Arusha. Baadhi ya waumini wa Dini ya Kiislamu jijini Arusha wameazimia kuliburuza Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) mahakamani, kwa wanachodai limevamia eneo lao la msikiti na kuanza ujenzi wa vibanda vya biashara bila ridhaa yao.
Eneo hilo la Msikiti wa Bondeni uliopo ndani ya kiwanja namba 478, Kitalu H na I jijini Arusha, linadaiwa kumilikiwa na Umoja wa Waislamu Mkoa wa Arusha (AMU), huku pia kukiwa na msikiti, jengo la ghorofa nne la Shule ya Sekondari ya Bondeni, maduka na eneo la wazi.
Akizungumzia hatua hiyo leo Jumatano Julai 24, 2024 jijini Arusha, Kaimu Katibu wa AMU, Mustapha Kihago amesema wamefikia uamuzi huo kwa kile alichodai kuwa Bakwata limekiuka taratibu na matumizi ya eneo lao.
Hata hivyo, Mwananchi Digital ilimtafuta Katibu Mkuu wa Bakwata Taifa, Sheikh Nuhu Jabir Mruma kuhusu hilo na amesema wako tayari kwa lolote ambalo AMU wanataka kulifanya.
“Kwanza hatuwatambui na hata umoja huo pia hatuutambui, lakini kama wapo wajue kabisa hakuna mali ya mtu mmoja mmoja, bali ni za Bakwata. Hivyo kama wanataka kwenda mahakamani waendelee na utaratibu wao na sisi tutakuja kujitetea na kuwasilisha ushahidi wetu huko huko mahakamani,” amesema Mruma.
Akizungumzia swala hilo, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shaaban Bin Juma amesema waliazimia kuwekeza vitega uchumi katika eneo hilo, ila kwa sasa wamesitisha kutokana na baadhi ya mambo kuingiliana (bila kuyataja).
“Nitatoa taarifa rasmi baadaye, kwa sasa niacheni kwanza kuna vikao vya ndani vinavyoendelea kujadili suala hili, tutakapokuwa tayari tutawajulisha,” amesema Sheikh Juma.
Awali, Kihago amesema “Bado kuna baadhi ya vitu na nyaraka tunakamilisha kwa mwanasheria wetu, kwa ajili ya kuliwasilisha jambo hilo mahakamani, tutafanya hivyo muda wowote kuanzia sasa,” Kihago.
Ameda kuwa eneo hilo ambalo waliliweka wakfu kwa ajili ya shughuli za kiibada, walishafanya mipango ya kujenga msikiti mwingine mkubwa kupitia wafadhili kutoka nchi za Uarabuni na Zanzibar, hivyo hawakubaliani na ujenzi holela wa majengo sambamba na vitega uchumi vingine.
“Hili ni eneo la ibada tu, ndio maana hata viongozi mbalimbali wa Serikali na kimataifa wakija Arusha wanaswali hapa, na mpango wetu ni kujenga msikiti mwingine ambao tayari mchoro ulishakamilika na tunasubiri majibu ya vipimo vya udongo kwa ajili ya kuanza ujenzi,” amedai kuongozi huyo.
Amesisitiza kuwa hiyo ndiyo sababu ya kutokubaliana na uamuzi wa Bakwata kujimegea ardhi hiyo na kuanza ujenzi wa vibanda katika eneo hilo.
Wakili wa AMU, Mustapha Akonay amesema suala hilo wanalifanyia kazi na wakati wowote wataliwasilisha mahakamani.