Sababu Kanda ya Ziwa kuwa kinara wizi wa watoto

Dar es Salaam. Kanda ya Ziwa inakabiliwa na matukio ya wizi wa watoto, ripoti mpya imebainisha.

Ripoti ya takwimu za uhalifu na usalama barabarani ya mwaka 2023 iliyochapishwa na Jeshi la Polisi Tanzania kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonyesha kuwa mikoa 40 ya kipolisi nchini ilisajili jumla ya matukio 73 ya wizi wa watoto mwaka jana.

Hata hivyo, kati ya idadi hiyo, mikoa saba ya kipolisi ya Kanda ya Ziwa pekee ilichangia matukio 35, sawa na karibu asilimia 48 ya idadi yote.

Mara na Kagera iliongoza katika orodha hiyo, kila moja ikiwa na matukio manane ya wizi wa watoto mwaka 2023. Mwanza na Geita ilifuatia katika nafasi ya tatu na nne, ikiwa na matukio saba na matano mtawalia.

Simiyu iliripoti matukio matatu ya wizi wa watoto  wakati Shinyanga na Tarime-Rorya ilikuwa na matukio mawili kila mmoja.

Wadadisi wa mambo wanasema hali hiyo inatokana na sababu mbalimbali zikiwemo imani za kishirikina.

“Inadaiwa kuwa watoto hawa wanatolewa kafara, hasa katika maeneo ya karibu na migodi. Imani hizo za kishirikina zinathibitishwa na taarifa za watoto waliokutwa wamekufa na sehemu za miili yao hasa sehemu za siri, zikiondolewa. Hii inaashiria kwamba vitendo hivyo ni vya kitamaduni,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga.

Amesema baadhi ya watu wasio waadilifu wana imani kuwa wanaweza kupata fedha au nafasi za uongozi/kuchaguliwa kwa kuwatoa kafara binadamu wenzao.

Amependekeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, ni muhimu kuimarisha uelewa wa jamii na utekelezaji wa sheria katika mikoa.

“Ninaiomba Serikali kuandaa mkakati wa dharura ili kukabiliana na suala hili kwa ufanisi na haraka,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi ameeleza kuwa hadi sasa, hakutakiwi kuwe na visingizio kuhusiana na kinachochochea tabia hizo katika Kanda ya Ziwa. Badala yake, kuwe na ripoti rasmi ya polisi kuhusu chanzo cha matukio haya.

“Ni jukumu la Jeshi la Polisi kufanya utafiti na kutoa ripoti kuhusu suala hilo. Hapo ndipo itakuwa rahisi kwa wadau wengine kutafuta njia bora za kuzuia vitendo hivi,” amesema.

Hata hivyo, amesisitiza pia kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kuwafuatilia kwa karibu watoto kwani wao ni miongoni mwa makundi yaliyo hatarini na wanategemea ulinzi wa wazazi, walezi na jamii.

“Kila mtu, kwa njia yake, anapaswa kuguswa na hatari inayoletwa na watoto kupitia utekaji nyara na anapaswa kuongeza juhudi za kuwalinda, kwani wamekuwa wakilengwa sana na vitendo kama hivyo,” amesema.

Wanaharakati wa haki za binadamu, pia, wanapendekeza kusainiwa kwa mikataba ya kimataifa inayohusu masuala ya upotevu na ukatili, kuongezeka kwa uwajibikaji, na utoaji wa elimu ili kumaliza tatizo la wizi wa watoto Kanda ya Ziwa.

Mratibu wa Umoja wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema kuna haja kwa Taifa kusaini mikataba ya kimataifa inayosimamia masuala ya watu kupotea na ukatili.

“Mikataba hii imeweka utaratibu mzuri wa kufuatilia masuala haya na pia itaongeza uwajibikaji, kwani moja ya sababu za kuendelea kwa vitendo hivyo nchini ni kutokuwepo kwa uwajibikaji miongoni mwa polisi na viongozi katika kufuatilia masuala haya,” amesema.

Ameeleza kuwa kuwepo kwa sheria kali zinazolenga masuala haya kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufupisha mchakato wa kuwawajibisha wahusika, kwani mikataba hii inaagiza kuundwa kwa kamati maalumu zinazohusika na kufuatilia masuala ya ukatili na watu kupotea.

“Kukuza elimu kwa jamii ni muhimu kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kujilinda wao wenyewe na watoto. Kuongezeka kwa umakini kunaweza kusaidia katika kushughulikia masuala yanayoendelea huku mamlaka zikijitahidi kutokomeza vitendo hivi,” amesema.

Amesema katika Kanda ya Ziwa, vitendo hivyo na vingine vya kikatili vimeshamiri kwa muda mrefu, na ni wakati mwafaka kuchukua hatua madhubuti za kupunguza na hatimaye kuvitokomeza kabisa.

“Imekuwa kawaida sana kusikia juu ya ukatili katika Kanda wa Ziwa. Hatupaswi kuridhika, badala yake tufanye kazi ya kutokomeza vitendo hivi na kuhakikisha usalama kwa kila mtu hasa watoto,” amesema.

Related Posts