Biden aelezea uamuzi wa kutowania urais wa Marekani – DW – 25.07.2024

Katika hotuba yake ya kwanza tangu alipojiondoa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Marekani katika uchaguzi wa Novemba 5, rais Joe Biden, alisema kuilinda demokrasia ni muhimu zaidi kuliko cheo chochote kile. Biden alitoa hotuba yake jana Jumatano, ya kwanza tangu alipotangaza anajiondoa mbio za kuwania urais kupitia mtandao wa kijamii Jumapili iliyopita na kwamba anakabidhi kijiti cha uongozi kwa makamu wake, Kamala Harris.

“Muelekeo na mustakhbali ulioongoka wa nchi hii ni mkubwa zaidi kuliko mtu yeyote kati yetu. Sisi tunaothamini muelekeo huu, tunauthamini sana; muelekeo wa demokrasia ya Marekani yenyewe. Ni lazima tuungane kuilinda demokrasia. Katika wiki za hivi karibuni imekuwa wazi bayana kwangu kwamba nahitaji kukiunganisha chama changu katika jitihada hii muhimu.”

Rais Biden amesema anafurahia kuwatumukia Wamarekani, lakini jukumu hili tukufu la kuliimarisha shirikisho halimuhusu yeye tu bali linawahusu Wamarekani wote; familia zote na mustakhbali wao.

Rais wa Marekani, Joe Biden, kulia, na makamu wake, Kamala Harris
Rais wa Marekani, Joe Biden, kulia, na makamu wake, Kamala HarrisPicha: Matt Kelley/AP Photo/picture alliance

Biden amesema ameamua njia nzuri muafaka ya kusonga mbele ni kukabidhi kijiti cha uongozi kwa kizazi kipya kwa kuwa hiyo ndiyo njia nzuri kabisa ya kuliunganisha taifa la Marekani.

Soma pia: Harris afanya kampeni katika jimbo la Wisconsin

Biden aidha amesema Marekani italazimika kuamua kati ya kusonga mbele au kurudi nyuma, kati ya matumaini au chuki, kati ya umoja na migawanyiko. Wamarekani lazima tuamue kama bado tunaamini katika uaminifu, ustaarabu, heshima, uhuru, haki na demokrasia.

“Katika miezi michache ijayo, Wamarekani watalazimika kuchagua muelekeo wa mustakhbali wa Marekani. Nilipitisha uamuzi wangu. Niliwajulisha fikra zangu. Ningependa kumshukuru makamu wetu wa rais shupavu, Kamala Harris. Ana uzoefu, ni mkakamavu. Amekuwa mshirika mahiri kwangu na kiongozi mzuri kwa taifa letu. Sasa chaguo liko kwenu, Watu wa Marekani.”

Biden amesema ataelekeza nguvu katika kuifanya kazi yake kwa weledi kama rais kwa muda uliosalia wa muhula wake, unaokamilika Januari 20, 2025, huku akiendelea kuulinda uhuru binafsi wa Wamarekani na haki za kiraia, kuanzia haki ya kupiga kura hadi haki ya kuchagua na kuamua.

Hotuba yaibua hisia mseto

Kama ilivyo kawaida yake mgombea wa chama cha Republican Donald Trump amekimbilia kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social na kuelezea maoni yake kuhusu hotuba ya Biden, akiandika kwamba ilikuwa vigumu kueleweka na mbaya sana. Kampeni ya Trump pia ilisambaza picha ya Biden akiwa amesimama mbele ya skrini inayoonesha hotuba ya Biden.

Rais mstaafu wa Marekani Barack Obama amemshukuru rais Biden katika taarifa aliyoituma pia kwenye mitandao ya kijamii, akirudia maneno ya Biden kwamba muelekeo na mustakhbali wa taifa ni mkubwa zaidi kuliko mtu yeyote. Obama amesema Biden ameyazingatia sana maneno haya katika miaka yote ya utumishi wake kwa Wamarekani.

(dpa, afptv)

Related Posts