TUZO za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa msimu huu zitafanyika Agosti Mosi, jijini Dar es salaam huku vita ya nyota wa Yanga na Azam FC, Stephane Aziz Ki na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ikianza upyaa Bara.
Nyota hao ambao msimu uliopita walichuana katika vita Mfungaji Bora na Aziz KI kuibuka mbabe mwishoni kwa kufunga mabao 21 dhidi ya 19 ya Fei, wote wameingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo tatu tofauti za Mchezaji Bora wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho na ile ya Kiungo Bora wa msimu.
Tuzo ya Kiungo Bora wa Ligi Kuu wanaowania ni Stephane Aziz Ki wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Kipre Junior wa Azam FC.
Kwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu kuna Aziz Ki, Djigui Diarra, Ibrahim Bacca na Yao Kouassi wa Yanga, Fei Toto, Kipre Junior wa Azam FC, Ley Matampi (Coastal Union) na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, huku kwa Mchezaji Bora wa Shirikisho mbali na Aziz KI na Fei, pia kuna Mzize, Kipre Junior na Bacca.
Tukio la Tuzo za TFF hutolewa kwa kuwazawadia wanamichezo wote waliofanya vizuri katika mashindano yanayoandaliwa na shirikisho hilo na Bodi ya Ligi (TPLB) na matukio mengine rasmi yenye kuambatana na mpira wa miguu kwa hapa nchini.
Msimu huu, kutakuwa na ongezeko la tuzo tatu ambazo hazikuwepo msimu uliopita na kati ya hizo mbili ni mpya na ambazo ni ya mchezaji bora wa Tanzania anayecheza nje (mwanaume) na mchezaji bora wa Tanzania anayecheza nje ya nchi kwa upande wa wanawake.
Katika sherehe hizo, kutakuwa pia na ugawaji wa tuzo nyingine ambazo hii itahusisha mchezaji bora anayecheza soka la ufukweni.
Kwenye vipengele vitano ambavyo vitatolewa usiku huo wa Agosti Mosi mwaka huu jijini Dar es Salaam, zitahusisha katika Kombe la Shirikisho la FA, Tuzo ya Ligi Kuu ya Wanawake, Tuzo ya Ligi Kuu Bara, Tuzo za Utawala na Tuzo za Ligi nyingine.
Katika tuzo ya mfungaji bora wa Kombe la FA wanaowania ni Clement Mzize aliyeifikisha Yanga fainali na kuchukua ubingwa huo na Edward Songo wa Maafande wa JKT Tanzania ambao wote msimu uliopita walifunga mabao matano kila mmoja.
Kipa bora wanaowania ni Djigui Diarra ambaye aliipa Yanga ubingwa wa michuano hiyo, Khomeiny Abukabar wa Singida Black Stars zamani Ihefu na Mohamed Mustafa wa Azam FC ambaye alijizolea umaarufu baada ya kuonyesha soka safi katika fainali.
Katika tuzo ya mfungaji bora wa Ligi ya Wanawake anayewania pekee ni Aisha Mnunka wa Simba Queens ambaye msimu uliopita alifunga mabao 20 huku kipa bora wakiwania Najath Abbas (JKT Queens), Caroline Rufaa (Simba Queens) na Mariam Shabaan wa Bunda Queens.
Wanaowania tuzo ya mchezaji bora kwa upande wa Ligi ya Wanawake ni Aisha Mnunka, Violet Nicholaus na Vivian Corazone wanaoichezea Simba Queens, Stumai Abdallah wa JKT Queens na Kaeda Wilson aliyekuwa anaichezeaa timu ya Yanga Princess.
Makocha bora wanaowania katika tuzo za Ligi ya Wanawake ni Juma Mgunda (Simba Queens), Ester Chabruma wa JKT Queens na Noah Kanyoga wa Ceasiaa Queens huku kikosi bora cha kinachounda soka la wanawake kikitangazwa siku ya tukio hilo usiku.
Tuzo ya mchezaji bora chipukizi kwa wanawake inawaniwa na Ester Maseke na Bituro Mgosi wa Bunda Queens na Lydia Kabambo wa JKT Queens.
Katika tuzo ya mwamuzi bora msaidizi wanaowania ni Sikudhan Mkurungwa, Glory Tesha, Zawad Yusuph, Monica Wazael na Getruda Gervas huku wanaowania mwamuzi bora ni Amina Kyando, Tatu Malogo, Ester Adalbert na Anitha Kisoma.
