Kazi imeanza Olimpiki 2024 Paris

MICHEZO ya Olimpiki Paris 2024 inazinduliwa rasmi leo Ijumaa, huku ikitazamiwa kuvuta hisia za wadau mbalimbali wa michezo na burudani kote duniani.

Michezo hiyo inarejea katika mji mkuu huo wa Ufaransa baada ya kupita miaka 100 na kuwa jiji la pili baada ya London kuandaa Olimpiki ya majira ya joto kwa mara ya tatu.

Olimpiki hufanyika kila baada ya miaka minne na michezo ya mwisho huko Tokyo ilikuwa ni mwaka 2020 japo ilifanyika 2021, kwani ilicheleweshwa kwa mwaka mmoja kutokana na janga la Uviko-19 na ilifanyika kwa kiasi kikubwa bila watazamaji, kuanzia maeneo ya kumbi hadi matukio ya michezo.

Kwenye makala ya 33 ya michezo hiyo, Mwanaspoti inakupitisha katika baadhi ya dondoo ili kujua kuhusu michezo hiyo ya Olimpiki ya Paris 2024.

Wakati michezo ya Olimpiki ikitazamiwa kuanza leo, baadhi ya michezo tayari imeanza kabla ya sherehe za ufunguzi rasmi, michezo hiyo ni Soka na Raga ya wachezaji saba ambayo ilianza Jumatano, pamoja na vishale na mpira wa mikono ambayo ilianza jana Alhamisi.

Sherehe za ufunguzi zitafanyika katika mji wa Seine, jijini Paris kuanzia saa 11:30 jioni kwa saa za Ufaransa, huku ikitazamiwa michezo hiyo kufanyika katika viwanja 35 kwa kushirikisha wachezaji 10,714 wanaowakilisha nchi 206 katika michezo 32, pia kutakuwa na matukio ya kimichezo 329 kwa siku 16 za michezo hiyo maarufu duniani.

Wanamichezo hao 10,714 wanatazamiwa kuchuana vikali kuwania medali 329 za dhahabu na hadi sasa jumla ya medali 5,084 ya aina zote zimetengenezwa.

Kama kawaida kila mji mwenyeji wa Olimpiki huunda medali za kipekee zinazoonyesha utamaduni na historia na katika medali za Olimpiki za Paris kila moja itajumuisha kipande cha chuma na cha asili kutoka kwa mnara wa Eiffel na hadi sasa

Matukio mengi kati ya 329 yatafanyika kote Paris na eneo lake la jiji kuu, lakini mengine yataandaliwa mamia ya kilomita kutoka jiji hilo na michezo ya kuteleza katika barafu yataandaliwa umbali wa kilomita 15,000 (maili 9,300) huko French Polynesia.

Viwanja 35 ambavyo vitaandaa michezo hiyo ni Aquatics Centre, Bercy Arena, Bordeaux , Champ-de-Mars Arena, Chateau de Versailles, Chateauroux Shooting Centre, Eiffel Tower, Elancourt Hill, Geoffery-Guichard, Grand Palais, Hotel de Ville, Invalides, La Beaujoire, La Concorde na  Le Bourget Sport Climbing Venue.

Zingine ni Golf National, Lyon, Marseille Marina, Marseille, Nice, North Paris Arena, Parc de Princes, Paris La Defense Arena, Pierre Mauroy Stadium, Pont Alexandre III, Porte de La Chappelle Arena, Stade Roland Garros, Saint-Quentin-en-Yvelines Velodrome and BMX Stadium, South Paris Arena, Stade de France, Teahupo’o, The Trocadero, Vaires-sur-Marne Nautical na uwanja wa Yves-du-Manoir.

Tanzania nayo ni miongoni mwa nchi 206 zinazoshiriki Olimpiki, huku ikiwa na wachezaji saba katika michezo mitatu ambayo ni Riadha, Judo na Kuogelea.

Wachezaji hao ni Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Jackline Sakilu na Magdalena Shauri kwa upande wa riadha, Mlugu Thomas wa Judo na Collins Saliboko na Sophia Lattif wa kuogelea.

Nyota hao wanatazamiwa kupambana na kuvunja rekodi zilizodumu kwa miaka 44 tangu Tanzania ilipopata medali ya kwanza na ya mwisho kupitia ya wachezaji wake Suleiman Nyambui na Filbert Bayi.

Nyambui alishika nafasi ya pili katika mbio za mita 5000 na kupata medali ya fedha sawa na Filbert Bay aliyeshika nafasi ya pili mbio za mita 3000 na ilikuwa ni Olimpiki ya mwaka 1980 Moscow Urusi.

Olimpiki ya mwaka huu itakuwa tofauti na nyingine zilizopita na ya sasa washindi wa medali ya dhahabu katika mashindano yote watapata zawadi ya fedha.

Jumla ya zawadi ya Dola 2.4 milioni ambao ni mgao wa mapato kutoka Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), hupokelewa na Shirikisho la Riadha la Dunia kila baada ya miaka minne.

