Wacheza gofu kuchuana ‘KCB East Africa Golf Tour

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Zaidi ya wachezaji 150 wanatarajiwa kuchuana katika shindano la wazi la mchezo wa gofu “KCB East Africa Golf Tour”, litalofanyika Agosti 3,2024 kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu Lugalo, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 24,2024,Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo , amesema lengo la shindano hilo ni kupata wachezaji wanne watakaoiwakilisha Tanzania katika fainali za mashindano hayo kwa Afrika Mashariki itakayofanyika Desemba, mwaka huu nchini Kenya.

“Wachezaji hao wanne wakishinda kule Kenya klabu nayo itanufaika, itakuwa na zawadi ambayo itatufanya tujivunie. Itakuwa ni shindano la siku moja na wachezaji wengi wamedhibitisha kushiriki,” amesema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa KCB Benki Tanzania, Cosmas Kimario ambao ni wadhamini wa mashindano hayo, amesema wamechagua kufanyia Lugalo kutokana na ubora wa viwanja vyake.

Ameeleza kuwa mashindano hayo yamenza Januari na yameshafanyika katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na sasa ni zamu ya Tanzania ili kupata wachezaji watakaongana na wenzao kwenye fainali nchini Kenya.

“Udhamini huu ni sehemu ya agenda ya KCB kuwekeza katika jamii kupitia michezo na misaada mbalimbali ya kijamii,” amesema.

Akizungumzia mfumo utakaotumika katika michuano hiyo, Nahodha wa Lugalo, Meja Japhet Lugalo amesema watacheza kwa mtindo wa “Stable Ford” ambapo mshindi atapatikana kwa kuhesabu mashimo kwa pointi.

Related Posts