Netanyahu aapa kuendelea na vita Gaza – DW – 25.07.2024

Kiongozi huyo ameshangiliwa na wanasiasa wengi kutoka chama cha Republican wakati akitoa hotuba yake katika bunge hilo, hotuba hiyo ikiwa yake ya nne ndani ya bunge la Marekani.

Netanyahu ametumia hotuba yake kwa bunge la Marekani kuwashtumu waandamanaji wanayoiunga mkono Palestina na kuwaita “wajinga wenye manufaa” wanaopokea ufadhili wa siri kutoka kwa Iran.

Amesema, “tunapopigana na Iran, tunapambana na adui muuaji zaidi wa Marekani. Vita vyetu ni vita vyenu, na ushindi wetu utakuwa ushindi wenu.”

Soma pia: Mashambulizi mapya yatikisa Ukanda wa Gaza

Hata hivyo, mgawanyiko wa kisiasa kuhusu vita vya Gaza ulijitokeza wazi wazi baada ya wabunge kadhaa wa chama cha Democratic kukosa kwa makusudi kuhudhuria hotuba ya Netanyahu huku maelfu ya waandamanaji wanaopinga vita vya Gaza wakionekana nje ya bunge.

Mamia ya watu walikusanyika nje ya majengo ya bunge huku wakiwa wamebeba mabango ya kuonyesha mshikamano na Palestina, likiwemo bango moja lililoandikwa “Netanyahu ni mhalifu wa kivita anayesakwa,” wakiashiria uamuzi uliotolewa mwezi Mei mwaka huu na mahakama ya kimataifa ya ICC kuomba hati ya kukamatwa kwa Waziri Mkuu huyo, waziri wake wa ulinzi na viongozi watatu wa Hamas kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.

Waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina wakisimama mbele ya majengo ya bunge la Marekani
Waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina wakisimama mbele ya majengo ya bunge la MarekaniPicha: Andrew Thomas/AFP/Getty Images

Rashida Tlaib, mbunge pekee wa Marekani mwenye asili ya Palestina, alibeba bango akimtaja Netanyahu kama “mhalifu wa kivita” na kumshutumu kwa mauaji ya kimbari.

Kwa mujibu wa polisi, watu watano walikamatwa ndani ya majengo ya bunge kwa kujaribu kutatiza hotuba ya kiongozi huyo wa Israel.

Akiizungumzia Iran, Waziri Mkuu huyo amedai kuwa Jamhuri hiyo ya Kiislamu ni mhimili wa ugaidi unayoitishia Marekani, Israel na kwa ujumla ulimwengu wa kiarabu. Amekwenda mbali zaidi na kuielezea Iran kama nchi ya kikatili inayopambana na ustaarabu.

Soma pia: Biden kukutana na Netanyahu katika Ikulu ya White House

Netanyahu ameongeza kuwa, mawakala wa Iran wamezishambulia shabaha za Marekani na kwamba Jamhuri hiyo ya Kiislamu inaamini kuwa, ili kushindana na Marekani ni lazima kwanza itawale eneo zima la Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, amejipiga kifua kwamba Israel ndio kizingiti kwa Iran kutimiza malengo yake eneo la Mashariki ya Kati.

Iran inaweza kumudu vita na Israel?

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Hotuba yake iliyodumu zaidi ya saa moja, Netanyahu alionekana kupuuza sauti za wakosoaji juu ya vita vya Gaza na badala yake kufahamisha kwamba hiyo ndio njia pekee kwa Israel kujilinda na kuendelea kuishi, ikionekana kuwa njia ya kuomba msaada zaidi wa kijeshi kutoka kwa Marekani.

Ametoa mkono wa shukrani kwa Marekani kwa kuipa Israel kile alichokiita “msaada wa ukarimu wa kijeshi” kwa miongo kadhaa na kuongeza kuwa, Israel imelipa fadhila hiyo kwa kuipatia Marekani taarifa muhimu za kijasusi ambazo baadaye zimekuwa sababu ya “kuokoa maisha ya watu wengi.”

Soma pia: Bunge la Israeli lapiga kura kupinga kuanzishwa taifa la Palestina 

Ziara ya Netanyahu nchini Marekani inatokea siku chache tu baada ya jaribio la mauaji dhidi ya mgombea urais kupitia chama cha Republican Donald Trump na pia tangazo la Rais Joe Biden la kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Netanyahu mwenyewe amewamwagia sifa Biden na Trump kwa juhudi zao kuelekea kupatikana kwa amani Mashariki ya Kati.

 

Related Posts