BAADA ya watani wa jadi kugombania saini ya kiungo wa JKT Queens, Amina Bilal hatimaye Simba Queens imefanikiwa kuizidi akili Yanga Princess na kumnasa mchezaji huyo kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Amina aliwahi kuwa nahodha wa Yanga, iliyomnasa akitokea Msimbazi, kabla ya msimu uliopita kujiunga na JKT Queens.
Awali Yanga ilikuwa ya kwanza kukamilisha karibu taratibu zote za kutaka kumrudisha kiungo huyo kikosini na kilichokuwa kimebaki ni kusaini tu, lakini Simba iliingilia kati dili hilo kwa kuweka dau kubwa lililomfanya amwage wino Msimbazi.
Amina sio mgeni kwa timu zote kwani msimu 2019/20 aliwahi kuichezea Simba kwa msimu mmoja kabla ya kutimkia Yanga alikodumu kwa misimu mitatu na baadae kwenda kujiunga na JKT.
Akizungumza na Mwanaspoti, mmoja wa viongozi wa Simba alisema tayari amekamilisha taratibu zote na kuungana na wenzake kambini. “Juzi alikamilisha baadhi ya vitu ikiwemo kucheki afya na kila kitu kilienda sawa na sasa yupo kambini na wenzake kwa ajili ya msimu mpya,” alisema kiongozi huyo aliyekataa kuandikwa jina gazetini na kuongeza;
“Kama mnavyojua ni mchezaji muhimu hasa eneo la kiungo na aliwahi kucheza Simba kwa uhitaji wa eneo hilo tunaona anakwenda kutusaidia.”