Tuzo ya timu yenye nidhamu, zinazowania ni Bunda Queens, Amani Queens na mabingwa wa msimu uliopita wa Ligi ya Wanawake Simba Queens.
Katika tuzo za Ligi Kuu Bara, mfungaji bora pekee anayewania ni Stephane Aziz Ki wa Yanga ambaye msimu uliopita alifunga mabao 21, mbele ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC waliokuwa wakifukuzana aliyemaliza kwa kufunga mabao 19.
Tuzo ya kipa bora wanaowania ni Ayoub Lakred wa Simba, Ley Matampi wa Coastal Union aliyemaliza kinara wa ‘Clean Sheet’ 15 na Djigui Diarra wa Yanga aliyemaliza na 14 huku beki bora wanaowania ni Yao Kouassi na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wote wa Yanga na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Makocha wanaowania tuzo ya kocha bora ni David Ouma (Coastal Union), Bruno Ferry (Azam FC) na Miguel Gamondi wa Yanga huku kikosi bora cha msimu wa Ligi Kuu Bara kitatangazwa rasmi usiku wa tuzo hizo zitakazofanyika jijini Dar es Salaam.
Tuzo ya meneja bora wa Uwanja inawaniwa na Amir Juma (Azam Complex), Nassoro Makau (Mkwakwani) na Shaaban Rajabu wa Lake Tanganyika Kigoma.
Kwa upande wa tuzo ya kamishina bora wanaowania ni Martin Kibua (Tanga), Zena Chande (Dar es Salaam), Hamis Kitila (Singida), Sadick Jumbe (Mbeya) na Abousufian Silia wa Iringa.
Tuzo ya mchezaji bora chipukizi msimu uliopita inawaniwa na Semfuko Charles (Coastal Union), Rahim Shomary (KMC) na Costantine Malimi wa Geita Gold.
Seti bora ya waamuzi inayowaniwa ni ile ya Yanga iliyoshinda mabao 5-1, dhidi ya Simba ambayo mwamuzi wa kati alikuwa Ahmed Arajiga wa Manyara aliyesaidiwa na Mohamed Mkono na Kassim Mpanga huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Ramadhan Kayoko.
Seti nyingine ni ile ya ushindi wa Tanzania Prisons iliyoifunga Simba mabao 2-1, ambapo mwamuzi wa kati alikuwa ni Nassoro Mwinchui aliyesaidiwa na Makame Mdogo, Neema Mwambashi huku mwamuzi wa akiba akisimamia Selemani Kinugani.
Nyingine ni ya ushindi wa Azam FC wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga ambayo mwamuzi wa kati alikuwa ni Hery Sasii wa Dar es Salaam aliyesaidiwa na Frank Komba na Kassim Mpanga huku mwamuzi wa akiba yaani ‘4 Offical’ akisimamia Isihaka Mwalile.
Seti nyingine ya waamuzi ni ya mchezo wa Azam FC na Mashujaa uliomalizika suluhu ambapo mwamuzi wa kati alikuwa ni Katanga Hussein akisaidiwa na Hamdan Said, Martin Mwalyaje huku mwamuzi wa akiba akiwa Ramadhan Kayoko wa Dar es Salaam.
Nyingine ni ya suluhu ya Yanga dhidi ya JKT Tanzania ambapo mwamuzi wa kati alikuwa Hery Sasii aliyesaidiwa kwa pamoja na Omari Kambangwa na Zawadi Yusuph huku refa wa akiba katika mchezo huo akisimamia Isihaka Mwalile kutoka jijini Dar es Salaam.
Seti ya mwisho ya waamuzi ni ya ushindi wa Yanga wa mabao 2-0 dhidi ya Simba ambapo inaundwa na mwamuzi wa kati, Ahmed Arajiga wa Manyara aliyesaidiwa na Mohamed Mkono, Kassim Mpanga huku refa wa akiba akisimamia Tatu Malogo kutoka Tanga.
Wanaowania tuzo ya mwamuzi bora msaidizi ni Frank Komba, Mohamed Mkono, Kassim Mpanga, Janeth Balama na Zawadi Yusuph huku mwamuzi bora wanaowania ni Tatu Malogo, Ahmed Arajiga, Abdallah Mwinyimkuu, Amina Kyando, Hery Sasii na Saad Mrope.
