MARA kadhaa amekuwa akihusishwa na vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga, japo mara zote dili za kwenda klabu hizo zilikuwa zikiishia njiani.
Kwa mfano kwa sasa amekuwa akitajwa huenda akatua Yanga baada ya dirisha dogo lililopita kutajwa sana na miamba hiyo wakati akiwa Singida Fountain Gate, ikielezwa anatakiwa kwenda kuchukua nafasi ya Gift Fred.
Jina lake kamili ni Abdulmajid Yahya Mangalo, mmoja ya mabeki wa kati wazawa wenye uwezo mkubwa katika kukaba na kuzuia mashambulizi akitumia akili nyingi na nguvu kidogo, jambo ambalo klabu nyingi kubwa zimekuwa zikimpigia hesabu za kumbeba ili azitumikie.
Licha ya kutokuwa na wasifu mkubwa, lakini Mangalo amekuwa mhimili mkubwa katika vikosi alivyowahi kuvitumikia kuanzia Biashara United hadi Singida FG aliokuwa nao msimu uliopita.
Nyota huyo aliyeanza kuwika na Biashara United alipoipandisha msimu wa 2017/18 kabla ya kushuka nayo tena msimu uliopita na kutua Singida Fountain Gate, kwa sasa amemalizana na timu hiyo baada ya kumaliza mkataba na anasubiri simu ziite ajue ataibukia wapi msimu ujao, huku Yanga ikitajwa zaidi.
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Mangalo amefunguka mengi ikiwamo tetesi za kutakiwa na Simba na Yanga na mustakabali wake baada ya kumaliza mkataba Singida FG.
Anasema pamoja kusemwa mengi kutua Simba na Yanga, hana haraka sana kwani anao wasimamizi wanaoshughulikia dili zote za usajili kwani wameshamtaka awe mtulivu.
Anasema yeye kazi yake ni soka, hivyo haoni kinachoweza kumzuia kupata namba katika kikosi chochote atakachosajiliwa, baada ya kuhusishwa na Yanga miezi kadhaa tangu atajwe Simba iliyokuwa chini ya Kocha Abdelhak Benchikha.
“Hizo tetesi na mambo mengine wanasimamia viongozi wangu, hivyo muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi, kimsingi wameniambia niendelee na yangu kama mchezaji na wao ndio watajua nini kitatokea baada ya kumaliza mkataba, Fountain Gate,” anasema Mangalo na kuongeza;
“Yanga na Simba ni timu kubwa na wachezaji wake wako fiti, ila kwa uwezo nilionao naweza kupata nafasi kama nitakuja kufanikiwa kutua katika mojawapo, nimekuwa hivyo kwenye timu nyingine nilizowahi kupita.”
Mangalo anakiri kama mchezaji amekuwa akiota kuzichezea timu hizo sambamba na Azam FC, kwani ni klabu za mfano kwa Tanzania kwa sasa, ndio maana anasubiri simu ziite ajue tu msimu ujao anaibukia wapi.
Beki huyu tangu alipotua Biashara United wakati ikijulikana Polisi Mara, amekuwa na uhakika wa namba hadi alipoipandisha timu hiyo baada ya waliokuwa wamiliki Jeshi la Polisi mkoani Mara kuikabidhi kwa wananchi na mwenyewe anafichua kinachombeba ni nidhamu bora alivyonayo.
Baada ya kutua nyota huyo alikuwa mhimili mkubwa akicheza mechi zote na kuhusika katika kupanda Ligi Kuu msimu wa 2017/18 kisha kushuka 2022/23.
Kama haitoshi baada ya kushuka na Biashara alitimkia Singida FG na licha ya timu hiyo kuwa na mastaa wengi lakini alikuwa na uhakika wa namba. Wakati anatua Singida ikiwa inatumia jina la Singida Big Stars kabla kuwa Singida FG (sasa Fountain Gate) alikuwa sambamba na Aziz Andambwile kutoka Mbeya City, Paul Godfrey ‘Boxer’ kutoka Yanga na Kelvin Sabato aliyekuwa akitokea Mtibwa Sugar.
