Wawili wadakwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara Tabora

Tabora. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linawashikilia watu wawili wakituhumiwa kwa mauaji ya mfanyabiashara Magreth Mwaviombo, aliyeuawa Julai 13, 2024 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Julai 24, 2024 na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Richard Abwao akisisitiza kuwa jeshi hilo halijalala.

Amesema, “kutokana na tukio la mauaji lililotokea Julai 13 tunawashikilia watu wawili kwa kuhusika na mauaji hayo. Majina yao hatutayaweka hadharani kwa sababu za kiuchunguzi, na taratibu zinaendelea kuhakikisha wanafikishwa mahakamani.”

Ameongeza kuwa jeshi hilo halijalala na kuwa licha ya matukio kutokea, jitihada za kiintelijensia zinaendelea kuhakikisha wahalifu hawapati nafasi katika mkoa huo.

“Tumekuwa na mikakati ya kuhakikisha tunazuia uhalifu kwa kutumia doria, ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia na kuzifanyia kazi. Malengo ni kuzuia makosa kabla hayajatendeka na wakati mwingine yanapotokea, tunafanya upelelezi wa kina,” amesema Abwao.

Kuhusu matukio ya mauaji ambayo yametokea hivi karibuni mkoani hapa, amesema jeshi hilo lina maofisa wakaguzi katika kila kata, jambo ambalo linawapa urahisi wa kushughulikia uhalifu.

“Kwenye kata zote ambazo ziko hapa manispaa tumeweka askari, jambo ambalo linatusaidia kupata taarifa kwa urahisi na haraka. Jeshi linaendelea kufanya doria za mara kwa mara ili wanaohatarisha usalama wa watu waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Mkakati ni kuhakikisha tunakuwa salama na hakuna anayeweza kuleta hofu,” ameongeza.

Ufafanuzi huo, unafuatia madai ya baadhi ya wakazi wa manispaa hiyo, kuwa ndani ya miezi miwili na nusu kuna matukio matatu ya watu kuuawa kwa kupigwa na vitu vizito na wauaji wakitoweka bila kufahamika.

Hata hivyo, Abwao amesema hawatamvumilia mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani, badala yake watamchukulia hatua kwa kuwa Tabora si eneo la wahalifu kuhalalisha matendo yao.

Aidha, kamanda huyo amewataka wananchi katika maeneo yote ya mkoa huo kutoa taarifa za uhalifu zinapowafikia ili zifanyiwe kazi kwa haraka, ili kuhakikisha amani inatawala.

Mwananchi limezungumza na baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Tabora ambao wameeleza hofu waliyonayo kutokana na vitendo vya mauaji vilivyotokea hivi karibuni.

Rasul Mziwanda, dereva bodaboda anayefanya shughuli zake mjini Tabora, amesema analazimika kufanya kazi nusu siku.

“Kutokana na matukio ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni, imenifanya nifanye kazi zangu nusu siku na ikifika saa 12 jioni nawahi nyumbani kutokana na kuhofia usalama wangu. Lakini kama Jeshi la Polisi limeamua kutoka na kuwasaka wahalifu, naamini hali itatulia na nitafanya kazi zangu za kukesha kama hapo awali,” amesema.

Zuwena Rashid, mfanyabiashara katika Manispaa ya Tabora, amesema mauaji hayo yamezua  hofu kwa wananchi wengi.

“Vitendo vya uhalifu hapa Tabora viliwahi kutokea huko nyuma na mkoa wetu hofu ikawa kubwa. Polisi walifanya kazi ya ziada na hali ikatulia. Sasa baada ya muda naona kama tunarudi tulipotoka, lakini kwa kuwa polisi wameamua kuingilia kati, naamini amani itatawala na wahalifu watashughulikiwa ipasavyo,” amesema Rashid.

Related Posts