Ujio wa ODM serikalini, mtihani mpya kwa Gachagua

Nairobi. Wakati Rais William Ruto akishika madaraka, naibu wake Geofrey Rigathi Gachagua alikuwa na nguvu na hakutaka kabisa kusikia wapinzani wakitaka mazungumzo na bosi wake.

Miongoni mwa kauli za majigambo zilizowahi kutolewa na Gachagua ni “Acha kazi ya kumlinda Rais kwangu. Ikiwa mtu yeyote atajaribu kukaribia Ikulu, nimeweka mitego kwenye kila njia inayowezekana wangechukua. Hakuna njia wanaweza kupita. Kwa hivyo, hakuna chochote cha kuwa na wasiwasi.”

Alimaanisha kuwa Serikali ya Kwanza ya Kenya haitakubali maridhiano yaliyofanywa na Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga mwaka 2018 kurudia tena kwenye utawala wa Rais Ruto.

Kumbe Gachagua alisahau kauli iliyowahi kutolewa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Harold Wilson kwamba mwaka mmoja ni muda mrefu sana katika siasa, kwani lolote linaweza kutokea.

Vuguvugu la maandamano ya vijana wanaojiita Gen-Z yamebadilisha kabisa sura ya siasa za Kenya ma hatimaye Rais Ruto anapita njia ile ile aliyopita Kenyatta.

Hilo linadhihirishwa na mabadiliko ya baraza lake la mawaziri likihusisha makada wa chama cha ODM.

Katika uteuzi huo, Rais Ruto amemteua John Mbadi wa ODM kuwa Waziri wa Fedha, Opiyo Wandayi kuwa Waziri wa Nishati na Petroli, Ali Hassan Joho kuwa Waziri wa Madini, Uchumi wa Bahari na Masuala ya Baharini na Wycliffe Oparanya kuwa Waziri wa Maendeleo ya Ushirika na Biashara Ndogo, Ndogo na za Kati (MSME).

Uteuzi wa Dk Ruto kwa wapinzani katika baraza lake la mawaziri umebadilisha mwenendo wa siasa nchini humo na unaonekana kumvuruga Naibu Rais Gachagua.

Hata wakati maandamano yamepamba moto hadi Rais Ruto kuuondoa muswada wa fedha wa mwaka 2024, Gachagua alikimbilia kumlaumu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Ujasusi za Kitaifa (NIS), Noordin Haji, akimtuhumu kwa kumpa Rais taarifa isiyo sahihi.

Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wanaona uhusiano wa kutatanisha kati ya Rais na naibu wake ulihitaji uwepo wa Odinga.

Wanasema Rais amekuwa akipigana kwenye pande mbili, upinzani kutoka ndani ya Serikali yake mwenyewe na wimbi la vijana wa kizazi cha Gen-Z ambao wameapa kumwondoa madarakani, hivyo kuwaleta wanachama wa ODM kunakusudiwa kuzuia meli yake kuzama.

Hata hivyo, hatua hiyo haijawafurahisha baadhi ya vigogo wa upinzani katika kambi ya Azimio, akiwamo Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Eugene Wamalwa na Jeremiah Kioni.

Kwa upande mwingine, kuingia kwa Odinga katika Serikali kunampa Ruto nafuu fulani, kwani anawaleta wote wa jamii ya Luo na pamoja na Mudavadi, Spika Moses Wetang’ula, ambaye bado yuko Kenya Kwanza, kura nyingi za kabila la Luhya.

Imetafsiriwa kutoka Nation.Africa.

Related Posts