Simba ya Fadlu mwendo wa boli, Njia zilezile za Sven, Mogella atoa tahadhari

SIMBA imeendelea kusukwa upya chini ya kocha mpya Fadlu Davids, lakini kama kuna mambo hataki kuona yanafanywa na mchezaji wake ni kutembea uwanjani, akitaka muda wote wawe wanakimbia kwa kasi, huku wakitembeza boli mwanzo mwisho kuelekea langoni mwa mpinzani.

Kikosi hicho hicho kimeweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya jijini Ismailia, Misri na inaelezwa Fadlu ameanza kuibadilisha kabisa katika falsafa ya uchezaji akirudisha ile iliyokuwa ikitumiwa zaidi na kocha Mbelgiji aliyewahi kuifundisha timu hiyo, Sven Vandenbroeck.

Katika mazoezi ya kocha huyo kutoka Afrika Kusini aliyetua Msimbazi akitokea Raja Casablanca ya Morocco akimpokea, Abdelhak Benchikha, kwanza ametaka kuona timu hiyo inacheza soka la haraka kwenda kuwabana wapinzani langoni mwao, kabla hawajajipanga kisawasawa mara kikosi hicho kikiunasa mpira.

Inapofika langoni, kocha huyo anayefundisha kwa vitendo na amekuwa mkali kwa washambuliaji, anataka kuhakikisha mabao yanapatikana hatua ambayo imekuwa ikiwaweka katika wakati mgumu washambuliaji wa timu hiyo akiwemo Steven Mukwala na Freddy Michael.

Kocha huyo hataki kuona wachezaji wa timu hiyo wanatembea kwa muda mrefu wakiwa uwanjani hasa wa eneo la kiungo na wengine wa mbele akitaka kama timu yake ina mpira kila moja anashiriki kutengeneza mashambulizi.

Mmoja wa wachezaji waandamizi wa kikosi hicho, aliliambia Mwanaspoti kuwa, tangu Fadlu aungane na timu amekuwa akiifanya timu icheze sana mpira na kushambulia kwa kazi kama ilivyokuwa enzi za Sven.

Nyota huyo alisema katika mbinu anazofundisha, ni kwamba hata timu ikipoteza mpira mambo yanatakiwa kubadilika kwa wote kushiriki kuusaka na kuupokonya kwa haraka na ambaye hakabi humgeukia kwa hasira.

Wachezaji wenye kasi wamekuwa wakipata mteremko kwa kocha huyo, lakini wale wenye kasi ndogo wamekuwa wakikutana na wakati mgumu ingawa amekuwa akiwapa nafasi ya kuwaelekeza kwa utaratibu.

Licha ya kupiga tizi la maana ni kwamba hadi sasa Fadlu bado hajakipata kikosi cha kwanza cha timu hiyo ambapo watu wachache pekee wana uhakika kiasi wakiwemo mabeki wawili Che Malone Fondoh, Karaboue Chamou na viungo Jean Ahoua na Joshua Mutale huku wengine wakiendelea kuchuana na kupishana.

Fadlu anaendelea kuwasoma zaidi wachezaji hao na wikiendi hii watashuka uwanjani kucheza mechi nyingine mbili kabla ya kujiandaa kurejea nchini mapema wiki ijayo kujiandaa na Tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 3, kisha kujipanga kwa mechi mbili za Ngao ya Jamii ikiwamo ile ya Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga itakayopigwa Agosti 8 kuanzia saa 1:00 usiku Kwa Mkapa.

Katika mechi za msimu uliopita za michuano hiyo, Simba ilianza kwa kuitambia Singida Fountain Gate kwa penalti kisha kucheza fainali na Yanga iliyokuwa imeifunga Azam kwa mabao 2-0 na dakika 120 ziliisha kwa timu hizo kutofungana na kulazimika kupigiana penalti na Mnyama akapata 3-1 na kurejesha tuzo hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Wananchi kwa misimu miwili mfululizo nyuma.

Nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ amekisifia kikosi kipya cha Simba, lakini akatoa angalizo kwa kusema ni ngumu kwa timu yenye idadi kubwa ya wachezaji wapya kufanya vizuri ndani ya kipindi kifupi, hivyo ni vyema mashabiki wa Msimbazi kutambua hilo wakati kocha wao, Fadlu Davids akiendelea kukisuka upya.

“Ninachokiona kwa sasa kocha anapambana kupata muunganiko, hili ni jambo ambalo huwa linahitaji muda, kama ikitokea wakielewana kwa haraka hiyo itakuwa bahati, natamani mashabiki wa Simba waonyeshe ukomavu kwa kuwa nyuma ya timu yao hasa kipindi hiki ambacho inajengwa,” alisema Mogella aliyewahi kuwika na timu kadhaa ikiwamo Yanga na kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm amewataja Steven Mukwala na Jean Charles Ahoua kama maingizo mapya katika kikosi cha Simba ambayo yanaweza kurahisisha kazi kwa kocha Fadlu kutokana na ubora ambao ameona kutoka kwao, amekuwa akivutiwa nao.

“Makocha tumekuwa wafuatiliaji, nipo Ghana lakini huwa nafuatilia ligi za nchi mbalimbali, najua kuwa Simba kwa sasa wanajaribu kukijenga upya kikosi chao, wamefanya usajili mzuri mfano Mukwala amefanya vizuri hapa (Ghana) ni kati ya washambuliaji hatari, namtabiria mazuri,” alisema Hans aliyewahi kuzinoa Singida United na Azam aliyeongeza;

“Ahoua naye amefanya vizuri Ivory Coast, jambo ambalo linaweza kuwa changamoto kwa Fadlu ni moja tu ambalo ni kupata kile kilichobora kwa kila mchezaji, kuwa na wachezaji wazuri ni moja lakini kupata kilichobora kwa wachezaji katika muundo wa timu vile anataka icheze ni jambo jingine, akifaulu hapo huenda Simba ikarejea katika makali yake.”

Kocha wa timu za vijana wa Azam FC, Mohamed Badru anaamini kocha wa Simba, Fadlu anaweza kukabiliwa na presha kutoka kwa mashabiki kutokana na upya wa kikosi chake ambacho kiuhalisi anahitaji muda kuanzia miezi miwili hadi mitatu kukisuka kuwa bora zaidi ulikilinganisha na wapinzani wao, Yanga ambao wanaonekana kuwa moto wa kuotea mbali.

“Maandalizi ya msimu ujao ‘pre season’yatatoa picha kwa Fadlu kuona wapi ambapo anatakiwa kuongeza nguvu kwa namna alivyokiona kikosi chake katika michezo ya kirafiki, kiukweli Simba imefanya usajili mzuri tena wa wachezaji wenye umri mdogo ambao wametoka kufanya vizuri walipotoka hivyo kama wakijipata tu basi wana nafasi ya kufanya makubwa kwa miaka mingi,” alisema kocha huyo.

Related Posts