SILINDE AGAWA MICHE BORA YA KAHAWA KWA WAKULIMA WA JIMBO LA MOSHI VIJIJINI.

NA WILLIUM PAUL, MOSHI.

KATIKA kuhakikisha wakulima wa zao la Kahawa katika Jimbo la Moshi vijijini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wananufaika na Kilimo hicho, Mbunge wa Jimbo hilo Prof. Patrick Ndakidemi alimualika Naibu Waziri wa Kilimo, David Ernest Silinde kugawa miche ya kisasa ya kahawa kwa wakulima wa Jimbo hilo.

Hafla hiyo ilifanyika katika Kata ya Kibosho Magharibi, na iliwashirikisha viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya, Naibu Mrajis wa Ushirika mkoani Kilimanjaro, Afisa Tawala wa Wilaya ya Moshi, Afisa Tarafa wa Kibosho, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Moshi, Afisa Ugavi wa Halmashauri ya Moshi, viongozi wa vyama vya msingi kutoka Jimboni Moshi Vijijini, Madiwani na viongozi wengine wa Serikali.

Akiongea katika hafla hiyo, Ndakidemi aliishukuru sana Bodi ya Kahawa Tanzania kwa kumpatia miche milioni moja ambayo itasambazwa katika jimbo lake la Moshi Vijijini.

Alimshukuru sana Naibu Waziri wa Kilimo kwa kukubali kuja kukabidhi miche hiyo kwa wakulima na wadau wengine wa zao la Kahawa kwa niaba ya Serikali.

Miche hiyo Chotara kutoka Kituo cha Utafiti wa zao la Kahawa Lyamungo imezalishwa na kutolewa bure kwa wakulima na Bodi ya Kahawa Tanzania.

Akikabidhi miche hiyo, Naibu Waziri Silinde aliishukuru sana Bodi ya Kahawa Tanzania kwa kazi nzuri wanayofanya kuwasaidia wakulima kupata miche bora ya zao la Kahawa nchi nzima.

Silinde aliahidi kwamba atarudi mkoani Kilimanjaro kabla ya mwisho wa mwaka kuja kusikiliza kero za Ushirika.

Related Posts