Angalia hapa majina ya ajira mpya serikalini

Dar es Salaam. Sekretarieti ya Ajira imewaita waliofanikiwa kupata ajira mpya serikalini kuchukua barua za kupangiwa vituo vya kazi.

Tangazo hilo limetolewa jana Jumatano Julai 24, 2024 na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, huku likibainisha ni wale waliofanya usaili kati ya Januari 15, 2023 hadi Juni 21, 2024 na wengine waliokuwa kwenye kanzidata.

“Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika utumishi wa umma anapenda kuwataarifu waombaji kazi wa nafasi mbalimbali waliofanya usaili kati ya Januari 15, 2023 na Juni 21, 2024 kuwa matokeo ya waombaji kazi waliofaulu usaili huo ni kama yalivyoorodheshwa katika tangazo hili.

“Orodha ya majina haya pia inajumuisha baadhi ya wasailiwa waliokuwa kwenye kanzidata (Database) kwa kada mbalimbali ambao wamepangiwa vituo vya kazi baada ya nafasi kupatikana,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa waombaji waliofaulu usaili wanatakiwa kuchukua barua za kupangiwa kituo cha kazi katika Ofisi za Sekretarieti ya Ajira katika utumishi wa umma zilizopo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwenye majengo ya Dk Asha Rose Migiro, masjala ya wazi ndani ya siku saba tangu tarehe ya tangazo hilo na baada ya hapo barua ambazo hazitachukuliwa na wahusika zitatumwa kupitia anuani zao za Posta.

Pia, taarifa hiyo imeeleza waombaji kazi waliofaulu usaili na kupangiwa kituo cha kazi wanatakiwa kuripoti kwa mwajiri katika muda ulioainishwa kwenye barua za kupangiwa kituo cha kazi, wakiwa na vyeti halisi (Originals Certificates) vya masomo kuanzia kidato cha nne na kuendelea, ili vihakikiwe na mwajiri kabla ya kupewa barua ya ajira.

Related Posts