Wazazi wasimulia watoto wao walivyofariki kwenye ajali ya moto

Bukoba. Watoto wawili wa familia moja wamefariki dunia kwa ajali ya moto baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea. Mpaka sasa chanzo cha moto huo hakifahamiki.

 Ajali hiyo imetokea jana Jumanne, Julai 23, 2024 usiku, katika Kijiji cha Rwagati Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.

Watoto waliofariki dunia katika ajali hiyo ni Justa John (9) na Julietha John (4).

Kaimu kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera, Karata Ramadhani amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, huku Katibu wa Hospitali ya Wilaya Bukoba, Inocenter Ngowi akisema miili ya watoto hao imehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi.

Hata hivyo, tukio hilo ni mfululizo wa ajali za moto zinazoendelea kutokea mkoani Kagera, ambapo Aprili 25, 2024 watu wanne walifariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika ajali ya moto uliounguza nyumba waliyokuwa wanaishi.

Moto huo ulidaiwa kusababishwa na mafuta ya petroli yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye madumu ndani ya nyumba hiyo.

Tukio jingine la hivi karibuni lilitokea Julai 20, 2024, watu saba waliokuwa wamelala ndani ya nyumba ya kulala wageni ya West End walinusurika  kifo baada ya moto kuteketeza vyumba vyote sita vya nyumba hiyo iliyopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani humo.

Wazazi wasimulia tukio lilivyotokea

Akisimulia kwa uchungu tukio lilivyotokea leo Jumatano Julai 23, 2024 mama mzazi wa watoto hao, Nashiwati Bashiru (26) amesema awali alikuwa na watoto wake sehemu anayofanya biashara ndogondogo ikiwamo ya kuni nje kidogo na nyumbani kwake.

Amesema alipigiwa simu na mteja wake akimwambia yupo nyumbani kwake (Nashitwa) na anahitaji kuni, hivyo akarudi kumuhudumia.

Ameeleza kuwa  baada ya kumuhudumia, aliamua kuchukua ndoo na kwenda kuchota maji mtoni huku akiwaacha wanawe ndani ya nyumba na kuwasisitiza wasitoke.

“Watoto niliwaacha hapa nyumbani nikaenda kufuata maji mtoni wakati narudi nilihisi mwili kuchoka nikaamua kukaa chini ili nitulie, baada ya dakika chache niliinuka na kuendelea nikakutana na mume wangu akanisimamisha na kuniuliza huku akihema ametandwa na hofu kubwa.. akauliza watoto wako wapi? nikajibu nimewaacha nyumbani kisha akanijibu nyumba inauungua moto,” amesimulia mama huyo.

Akisimulia tukio hilo, baba mzazi wa watoto hao, John Paschal amesema alikuwa wa kwanza kufika nyumbani akitoka kazini na kukuta moto unateketeza nyumba yake ya vyumba vinne.

Amesema taarifa za moto alizipata akiwa kazini na wakati anarejea nyumbani akakutana na mkewe, akamuulizia kuhusu watoto akasema amewaacha nyumbani.

Amesimulia kuwa alikimbia mpaka nyumbani kwa kuwa mlango ulikuwa umefungwa hakufanikiwa kuufungua na wakati huo moto ulishakuwa mkubwa ukiwaka kila kona.

“Nilifika nyumbani nikakuta moto unateketeza nyumba taarifa za watoto wangu nilikuwa sijui kama wapo ndani mke wangu ndio aliniambia ila nakumbuka ndani ya nyumba zilikuwepo bati 20 mpya mifuko minne ya simenti chumba kingine kilikuwa na mizigo ya kuni imejaa pamoja na nyasi mizigo minne vyote vimeteketea,” amesema baba huyo.

Paschal amesema mtoto mmoja Justa alikuwa anasoma darasa la kwanza Shule ya Msingi Mubembe na mwingine aliyemtaja kwa jina la Julietha alikuwa hajaanza shule.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mubembe kata ya Kemondo, Zepheline Joseph amesema alipokea taarifa za uwepo wa ajali hiyo ya moto saa mbili usiku kutoka kwa wananchi waliokuwepo eneo la tukio.

Amesema alichukua uamuzi wa kuujulisha uongozi wa ngazi zote kuhusiana na ajali hiyo kabla ya kuelekea eneo la tukio.

“Mimi nilipofika pale nilikuta moto huo  umeteketeza nyumba nzima na nikaambiwa kuna watoto wawili pia wamefia ndani ya nyumba hiyo,” amesema mwenyekiti huyo.

Related Posts