Kiasi hicho kitatumika kuwazawadia wanariadha watakaoshinda medali ya dhahabu katika mashindano yote 48 na kila mmoja atapata Dola za Marekani 50,000 (Sh135 milioni).

Wakati tukijiandaa na sherehe za ufunguzi, rekodi zinaonyesha Marekani ndiyo imeshinda medali nyingi zaidi kati ya kamati zote za kitaifa za Olimpiki (NOCs).

Imebeba medali nyingi zaidi katika makala 18 kati ya 28 ya michezo ya Olimpiki iliyoshiriki na kuifanya kuwa timu iliyofanikiwa zaidi katika historia ya mashindano hayo, ikiwa na Jumla ya medali 2,667 kati ya hizo medali 1,077 za dhahabu, 840 za fedha na 750 za shaba.

Wakati michezo ya Olimpiki za Paris ikifanyika kwa mara ya 33, historia inaonyesha sherehe ya kwanza ya michezo hiyo ya kisasa ilifanyika Ugiriki na kuwavutia wanamichezo wengi na nchi 14 ambazo ni Ugiriki, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Australia, Chile, Bulgaria, Austria, Denmark, Hungary, Italia, Sweden, Uswisi na Marekani ndizo zilizishiriki.

Linapokuja suala la medali kwenye michezo hii, kuna wanamichezo wamezichukua mara nyingi sana na kuweka rekodi ambayo hadi leo haijawahi kuvunjwa.

Mwogeleaji wa Marekani Michael Phelps ndiye mwana Olimpiki aliyeng’ara zaidi kuliko wengine wote, akiwa na medali 28, 23 zikiwa za dhahabu. Pia ndiye mwanariadha wa kwanza kushinda medali 8 za dhahabu kwenye Olimpiki moja.

Nafasi ya pili inashikiliwa na mwanamichezo ya mitindo (gymnast), kutoka Soviet, Larisa Latynina mwenye medali 18, akifuatiwa na Marit Bjørgen wa Norway mwenye medali 15.

Wakati ulimwengu ukiitazama Paris kwa michezo ya Olimpiki ya 2024 inayoanza wiki hii, wanamichezo wa Kiafrika nao wana historia ya kujivunia kwenye michezo hiyo.

Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto ina historia ndefu ya kuleta matukio ya kusisimua na maonyesho ya kuvutia huku wanariadha kutoka kote ulimwenguni wakiacha alama zao katika michezo tofauti.

Nigeria inatambulika kama mojawapo ya mataifa yanayopenda michezo zaidi barani Afrika, ikijivunia rekodi ya mafanikio katika nyanja mbalimbali na matukio ili kuthibitisha sifa yake.

Mojawapo ya matukio ya dhahabu barani Afrika kwenye Olimpiki ilikuwa mwaka 1996 Atlanta, Marekani na Chioma Ajunwa alikuwa mwanamke wa kwanza mweusi Mwafrika kushinda medali ya dhahabu ya Olimpiki kwenye mbio za viwanjani, pia, kikosi cha Nigeria cha ‘Dream Team’ chini ya umri wa miaka 23 kiliishangaza dunia na kuwa taifa la kwanza la Afrika kushinda medali ya dhahabu ya Olimpiki katika soka baada ya kuichapa Brazil ambayo ilijaa nyota, katika mchezo wa nusu fainali kisha kuifunga Argentina kwenye fainali.

Pia, kwenye Michezo ya Olimpiki ya 2000 huko Sydney, Cameroon ilishinda Uhispania katika fainali na kuwa timu ya pili ya Kiafrika kushinda medali ya dhahabu kwenye mchezo wa soka kwa wanaume.

Katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020, Eliud Kipchoge wa Kenya aliimarisha nafasi yake kama mwanariadha bora zaidi wa marathon wa wakati wote. Akawa mtu wa tatu katika historia kutwaa mataji mawili ya mbio za Olimpiki.

Vile vile, mzalendo Faith Kipyegon alionyesha uthabiti na uthubutu, na kushinda medali za dhahabu huko Rio 2016 na Tokyo 2020.

Mwanariadha wa mbio ndefu wa Ethiopia Kenenisa Bekele alishinda fainali zote za mita 5000 na 10000 na kuweka rekodi katika michezo ya Olimpiki ya Beijing ya 2008.

Kwa mujibu wa Olympedia, nchi za Afrika zimejikusanyia jumla ya medali 286 tangu mwaka 1956.

Vinara ni Kenya wakiwa na medali kwa 113, medali 35 za dhahabu, 42 fedha na 36 shaba, ikifuatiwa na Afrika Kusini kwa Medali 89,27 dhahabu,33 fedha na 29 shaba huku Ethiopia ikishika nafasi ya tatu kwa medali 58, dhahabu 23 sawa na shaba pamoja na medali 12 za fedha.

Wakati wengi wanasubiri sherehe za ufunguzi za michezo hiyo taarifa zinaeleza wanamuziki nyota wa kimataifa Céline Dion na Lady Gaga ndio watatumbuiza kwenye ufunguzi na tayari wamewasili Paris.

Related Posts