Polisi yawashikilia watu 21 wakituhumiwa kwa uhalifu

Unguja. Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linawashikilia watuhumiwa 21 wakidaiwa kujihusisha na matukio ya wizi, uporaji na unyang’anyi wa kutumia mapanga.

 Watuhumiwa wamekamatwa baada ya polisi kufanya oparesheni maalumu ya kuwasaka watu wanaojihusisha na matukio ya uhalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 16, 2024 ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu amesema pia wamekamata mali iliyoibwa.

Kamanda Mchomvu amesema watuhumiwa wamekamatwa katika maeneo ya Fuoni, Kinuni, Nyarugusu, Pangawe, Kwarara, Tomondo, Mwanakwerekwe, Darajabovu, Bububu, Mtoni na Dole.

Amesema mali zilizokamatwa ni pikipiki tatu na simu tatu. Pia watuhumiwa walikamatwa wakiwa na mapanga manane na visu vidogo viwili.

Baadhi ya watuhumiwa wa uhalifu waliokamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharib]i, leo Aprili 16, 2024.  Picha na Zuleikha Fatawi

Kamanda Mchomvu ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi, ili kuhakikisha wanakomesha vitendo vya udhalilishaji na matukio mengine ya kihalifu kwa lengo la kudumisha amani.

“Jeshi linatoa onyo kwa yeyote atakayejaribu kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani, tutamkamata na kumchukulia hatua,” amesema.

Mkazi wa Bububu, Halima Ismail amesema katika maeneo wanayoishi kwa sasa wana hofu hasa usiku kutokana na kuwapo matukio ya wizi.

Amesema Jeshi la Polisi linapaswa kufanya oparesheni kila wakati ili kukomesha uhalifu unaoendelea.

Related Posts