Coastal yamnasa straika Mkenya | Mwanaspoti

WAGOSI wa Kaya, Coastal Union, ipo hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa straika Mkenya, John Mark Makwata kutoka Kariobangi Sharks inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Timu hiyo inayoshiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, inataka kukamilisha dili hilo baada ya kuvutiwa na mchezaji huyo ambaye msimu uliopita katika Ligi Kuu ya Kenya (KFKPL), alifunga mabao 16 kupitia  michezo 13 aliyocheza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Coastal, Abbas Elsabri alisema, hawezi kuzungumza moja kwa moja juu ya uhamisho wa nyota huyo kwani bado wanaendelea na taratibu za usajili na zitakapokamilika wataweka wazi.

“Kuna baadhi ya wachezaji tuko katika mazungumzo nao mazuri ya kupata saini zao hivyo niwahakikishie mashabiki zetu bado zoezi la usajili linaendelea kimyakimya, lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi msimu ujao,” alisema Elsabri.

Elsabri aliongeza, maandalizi ya kikosi hicho yanayoendelea hadi sasa kisiwani Pemba Zanzibar, yanawapa imani kubwa kwao kuanzia benchi la ufundi hadi viongozi, hivyo mashabiki watarajie mambo bora zaidi msimu ujao wa mashindano mbalimbali.

Kwa upande wa kocha wa timu hiyo Mkenya David Ouma alisema, kwa asilimia kubwa wachezaji wanazidi kuelewana huku akiweka wazi michuano ya Kombe la Kagame 2024 iliyomalizika wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam imemsaidia kwa kiwango kikubwa.

Makwata alizidiwa mabao matatu tu katika Ligi Kuu ya Kenya msimu uliopita na Mfungaji Bora, Benson Omalla wa Gor Mahia aliyefunga 19 na kukiwezesha kikosi hicho kutwaa  ubingwa wa 21 ikivuna pointi 73. 

Related Posts