Kaseja matumaini kibao Kagera Sugar

IKIWA imemaliza siku 15 tangu ilipoanza maandalizi ya msimu mpya Julai 12, mwaka huu, Kocha wa makipa wa Kagera Sugar, Juma Kaseja amesema maendeleo ya kikosi chao siyo mabaya huku akiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri Ligi Kuu Bara.

Timu hiyo ilianza maandalizi ya Ligi Kuu itakayoanza Agosti 16, mwaka huu kwa kuweka kambi yake mjini Bukoba na inajifua kwenye uwanja wa Kaitaba na kwenye fukwe za Ziwa Viktoria mjini humo.

Kaseja alisema hakuna msimu ambao ni rahisi ndiyo maana walianza mapema maandalizi kwa kugawa mazoezi yao wakianza kwa kujenga utimamu wa mwili na mbinu za kiufundi.

“Tumeanza na kuweka miili sawa kisha tunakuja kwenye ufundi na mbinu za jinsi ya kucheza. Kwa upande wangu hali siyo nzuri sana wala mbaya sana, tunajaribu kuandaa timu tumegawa wiki za maandalizi kwa kujenga miili, kiufundi na mbinu za kucheza uwanjani,† alisema Kaseja.

Daktari wa timu hiyo, Ally Malindi alisema kuna mabadiliko makubwa kwenye idara ya tiba na timu imeongeza vifaa vya kisasa na wachezaji waliporipoti kambini walifanyiwa vipimo kuangalia kama wamepitiliza uzito na majeraha yanayotokana na mechi za mtaani wakiwa likizo.

“Waliporipoti kambini tulifanya tathmini ya kimatibabu kujua utimamu wao wa mwili tumeridhika wako vizuri kiafya. Wachezaji wangu watakuwa vizuri zaidi kutokana na aina ya mazoezi wanayopewa, pia itawasaidia kukwepa majeraha kwasababu wako fiti kimwili.

“Hii itatusaidia katika mechi zetu kwani ligi itaanza tukiwa tumeshakuwa imara kwenye utimamu. Natarajia kuiona Kagera Sugar inafika mbali kwa sababu ya aina ya mazoezi tunayofanya, wachezaji wanakula kwa wakati na kila kitu kiko sawa,† alisema Malindi

Related Posts