UNIDO kuwanoa wajasiriamali kutoka mikoa 10 kuboresha biashara

Dar es Salaam. Wajasiriamali wadogo na wa kati kutoka mikoa 10 na wilaya 40 watanufaika na mpango wa mafunzo unaolenga kuwajengea uwezo wa biashara zao kwa kuzingatia ubora, usalama wa chakula, mahitaji ya masoko na kuongeza ushindani wa bidhaa zao katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

 Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Tanga, Singida, Ruvuma, Mwanza, Geita, Shinyanga, Kilimanjaro, Kagera na Kigoma na wajasiriamali watanufaika na fursa hiyo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kupitia mradi wake wa Qualitan, ikiwa ni kati ya programu inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU).

Mradi huo utakaotekelezwa kwa miezi sita kuanzia Agosti, 2024, UNIDO itashirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Kuhudimia Viwanda Vidogo (Sido) kutoa mafunzo hayo ambayo uandaaji ulishirikisha sekta binafsi kwa kupokea na kujumuisha mchango wa utaalamu kutoka kwa mashirika yakiwamo ya TWCC na TCCIA.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Julai 25, 2024 na UNIDO kuhusiana na uzinduzi huo, imemnukuu mshauri mkuu wa kiufundi wa mradi huo, Stefano Sedola akisema mradi huo unaratibu mafunzo kwa biashara 1,000.

Amesema lengo ni kuwapatia maarifa, ujuzi, zana na mbinu kuhusu viwango vya ubora, usalama na mahitaji ya masoko.

“Mafunzo haya yatalenga michakato ya uzalishaji, thamani ya bidhaa na upatikanaji wa masoko yenye faida ndani na nje ya nchi. Bidhaa sita za chakula itakayohusishwa ni mchele, asali, viungo, unga, samaki na bidhaa za samaki na mafuta ya kula,” amesema Sedola.

Amesema nyenzo za mafunzo kama vitini na miongozo mingine imeandaliwa na wataalamu kutoka TBS na Sido na kuthibitishwa kupitia tathmini ya mahitaji ya mafunzo hayo.

“UNIDO inafanya kazi kwa karibu na TBS kuboresha na kukidhi viwango vya ubora na Sido kuboresha shughuli za wajasiriamali wadogo na wa kati katika kupitia mbinu jumuishi,” amesema.

Sedola amesema tukio hilo litawaleta pamoja wizara, idara na taasisi za Serikali, Umoja wa Ulaya, wakuu wa taasisi zilizohusika katika uandaaji wa programu hiyo, watekelezaji wa miradi, wajasiriamali wadogo na wa kati na wadau wanaotekeleza mipango mbalimbali kama hiyo nchini.

 “Pia litatoa fursa kwa wadau hao kushirikishana, hivyo kukuza ushirikiano na kujenga muafaka katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.

Kupitia taarifa hiyo, Mratibu wa Mradi wa Qualitan, Valency Mutakyamirwa amesema mradi huo unaotekelezwa na UNIDO ukishughulikia lengo la pili kwenye mradi wa Begin, unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya.

“Afua ya mradi huu ni kuimarisha uwezo wa TBS, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na kufikia maabara za upimaji na metrolojia, shughuli za viwango, Tehama na usimamizi wa mifumo,” amesema.

Related Posts