INDIA, TANZANIA WAJADILIANA UHIFADHI WA MISITU, WANYAMAPORI

Na Mwandishi Wetu,Rome

UJUMBE wa Serikali ya India umekutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Serikali ya Tanzania, na Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa – FAO Katika Bara la Africa kujadiliana fursa za ushirikiano baina ya Tanzania na India kwenye nyanja ya uhifadhi wa Misitu na Wanyamapori.

Mazungumzo hayo yamefanyika jana Julai 24, 2024 katika ofisi za Makao makuu ya FAO, Rome nchini Italy yaliongozwa na Shri. Jitendra Kumar, Mkurugenzi Mkuu wa Misitu na Katibu Maalum katika Wizara ya Mazingira, Misitu, na Mabadiliko ya Tabianchi (MoEFCC) India. Huku Kamishna wa Uhifadhi – TFS Prof. Dos Santos Silayo ambaye ni makamu mwenyekiti wa Mkutano wa Kamati ya Misitu (COFO27) na mwakilishi wa Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Barani Afrika,akiongoza ujumbe kutoka nchini Tanzania.

Wajumbe wengine waliohudhuria mkutano huo kutoka India ni maafisa waandamizi wakiwemo Shri. R. Raghú Prasad, Inspekta Jenerali wa Misitu, na Shri. Kamal Ject Singh, Naibu Inspekta Jenerali wa Misitu kutoka MoEFCC, pamoja na Shri Anoop Singh, Mkurugenzi Mkuu wa Utafiti wa Misitu nchini India na baadhi ya maafisa wa ubalozi wao. Huku Upande wa Tanzania ukiwa na Dr. Elikana John, Afisa Mwandamizi na Mtalaam wa Misitu, Edward Kilawe, Mtanzania na Mwakilishi wa FAO Katika Bara la Africa yenye Makao Mkuu ya Jijini Accra Ghana.

TFS, Prof. Silayo anasema mazungumzo hayo yalijikita katika ushirikiano wa kimataifa katika kujenga uwezo wa tathmini ya rasilimali za misitu, ikiwa ni pamoja na upimaji na utafiti wa misitu, uendelezaji wa mfumo wa ufuatiliaji wa moto wa misitu kwa wakati sahihi, na ushiriki katika Umoja wa Kimataifa wa Wanyama Jamii ya Paka Wakubwa, unaohusisha Afrika Kusini, Ghana, Kenya, Zimbabwe, na Namibia.

“Kwa pamoja tumezungumza umuhimu wa nchi zetu mbili kushirikiana katika uhifadhi ikiwa ni mwendelezo wa mahusiano mazuri yaliyopo baina yaTanzania na India, kama yalivyotiwa msukumo na Waheshimiwa Viongozi wakuu wa nchi hizi!

Tumekubaliana kuanza mazungumzo ya kuiwezesha Tanzania kujiunga na umoja wa nchi zinazoweka nguvu pamoja kuhifadhi Wanyama jamii ya paka wakubwa (International Big Cat Alliance). Umoja huu utawezesha nchi zetu kubadilishana uzoefu, utalaam, teknologia na vifaa vitakavyowezesha uhifadhi na ufuatiliaji wa misitu na rasilimali za wanyamapori. Mazungumzo yanaendelea kufanikisha azma hii. Tunaishukuru ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Rome kwa kuratibu mazungumzo hayo.,” amesema.

Mkutano huo wa pande mbili, uliofanyika kandokando ya kikao cha 27 cha Kamati ya Misitu (COFO), ulitoa jukwaa kwa pande zote mbili kuchunguza njia za ushirikiano zitakazonufaisha sekta za misitu na wanyamapori.


Related Posts