AKILI ZA KIJIWENI:Haitopendeza Coastal ikimtimua Ouma

KUNA tetesi Coastal Union inafikiria kuachana na kocha wao wa sasa, Francis Ouma na kisha nafasi yake ichukuliwe na kocha mmojawapo wa timu ya Ligi Kuu.

Kufanya vibaya kwa timu hiyo kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yaliyomalizika wiki iliyopita kunatajwa kuchangia ushawishi wa uamuzi wa kutaka kumtimua.

Hata hivyo, inaripotiwa amepishana na vigogo baadhi kwenye masuala yanayohusu timu hiyo hivyo kuna wanaoshauri awekwe kando na aletwe mwingine.

Kwa maoni yangu nawashauri Coastal wawe na uvumilivu na kocha Ouma ambaye ametajwa kuwania Tuzo ya Kocha Bora wa msimu sambamba na Bruno Ferry wa Azam na Miguel Gamondi wa Yanga na kama kuna mpango huo unaotajwa wa kumtimua basi wausitishe na waendelee naye.

Ouma ni mwalimu mzuri na ushahidi wa hilo ni kazi nzuri aliyofanya msimu iliopita ambapo aliiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu huku ikikata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Kutofanya vizuri kwenye Kombe la Kagame hakupaswi kutumika kumhukumu kocha Ouma kwa vile timu haikuwa imefanya maandalizi ya kutosha, pia wachezaji walikuwa ndio kwanza wametoka mapumzikoni.

Ikumbukwe kwenye Kombe la Kagame, Coastal Union haikuwa na mabeki wake wawili walioifanya kuwa imara msimu uliopita ambao ni Lameck Lawi na Felly Mulumba.

Lawi alikuwa katika maandalizi ya kwenda Ubelgiji kujiunga na timu ya Gent wakati Felly Mulumba hayupo katika kikosi cha Coastal Union kwa sasa baada ya kuachwa mwanzoni mwa dirisha la usajili linaloendelea.

Yule Ouma anaonekana ni mtu sahihi sana kwa Coastal Union kwani anaitengeneza timu na inafanya vizuri kwa bajeti ndogo jambo ambalo huwa gumu kwa makocha wengi kulifanya.

Related Posts