Aweso aagiza mhandisi Moruwasa asimamishwe kazi

Morogoro. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameiagiza Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani Morogoro (Moruwasa) kumsimamisha kazi Mkuu wa Kitengo cha Ufundi, Thomas Ngulika, kwa tuhuma za kusema uongo kuhusu sababu za baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Morogoro kukosa maji.

Aweso ametoa agizo hilo leo Jumatano, Julai 24, 2024, wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani humo, ambapo alikagua mitambo ya kusukuma maji, shughuli za uzalishaji maji, na kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa uboreshaji wa huduma ya maji Gairo.

Katika ziara hiyo, Aweso amezungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali ili kujua changamoto za maji wanazokutana nazo. Pia, amefanya kikao na watumishi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu.

Ngulika alimweleza Waziri Aweso kuwa alishakamilisha taratibu zote zinazohitajika kupata fedha za ukamilishaji ununuzi wa vifaa ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji iliyositishwa kwa takriban wiki tatu zilizopita.

Hata hivyo, baada ya Waziri Aweso kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa maeneo ya Nane Nane, Tungi, na Tubuyu hayana maji kwa zaidi ya wiki tatu sasa, hakuridhishwa na maelezo ya mhandisi huyo na hivyo akatoa agizo la kumsimamisha kazi.

Aweso amesema wizara haitakuwa tayari kumvumilia mtu yeyote atakayeenda kinyume na sheria katika kutekeleza wajibu wa kuwatumikia wananchi. “Sitovumilia na hatutokuwa tayari kuona mtu kwa makusudi anatoa taarifa za uongo wakati yeye ndiye anahusika kwenye hilo jambo.

“Eneo la Tungi, Nanenane na maeneo mengine wiki ya tatu hawana maji, mtendaji anaulizwa anaongea uongo kwa makusudi tu, haiwezekani. Mimi nitaanza na huyu mtu wetu anayehusika na masuala ya ufundi kwenye mamlaka hii. Hatufai, atupishe. Bodi ipo hapa, asimamishwe mara moja,” alisema Aweso.

Waziri Aweso aliongeza kuwa kuna baadhi ya watumishi ambao si waadilifu wanaofanya kazi kinyume na matakwa ya taasisi hiyo, kwa kuwaunganishia maji wateja bila kuwasajili kwenye mfumo wa ulipaji.

Akijibu shutuma hizo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Moruwasa, Kiguhe Benno, amesema alipokea malalamiko hayo na kuwaita watuhumiwa ambao ni wateja na kuzungumza nao kutaka kujua kama walifuata utaratibu wa kuwaunganisha na akawasamehe kwa makosa waliyoyafanya.

“Niliwaita na kuzungumza nao kutaka kujua orodha ya watu 12 ambao wanatumia maji bila kuunganishwa kwenye mfumo, na katika mahojiano hayo, Noha Sempambo, ambaye ni mtumishi wa Moruwasa, akatajwa kuwa ndiye aliyewaunganisha watu,” amesema Benno.

Noha Sempambo, mmoja wa mafundi wanaodaiwa kuwaunganishia maji wateja bila kufuata taratibu, amesema anashangazwa na yeye kutajwa kwenye orodha hiyo kwa sababu jukumu lake ni ufundi na si usajili.

“Sikutegemea kama ingefikia hatua hii. Mkurugenzi yupo, ofisa utumishi yupo, leo tunaitwa kwenye kikao na waziri sijui ni chuki au kitu gani mtu ananisingizia. Kama ni kweli tumewawekea wateja maji bila usajili, kazi ya usajili ni ya nani? Sio mimi. Kazi yangu ni ufundi, sijawaunganishia maji wateja ili wakwepe kulipa ankara, ila naomba radhi makosa haya hayatajirudia tena,” amesema Sempambo mbele ya Aweso.

Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amewataka wasimamizi na watendaji wa Bonde la Wami – Ruvu kutimiza wajibu wao ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (Moruwasa) kuhakikisha mazingira ya bwawa la Mindu, ambalo ni tegemeo la wananchi wa Morogoro, yanakuwa sawa.

“Huwezi ukaruhusu majani yamefika mpaka kwenye bwawa na leo tumekuja tumekuta makazi ya watu yanazidi kusogea katika chanzo hiki kikuu cha maji. Nafikiri tushirikiane sasa hii sio kazi ya mtu mmoja na nyie mkubali pia kushirikisha kwa sababu jamii ipo na viongozi wapo. Usipowashirikisha utakwama tu,” amesema Aweso.

Related Posts