Nyuki wa kishirikina wawashambulia watumishi wa Mungu Kanisa la TAG Kiomboi

Na Seif Takaza, Singida
Ukistaajabu ya Musa utayaona ya filauni, hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya nyuki wanaodaiwa kuwa wa kishirikina waliotumwa na wachawi kuwawashambulia watumishi wa Mungu wa Kanisa la TAG Kiomboi, linaloongozwa na Askofu Yonah Suleman Essya, baada ya maombi ya kutoa mapepo kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Igumo iliyopo wilayani Iramba, mkoani Singida.

Tukio hilo lilitokea hivi karibuni baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo kupokea taarifa kuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Igumo walikuwa wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na wachawi kuwatupia mapepo. Askofu Yonah Suleman Essya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani (Dini mbalimbali) wilaya ya Iramba, pamoja na jopo la watumishi wa Mungu, walifanikiwa kuwaondoa mapepo wanafunzi hao baada ya maombezi. Wakati wa maombezi, bundi watano, ambao inasemekana ni watu waliojigeuza kuwa bundi, walikamatwa.

Katika maombezi hayo, Mchungaji Yonah aliwaomba vijana wa kikundi cha maombi na maombezi alioambatana nao kuwaonyesha bundi hao hadharani. Ghafla, kundi la nyuki waliotumwa kishirikina lilijaribu kuwadhuru watumishi hao wa Mungu, lakini Askofu Yonah alifanya maombi na nyuki hao walitoweka.

Mmoja wa wanafunzi alipoibuka baada ya maombezi alisema, “Hao si bundi, ni binadamu waliojibadilisha kuwa bundi. Sisi wanafunzi sio wachawi, lakini bibi mmoja huja darasani akijibadilisha kuwa nyoka na wakati mwingine kuwa bundi. Tukimuona tunaanguka chini na kupagawa,” amesema mwanafunzi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa kwa usalama wake.

Mwanafunzi huyo aliongeza kuwa bibi huyo hataki watoto wa shule hiyo wasome na kufaulu mitihani yao, na baadhi ya wananchi wa kitongoji hicho hawataki maendeleo ya watoto wao katika elimu.

Askofu Yonah, baada ya wanafunzi hao kutolewa mapepo, aliwaeleza wazazi kuhusu faida ya elimu na kuwasihi kuwatekelezea mahitaji muhimu. “Ni kitu cha ajabu sana wachawi kuwafuata wanafunzi na kuwatupia mapepo ili wasiendelee na masomo. Wachawi wanapata faida gani?” alisema kiongozi huyo wa dini.

“Kwa sasa, watoto hawa wamepona. Sipendi watoto kudhulumiwa haki zao na kuharibu akili zao ili wasisome. Nawataka wazazi kuachana na tabia za kishirikina ili watoto waweze kuzifikia ndoto zao,” aliongeza Askofu Yonah. Pia, alisisitiza kuwa yeyote atakayeenda kinyume na sheria atachukuliwa hatua kali za kisheria kama alivyoagizwa na Mkuu wa Wilaya.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Igumo, Elisante Gyuzi, alisema kuwa wanafunzi wamekosa amani ya kusoma kwa sababu ya wachawi wanaowatupia mapepo. “Ni zaidi ya wiki tatu sasa wanafunzi hao wamekuwa wakiteswa na mapepo. Sisi walimu tunashindwa kufundisha kwa sababu ya hili. Wachawi hawapendi kabisa kuwepo na shule hapa,” alisema Mwalimu Gyuzi.

Shule ya Msingi Igumo inajivunia matokeo mazuri, imefikia asilimia 95% ya ufaulu, ukilinganisha na hapo awali. Mwalimu Gyuzi alitoa wito kwa wazazi kuachana na tabia za kishirikina ili watoto waweze kuzifikia ndoto zao.

Judith Laizer, Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi wilaya, alionyesha kusikitishwa na kitendo hicho na kuwataka wale wenye mchezo wa ushirikina kuacha mara moja. “Niko hapa kuhakikisha wanafunzi hawa wapo katika hali nzuri. Hao bundi waletwe tuwachome moto na kuwateketeza kabisa. Wazazi, wanafunzi hawa ni taifa la kesho. Inawezekana wakawa Rais, Mbunge, Daktari, Walimu, na fani nyingine. Tusifanye mchezo na maisha yao ya baadae,” alisema Judith Laizer.

Related Posts