Bao bora la msimu litatangazwa usiku wa tuzo hizo sawa na ilivyokuwa pia kwa upande wa tuzo ya mchezo wa kiungwana (Fair Play).
Kwa upande wa tuzo ya timu yenye nidhamu bora zinazowania ni Singida Black Stars zamani Ihefu, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar.
Katika tuzo nyingine zinazowaniwa ni mchezaji bora wa Ligi ya Championship ambapo wanaowania ni Boban Zirintusa wa Biashara United, Edgar William na Casto Mhagama wote wanaoichezea KenGold ambao ndio waliokuwa mabingwa msimu uliopita.
Wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa First League ni Mohamed Bakari na Ayoub Masudi wa African Sports na Ahmad Ndondi wa Malimao FC.
Wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa Ligi ya vijana ni Bruno Nataly wa Kagera Sugar, Omary Shaaban Mwinyimvua wa Dodoma Jiji na Ally Mohamed Golo wa Azam FC.
Kwa upande wa tuzo ya mchezaji bora wa soka la ufukweni wanaowania ni Jaruph Rajabu Juma wa Friends of Mkwajuni, Yahya Tumbo wa Vingunguti Kwanza na Abdillah Mohammed wa Ilala FC.
Tuzo ya mchezaji bora wa Tanzania anayecheza nje kwa upande wa wanaume wanaowania ni Mbwana Samatta, Novatus Dismas na Himid Mao Mkami huku kwa wanawake wanaoshindania tuzo hiyo ni Clara Luvanda, Aisha Masaka na Oppah Clement.
Kwenye upande wa tuzo za utawala ambazo zitatangazwa siku ya sherehe hizo ni tuzo ya Rais, Tuzo ya Heshima Soka la Wanawake, Tuzo ya Heshima na Tuzo ya mchezaji gwiji.
Msimu uliopita Yanga ilipata jumla ya tuzo 12 zikiwemo za mmoja mmoja na zile za kikosi bora ambapo aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Fiston Mayele alichukuwa ya Mfungaji Bora, Bao bora la msimu, Mchezaji Bora wa jumla wa msimu yaani (MVP).
Kipa wa timu hiyo, Djigui Diarra alishinda tuzo mbili za kipa bora wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi Kuu na Dickson Job akipata ya beki bora wakati Bakari Mwamnyeto akiwa mchezaji bora wa ASFC na wote waliingia katika kikosi bora.
Aliyekuwa kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alikuwa kocha bora huku Clement Mzize akishinda tuzo ya mchezaji bora kijana chini ya miaka 20.
Simba ndiyo ilikuwa timu ya pili wachezaji wake kuchukuwa tuzo nyingi ikiongozwa na Saido Ntibazonkiza aliyebeba tatu ya mfungaji bora baada ya kufunga mabao 17, Fair Play (mchezo wa kiungwana) na kiungo bora huku pia akiingia kwenye kikosi bora.
Wengine ni Henock Inonga, Mohammed Hussein, Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin, Clatous Chama ambao wote waliingia kikosi bora cha msimu.
Tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa Ligi Kuu ilienda kwa Lameck Lawi wa Coastal Union huku mchezaji bora wa Championship alikuwa Edward Songo wa JKT Tanzania wakati Kamishina Bora wa Ligi Kuu tuzo hiyo ilikwenda kwa Isack Munisi.
Tuzo ya mwamuzi bora wa Ligi ya wanawake (WPL) msimu wa 2022/23 ilienda kwa Ester Adalbert wakati mwamuzi msaidizi ni Glory Tesha.
Mwamuzi bora wa Ligi Kuu Bara msimu huo tuzo hiyo ilienda kwa Jonesia Rukyaa huku tuzo ya mwamuzi msaidizi ikienda kwa Frank Komba.
Tuzo ya seti bora ya waamuzi ilikwenda kwa Jonesia Rukyaa, Zawadi Yusuph, Athuman Rajabu na Ally Simba katika mechi ya Geita Gold na Dodoma Jiji.
Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu uliopita tuzo hiyo ilienda kwa Jentrix Shikangwa wa Simba Queens aliyefunga mabao 17. Kocha wa JKT Queens, Ally Ally alishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Wanawake huku mchezaji bora akiwa ni Donisia Minja.