Anasema, pia mechi ambazo beki huyo amekosa, zimekuwa zikiigharimu timu hiyo ikiwamo kipindi alipokuwa majeruhi wa kifundo cha mguu.
Mangalo anasema uwezo binafsi, nidhamu, kusoma falsafa ya makocha ndio siri inayompa uhakika wa namba akieleza popote anaanza kikosi cha kwanza.
“Ni kwa sababu ya nidhamu ndani na nje ya uwanja, uwezo na juhudi binafsi na kuelewa haraka mfumo wa makocha ninaokutana nao, wanaponiamini nawaaminisha kwa kazi uwanjani,” anasema Mangalo.
Singida ni moja ya timu zilizokuja kuzinduka mwishowe kwenye Ligi Kuu licha ya msimu uliopita kucheza Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa raundi ya pili na Future ya Misri.
Mangalo anasema timu iliyumbishwa hasa baada ya dirisha dogo kufungwa kwa baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza cha timu hiyo kuondoka kuhamia Ihefu (sasa Singida Black Stars).
Anasema, licha ya mwenyewe kuwa nje kwa muda mrefu sasa akiuguza majeraha yake, lakini pia ishu ya kuondoka kwa wachezaji saba hao nayo iliiyumbisha Singida na walipambana kwa juhudi hata kuiokoa isishuke daraja, kwani hali ilishakuwa tete.
Anasema kuondoka kwa nyota hao ambao walikuwa na muunganiko mzuri, lakini haikupaswa kuwa chanzo cha timu kutofanya vizuri kwakuwa wengi wao walikuwa na uwezo unaofanana.
“Sitaki kutaja moja kwa moja dirisha dogo kuwa sababu, lakini waliopo tungeweza kuipigania timu kulinda matokeo tuliyokuwa nayo, japo nami sikucheza mechi kadhaa kutokana na majeruhi, lakini kuondoka kwa hao wachezaji ilileta changamoto iliyoleta presha kwa waliobaki na mashabiki, lakini hali ilitulia.”
Nyota huyo anasema kati ya vitu vilivyomkosesha raha msimu uliopita ni majeraha yaliyomweka nje ya uwanja kwa muda mrefu, japo aliporejea aliendelea na moto wake kiasi cha kuzu kelele pale ambako hakuitwa kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kilichokuwa kikijiandaa na mechi za kimataifa.
“Nilikuwa naumia mno kutokuwa uwanjani kuendeleza majukumu yangu, japo nashukuru nilipona na kurejea vizur.”
Beki huyo anasema hadi sasa beki aliyewahi kucheza naye aliyemaliza msimu akiwa na Ihefu, (Singida Black Stars), Mkenya Joash Onyango ndiye anayemkubali kutokana na mengi aliyojifunza kwake.
Anasema nyota huyo licha ya baadhi ya mashabiki wamekuwa wakimkashifu na kumtuhumu ni mzee, lakini jamaa alikuwa injini katika eneo la beki na kwamba alimpa madini mengi na kazi kubwa ilifanyika.
Mbali na kuzitamani kuzichezea Simba, Yanga na Azam, lakini Mangalo anasema kiu yake kubwa ni kuona anafika mbali katika maisha yake ya soka, hususani kucheza soka la kulipwa.
Anasema anaamini uwezo wa kucheza nje upo kwa jinsi alivyo na kipaji, lakini anapenda kulitumikia taifa lake kupitia Taifa Stars.
Anasema kiu yake ni kuona mchango wake ukionekana kwenye timu nchi yake, hivyo yuko tayari kuvaa jezi ya Taifa Stars na kufanikisha ndoto zake na Taifa kwa ujumla.
“Nadhani kila mmoja anaona uwezo wangu uwanjani, mchezo wa mpira sio maneno, naamini muda wangu ukifika niko tayari kuweka mchango wangu kwa nchi yangu. Wapo viongozi ambao wana jukumu la kuangalia nani anastahili kwa muda gani, hivyo siku wakiona nafaa naamini wataniita kwa kuwa hii ni timu ya taifa na siyo ya mchezaji mmoja” anasema nyota huyo.