Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson amuapisha Balozi Mohamed Thabit Kombo

Na Esther Mnyika, Mtanzania

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, leo amemuapisha Balozi Mohamed Thabit Kombo na kumtaka kufanya kazi aliyokusudiwa ili kukamilisha mipango mingi ya maendeleo iliyoanzishwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza baada ya kumuapisha katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, Dk. Tulia alisema kuwa kuteuliwa kwa Balozi Kombo kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kuendeleza mipango mingi ya maendeleo iliyowekwa na Rais.

“Rais Dk. Samia ana mipango mingi na mingi ameiweka wazi, hivyo anawategemea ninyi ili kuweza kuitekeleza kwa ustawi wa Taifa,” alisema Dk. Tulia.

Alisema kuwa uapisho huo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 30(2)(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Februari 2023, ambapo inatamka kuwa Mbunge kabla ya kuanza kazi ataapishwa na Spika.

Aidha, Dk. Tulia alifafanua kuwa sheria hiyo imempa mamlaka Spika kuchagua eneo la kumuapishia kama hakuna mkutano wa Bunge unaoendelea na baadaye kutoa taarifa bungeni kwenye kikao cha kwanza.

Kombo aliteuliwa na Rais Dk. Samia kuwa Mbunge na Waziri Julai 21, 2024, baada ya kutenguliwa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Januari Makamba.

Baadhi ya wabunge walioshiriki katika hafla hiyo ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stegomena Tax, na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Londo.

Related Posts