Fei Toto anavyomliza Nasreddine Nabi

KOCHA wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Nasreddine Nabi amesema bado anaumia moyoni kumkosa kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Akizungumza na Mwanaspoti akiwa Uturuki ambapo Kaizer imeweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya, Nabi alisema ana kiu ya kufanya kazi na wachezaji wa Kitanzania, lakini namba moja ni Fei Toto.

Alisema alijaribu kumshawishi Fei Toto ajiunge na timu yake hiyo mpya lakini uongozi wa Wasauzi hao wamemwambia matajiri wa Chamazi wanataka fedha nyingi. Azam inatajwa kuhitaji kiasi cha Sh2 bilioni kumwachia Fei Toto aliyebakiza miaka miwili kwenye mkataba na timu hiyo.

“Nampenda sana Fei Toto, unajua nawapenda Watanzania nilitamani mmoja awe kwenye timu yangu ili nisaidie kukuza vipaji nje ya hapo Tanzania,” alisema Nabi aliyewahi kufanya kazi na Fei Toto wakiwa Yanga.

“Nilipoona hitaji la kumsajili mchezaji akili ya kwanza ilikuja kwa Fe Toto. Nampenda sana nilitaka nije nifanye naye kazi ili akue zaidi. Bahati mbaya viongozi wa Kaizer wameniambia klabu yake imetaka fedha nyingi hakuna namna tena kwa sasa, “ alisema Nabi.

“Nilifurahia alivyofanya vizuri msimu uliopita kwa kukaribia kuwa mfungaji bora, sio kazi rahisi kupata mafanikio kama hayo ukiwa nje ya klabu kubwa mbili za Simba na Yanga.”

Akiwa Yanga, Nabi alimbadilisha Fei kuwa kiungo bora akifunga na kutoa asisti kwa kumpandisha kuwa kiungo mshambuliaji badala ya kiungo mkabaji.

Related Posts