Miongoni mwa maswali ambayo ni kawaida kukutana nayo kwa wanawake wanaofanyiwa upasuaji wa kuondoa nyumba ya uzazi au kizazi, ni kuhusu kushiriki tendo la ndoa, mara baada ya upasuaji huo.
Upasuaji huu kitabibu hujulikana kama Hysterectomy, hufanyika kwa sababu za kiafya au binafsi. Ieleweke upasuaji huu hauondoi sehemu za uke ambazo ndizo zinazohusika katika tendo na misisimko yake.
Uainishaji upasuaji huu unategemeana na namna ulivyofanyika na kiungo kilichoondolewa. Aina ya kwanza hujulikana kama Total Hysterectomy, ambapo nyumba na mlango wa uzazi huondolewa.
Kama mlango wa uzazi utaachwa ndipo aina ya pili ya upasuaji hupatikana unaojulikana kama Subtotal Hysterectomy. Na pia mirija na kokwa za kike, yaani ovari zinaweza kuondolewa.
Wakati wa upasuaji viungo hivi vitaondolewa kuendana na tatizo la mgonjwa au sababu elekezi ya kufanya upasuaji huu.
Hivyo basi kuondolewa nyumba ya uzazi, mlango wa uzazi, mirija au kokwa za kike hakumfanyi mwanamke kukosa hisia nzuri wakati wa kujamiiana wala kushindwa kufika kileleni baada ya kupona jeraha.
Hii ni kwa sababu upasuaji huu haugusi wala kuondoa sehemu za ukeni, zenye kuchochea msisimko wa kujamiiana.
Ni kweli wakati wa upasuaji yapo madhara machache, ikiwamo kujeruhiwa kwa baadhi ya mishipa ya damu na ya fahamu inayohusika na kuleta misisimko ya hamu ya kujamiiana.
Kwa kawaida mwanamke aliyefanyiwa upasuaji huu atahitajika kutojamiiana na mwenza wake kwa kipindi cha muda wa wiki 4 hadi 6.
Muda huu ni kwa ajili ya jeraha kupona kabisa na pia kutoa nafasi kwa uchafu kutoka au damu kukoma kuvuja kupitia ukeni.
Kama atajihisi hayuko tayari kujamiiana baada ya kipindi kilichopangwa na watalaamu wa afya asiwe na wasiwasi, kwani kila mwanamke ana matokeo tofauti baada ya upasuaji huu.
Ikumbukwe kuwa kuondoa kiungo hiki mwilini kwa mwanamke huwaacha wakiwa na majeraha ya kihisia, ikiwamo huzuni au sonona (depression) kutokana na kuondokewa na kiungo hicho.
Matukio haya humfanya kuwa na shinikizo la kiakili, kuumia kihisia na kumfanya kuwa mwoga kujamiiana. Hii ndiyo sababu kubwa ya wao kukosa hamu ya kujamiiana.
Pia anaweza kupata matatizo mengine ya kujamiiana, ikiwamo uke kuwa mkavu, kutofika kileleni, maumivu wakati wa kujamiiana na kutoka damu mara baada ya kujamiiana.
Vilevile kuvurugika kwa hisia zao kunachangiwa na kujikita zaidi katika kushikamana na maelekezo ya daktari wakati wanapojiuguza nyumbani, kama vile kuelekezwa kutumia dawa, vyakula, shughuli asizotakiwa kufanya na mazoezi mepesi ya kufanya.
Vitu hivi vinaweza kuhamisha akili yake na asijikite katika hisia za mapenzi.
Kwa wanawake wa umri wowote ule ambao wamefanyiwa upasuaji huu na kuondolewa kokwa za kike na nyumba ya uzazi, hii itasababisha kufikia ukomo wa hedhi kwa kuwa zile homoni zinazoleta mizunguko ya hedhi hazitazalishwa tena.
Athari yake ni pamoja na viwango vya homoni za kike kubadilika, hii ina athari katika maisha ya mwanamke kwa upande wa kujamiiana.
Inashauriwa anapoona mabadiliko haya kufika mapema katika huduma za afya au kumjulisha daktari wake ili kupata ushauri na matibabu.
Ukiachana na hayo, faida ya kuondolewa kizazi kwa wanawake watu wazima, kunawaepusha na saratani ya nyumba ya uzazi na magonjwa mengine katika nyumba ya uzazi.