CAF yairudisha tena Yanga Dar

KAMA ambavyo Mwanaspoti liliwahabarisha wiki iliyopita kwamba, Yanga huenda ikalainisha mambo katika Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Vital’O ya Burundi, ndivyo ilivyo baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuridhia ombi la Warundi kuhamia Azam Complex kucheza mechi za nyumbani za michuano hiyo.

Yanga sasa haitalazimika kwenda Burundi, baada ya Vital’O kuomba kuutumia Azam uliopo Chamazi na CAF kuridhia ikiwa ni timu kadhaa zilizoomba kuutumia uwanja huo kwa michuano hiyo kwa hatua za awali.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara, awali walitakiwa wacheze ugenini Agosti 17 kwa kuifuata Vital’O katika mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini sasa watasalia Dar kama ilivyokuwa msimu uliopita ilipovaana na Asas ya Djibouti.

Yanga itarudiana na Vital’O kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Agosti 24 na timu itakayofuzu itatinga raundi ya pili na kucheza na mshindi kati ya CBE ya Ethiopia ama SC Villa ya Uganda.

Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Uwanja wa Azam Complex, Amir Juma alisema, Vital’O ni kati ya timu tano zilizoomba kutumia uwanja huo kwa mechi hizo za kimataifa (CAF).

“Tumepokea maombi ya Vital’O na tumeshawajibu kwamba tumekuwakubalia  na kwamba mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Yanga itafanyika hapa Azam Complex. Mbali na Vital’O pia nyingine zilizoomba ni Rukinzo ya Burundi, Horseed ya Somalia zinazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika,” alisema.

Alizitaja nyingi ni As Arta Solar 7 ya Djibouti, Dekadaha ya Somalia zitakazokutana katika mechi za  Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akisema safari hii Yanga haijaomba kuutumiwa uwanja huo hadi sasa.

Amir alisema, sio Yanga tu, bali hata timu nyingine za ndani kama Simba, Coastal Union nazo hazijaomba hadi sasa, ingawa kwa mujibu wa taarifa kutoka klabu ya Coastal ni kwamba huenda ikahamia hapo kwa mechi hizo za CAF na zile za Ligi Kuu Bara itacheza Uwanja wa KMC kwani Uwanja wa Mkwakwani unakarabatiwa kwa sasa.

“Timu ya ndani hapa itakayotumia uwanja wetu ni Azam FC ambao ni wenyeji, lakini klabu nyingine bado hatujapokea maombi yao, labda tusubiri kwa kuwa klabu kama Simba wao hawaanzii hatua hii labda huko mbele wataleta maombi yao.”

Related Posts