LIGI soka ya Korosho Cup Cup inatarajia kuzinduliwa Agosti 10 mwaka huu katika Jimbo la Lulindi, Masasi, mkoani Mtwara huku zawadi nono zikitangazwa kwa washindi.
Mwandaaji na Mdhamini wa ligi hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Utalii 255 Community, Angelina Malembeka, amesema, bingwa atazawadiwa pikipiki ya magurudumu matatu maarufu kama guta yenye thamani ya sh. 6,000,000, kombe, jozi moja ya jezi, mpira mmoja na fedha taslimu sh. 100,000 za mafuta.
Malembeka, amesema,mshindi wa pili atapata kitita cha sh. 1,000,000, jozi moja ya jezi na mpira mmoja, huku mshindi wa watu akiondoka na sh.500,000 na mshindi wa nne akipata sh. 200,000.
“Golikipa bora atazawadiwa shilingi 50,000, mfungaji bora shilingi 50,000, kocha bora shilingi 50,000 na mwamuzi bora shilingi 50,000,”alieleza.
Malembeka ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu akiwakilisha Mkoa wa Kaskazini Unhuja, ameeleza kundi bora la ushangiliaji litaondoka na kitita cha sh.100,000.
“Timu zote zinazoshiriki zitapewa jezi jozi moja na mipira miwili. Waamuzi wote watapewa sare,”amesema.
Amebainisha, ligi hiyo itatimua vumbi katika vituo vitatu ambavyo ni Kata ya Namwanga, Kata ya Chiungutwa na Kata ya Mchauru.
“ Kila kituo tutakipa filimbi, kadi nyekundu na njano, kibao cha kubadilisha wachezaji, pampu ya kujaza mpira, nyavu za golini na beji za makapteni,”amebainisha.
Amesema kaulimbiu ya michuano hiyo inasema ni Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 ikilenga kuhamasisha wananchi wa Jimbo la Lulindi kushiriki uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Masasi, kimebariki michuano hiyo na kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi.
Mweka Hazina wa chama hicho,Japhari Lwenge, amesema ligi hiyo itashirikisha timu 14 kutoka kata 14 za Jimbo la Lulindi.
“Ligi itaanzia ngazi ya Kata kwa kushirikisha timu za mitaa kisha, kila kata itatoa timu moja itakayoshiriki michuano hiii,”amesema Lwenge.