuwateua wasimamizi hao wa mirathi kuwa Wakurugenzi wenza katika kampuni hiyo, na hivyo kuendesha kampuni peke yake au na mtoto wake (Adam), ambaye anadaiwa kumteua bila kuwashirikisha wasimamizi wa mirathi namba mbili na tatu ambao ni watoto wa marehemu Zacharia Hans Poppe.

Amedai, hali hiyo ipo pia katika kampuni ya Hans  Poppe Holders Ltd, ambapo marehemu Zacharia  Hans Poppe alikuwa anamiliki  asilimia 28 za hisa zote zilizokuwa katika kampuni hiyo.

“Kutokana na wateja wetu hawa kutokushirikishwa katika kampuni hiyo, tunaomba Mahakama ielekeze Caeser Hans Poppe  na Adam Caeser Poppe, walete taarifa ya benki( Bank Statement) ya kampuni ya Z.H.Poppe Limited pamoja na Hans Poppe Holder Limited za tangu Zacharia Hans Poppe afariki dunia hadi sasa,” amedai Wakili Msengezi

Wakili Msengezi ameendelea kudai kuwa, wateja wake wanataka Wakurugenzi hao wawasilishe nyaraka na barua mbalimbali za mikopo waliyochukua kutoka katika taasisi za fedha mpaka sasa, ambayo wanadai walichukua katika benki ya BOA, Equity Eco, na TCB banki

“Pia tunaomba walete mikataba ya makubaliano ya upangishaji kwa wapangaji katika jengo la Hotel iliyopo Iringa.”

Wakili huyo aliendelea kudai kuwa Wakurugenzi hao wanatakiwa pia wapeleke mahakamani hapo orodha ya makubaliano ya eneo la kituo cha mafuta( Petrol Station) kilichopo Visiga, ambalo imepangishwa kwa kampuni ya mafuta ya Puma.

“Mheshimiwa Jaji, lengo letu ni kuangalia mapato na matumizi ya fedha ambazo zimeandaliwa kwa kipindi hicho na hawa wahusika ambao ni Wakurugenzi,” amedai 

Vile vile wakili Regina Helman anayemwakilisha mtoto mkubwa wa marehemu Zacharia Hans Poppe, Analisa Zacharia Poppe ameomba mahakama hiyo, ielekeze Wakurugenzi hao wawasilishe mkataba wa mauziano ya gari aina ya Toyota Nissan Patrol, ambayo iliuzwa bila wasimamizi wa mirathi kushirikishwa.

Vile vile mawakili hao waliomba Caeser na Adam wawasilishe mkataba wa makubaliano ya  usafirishaji wa bidhaa za mafuta walioingia na kampuni ya mafuta ya Engen Petroleum dhidi ya Kampuni ya Z.H. Poppe ya kupeka mafuta DR Congo.

Wakili Msengezi na Helman, baada ya kumaliza kuwasilisha maombi hayo, Wakili Kibatala alipewa nafasi ya kujibu hoja hizo.

Kibatala awasilisha maombi madogo

Baada ya maelezo hayo, Wakili Kibatala amedai, hawaoni msingi wa maombi yaliyofanywa na waleta maombi katika kesi hiyo ya kuwataka Wakurugenzi hao wawili wa kampuni za Zacharia HansPoppe kupeleke kile kilichoombwa mahakamani bila kuzihusisha kampuni zenyewe.

Kibatala ameeleza mahakama kuwa amewasilisha maombi madogo namba 1671/ 2024 mahakamani hapo akiomba mali zote zinazohusiana na Kampuni ya Z.H.Poppe Limited zisijadiliwe mahakamani hapo katika kesi hiyo ya mirathi namba 177 ya mwaka 2024 ya Zacharia HansPoppe kwa sababu kuna kesi nyingine inaendelea Mahakama Kuu.

Kibatala amedai kuwa, maombi hayo ameshayawasilisha rasmi mahakamani hapo kwamba yanatakiwa kujibiwa na upande wa pili (waleta maombi) kwa kiapo kinzani na wapeleke ushahidi ili mahakama hiyo iweze kuwa na kumbukumbu sahihi.

“Vile vile, maombi ya kesi hii ya  mirathi ya Zacharia HansPoppe  yaliwasilishwa na  wasimamizi wawili ambao ni Angel Poppe na Abel Poppe, lakini msimamizi wa kwanza ambaye ni Aldo HansPoppe  hajaulizaa kama ameridhia? kwa sababu hawawezi kufanya jambo peke yao, lazima washirikishane,” amedai Kibatala.

Akijibu hoja za Wakili Kibatala, Wakili Msengezi amedai kuwa Aldo amekuwa akishiriki na kuhudhuria mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo na amesikia maombi ya wasimamizi wa mirathi na hajawahi kuyapinga.

Kuhusu kupeleka kiapo pamoja ushahidi, wakili Msengezi alisema Kibatala amehusisha kampuni moja tu na hajasema chochote kuhusu Z.H. P Ltd na HansPoppe Hotels Ltd, ambazo zinamilikiwa na marehemu Zacharia.

“Mheshimiwa Jaji, hapa Wakili wenzangu(Kibatala) hakuongelea kitu chochote kuhusu hisa zilizopo katika kampuni hizo mbili za Z.H.P Ltd na Hans Poppe Hotels Ltd, ambapo kwenye Z.H.P Limited, marehemu Zacharia HansPoppe anamiliki asilimia 90 ya hisa katika kampuni hiyo, huku kwenye HansPoppe Hotels Ltd anamiliki asilimia 28 ya hisa katika kampuni hiyo,” amedai Wakili Msengezi.

Hata hivyo, Msengezi amedai kuwa vitu walivyoomba mahakamani hapo vinahusu pia uendeshaji wa kampuni hizo na kwamba Caeser na Adamu wanahitaji kujua kwa sababu ni wasimamizi wa mali na wanawajibu wa kulinda mali za marehemu kama ilivyo kwa wasimamizi wengine, ambayo ni Abel na Enjoy.

Baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, jaji Barthy amewapa siku 14 kufanya majumuisho ya maombi hayo kwa njia ya maandishi na kisha kuahitisha kesi hiyo hadi Agosti 20, 2024 kwa ajili ya kutoa uamuzi.

Jaji Barthy amesema tarehe hiyo kutakuwa na maamuzi mawili; kutoa uamuzi maombi yaliyowasilishwa na Kibatala na kusikiliza kesi ya msingi.

Zacharia HansPoppe alifariki dunia, Septemba 10, 2021 katika Hospitali ya Aga Khan alikokuwa akipatiwa matibabu na mazishi yake yalifanyika Septemba 15, 2021 mkoani Iringa.

Hans Poppe atakumbukwa na wanachama na klabu ya Simba kwa ujumla kwa kuleta mafanikio makubwa ikiwamo uhamasishaji aliofanya baada ya kuteuliwa pia kuwa Mwenyekiti wa kundi la marafiki wa Simba ‘ Friend of Simba’ ambapo kundi hilo lilijizolea umaarufu mkubwa ndani ya klabu hiyo.

Related Posts