Musukuma ataka ‘mashangingi’ ya Serikali yafungwe mfumo wa gesi

Dodoma. Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma ameshauri magari ya mawaziri yafungwe mfumo wa gesi (CNG) kupunguza matumizi ya mafuta.

Musukuma amesema hayo leo Alhamisi Aprili 25, 2024 alipochangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2024/25, iliyowasilishwa Aprili 24,2024 na waziri wa wizara hiyo, Dk Doto Biteko. 

Amesema kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam kwa Toyota Land Cruiser V8 mafuta yanayotumika ni ya Sh500, 000 lakini ukitumia gesi ni Sh94, 000 kwenda na kurudi.

Musukuma amesema kwa kuwa wanahangaika sana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu matumizi mabaya ya Serikali, anashauri magari yote ya mawaziri yafungwe mfumo wa gesi ili kupunguza gharama.

“Kwa sababu sasa hivi muda mwingi mko Dar es Salaam, mpo Dodoma sasa kwa kubana matumizi mkiyafunga mitungi kule nyuma msafiri kila wiki kwenda Dar es Salaam na kurudi, Serikali itakuwa ina save (inapunguza) matumizi,” amesema.

Mbali na hilo, amezungumzia adha wanayopata wenye magari tente mfumo huo wanapoenda kujaza gesi.

Amesema mtu analazimika kwenda kituo kati ya viwili vya Dar es Salaam saa 9.00 usiku.

“Tumefika pale saa 8.00 mchana watu wanaongea kutuelimisha. Wale watu waliopanga foleni wanasema hivi, hawa ni wabunge au ni kina nani, wamekuja kufanya nini, sisi hatutaki wabunge tunataka gesi,” amesema.

Amesema mtu anakaa saa tisa kwenye foleni ya gesi.

Dk Biteko ambaye pia naibu waziri mkuu alipowasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo jana Aprili 24, 2024 alisema hatua zinachukuliwa kuwezesha vyombo vya moto vinavyomilikiwa na Serikali kutumia CNG.

Alisema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA) zinaendelea na taratibu za kumpata mshauri mwelekezi wa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa michoro ya kihandisi na tathmini ya athari ya mazingira na jamii, ili kuwezesha GPSA kujenga vituo vya CNG katika bohari za Dar es Salaam na Dodoma.

Hatua hiyo, alisema itawezesha vyombo vya moto vinavyomilikiwa na Serikali kutumia CNG.

Dk Biteko alisema watakamilisha ujenzi wa vituo vya CNG (kituo mama katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vituo vidogo vya Kairuki na Muhimbili, mkoani Dar es Salaam.

Alisema Serikali imejipanga kununua vituo vitano vya CNG vinavyohamishika vitakavyotoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam.

“Sekta binafsi itaendelea kushiriki katika ujenzi wa vituo vya CNG na karakana za kubadilisha mifumo ya matumizi ya nishati ya gesi asilia kwenye magari,” alisema.

Alisema sekta binafsi imeendelea kutumia fursa ya matumizi ya CNG katika vyombo vya moto kwa kujenga vituo Dar es Salaam na Pwani, pamoja na karakana nane za kubadilisha mifumo ya matumizi ya CNG kwenye magari, ambayo ni nyenzo muhimu ya kuchochea matumizi ya gesi katika magari.

Related Posts