Amnesty yapendekeza vikwazo zaidi vya silaha Sudan – DW – 25.07.2024

Katika ripoti yake kuhusu silaha zinaendelea kuongezeka katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita, shirika hilo limesema vita nchini Sudan kati ya jeshi na wanamgambo cha RSF vinachochewa na usambazaji wa silaha usiozuiliwa na washirika kutoka sehemu nyengine duniani wanaounga mkono pande zinazohasimiana nchini humo.

Soma pia: Marekani yaandaa mazungumzo ya kusitisha mapigano Sudan

Ripoti hiyo mpya iliyopewa jina la “Silaha Mpya Zinazochochea Migogoro ya Sudan”, imegundua silaha zilizotengenezwa hivi karibuni au kuhamishwa kutoka nchi zikiwemo Urusi, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu, Serbia, Yemen na China zilikuwa zikiingizwa na kutumika katika medani ya vita.

Kwa mujibu wa mjumbe wa Marekani nchini Sudan Tom Perriello, tangu vita vilipozuka mwezi wa Aprili mwaka jana, vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu, huku mashirika mengine yakikadiria idadi ya waliofariki ni takriban watu 150,000.

Mkuu wa kitengo cha utafiti wa migogoro wa Amnesty International Brian Castner ameliambia shirika la habari la AFP kuwa maelfu ya silaha zinaingizwa Sudan na kuchochea ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Soma pia: WHO yaonya juu ya kuongezeka kwa mashambulizi kwenye hospitali nchini Sudan

Castner,amesedokeza kuwa idadi ya silaha ndogo ndogo zinazoingia Sudan ni ya kutisha huku watu wengi wakiuwawa kwa silaha hizo ameongeza kusema kuwa matukio mengi ya ukiukaji,  ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia na kuhamishwa, yanafanikiwa kwa utumiaji wa silaha ndogo.

Ufuatiliaji na utekelezwaji wa vikwazo

Sudan | Mapigano huko Khartoum
Watu wanapita kwenye jengo lililojaa matundu ya risasi katika Souk Sitta (Soko la Sita) kusini mwa Khartoum.Picha: AFP/etty Images

Aidha ripoti hiyo imegundua kuwa vikwazo vya silaha, vilivyowekwa tangu mwaka 2004 vimetumika tu kwa eneo la Darfur magharibi, na kwamba utekelezwaji wake ni mdogo na kwamba havina athari yoyote ya maana katika kuzuia usambazaji wa silaha hizo.

Mkurugenzi mkuu wa Amnesty katika kushughulikia Athari za Haki za Kibinadamu za Kikanda, Deprose Muchena, amesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lazima “lipanue kwa haraka vikwazo vya silaha kwa maeneo mengine ya Sudan, na pia kuimarisha mifumo yake ya ufuatiliaji na uhakiki.

Soma pia: Sudan Kusini: Hakuna Mafuta, hakuna chakula

Huku haya yakiarifiwa, pande zote mbili za mzozo zimekuwa zikishutumiwa mara kwa mara kwa uhalifu wa kivita ikiwa ni pamoja na kuwalenga raia kimakusudi, ufyatuaji risasi kiholela wa maeneo ya makazi na kuzuia misaada ya kibinadamu, huku mamilioni ya Wasudan wakiteseka kwa njaa.

Vurugu zauwa watu 38 El-Fashir Sudan

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Siku ya Jumatatu, shirika la misaada la matibabu la Ufaransa la Madaktari Wasio na Mipaka lilisema kwamba kati ya maelfu ya majeruhi wa vita waliotibiwa katika mojawapo ya hospitali zake kuu katika mji mkuu wa Sudan, asilimia 53 walipata majeraha ya risasi.

 

Related Posts