Uchunguzi safari ya China ya DED wakamilika

Geita. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Geita imekamilisha uchunguzi safari ya China aliyokwenda aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi.

Uchunguzi huo ulioanza mwanzoni mwa Novemba 2023, ulitokana na agizo la aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe la kuitaka Taasisi hiyo kuchunguza safari ya mkurugenzi huyo kama ilikuwa na masilahi ya halmashauri au ni maslahi binafsi.

Pia, aliitaka taasisi hiyo kubainisha kama matumizi ya safari hiyo yalitokana na fedha za halmashauri au ni za binafsi na endapo watabaini alitumia fedha za halmashauri, zirejeshwe na zielekezwe kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumza leo Aprili 25, 2024 wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa miezi mitatu iliyopita, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Azza Mtaita amesema uchunguzi umekamilika, kwa sasa jalada lipo kwenye hatua nyingine ya kupata maoni ya kisheria ili hatua nyingine ziweze kufikiwa.

Hata hivyo, Mtaita hakueleza kilichobainika katika uchunguzi huo.

Zahra aliyehudumu kama mkurugenzi wa mji wa Geita kwa zaidi ya miaka miwili na Desemba 2023 alihamishwa kwenda Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro wakati uchunguzi huo ukiendelea.

Akizungumzia ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Mtaita amesema kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, taasisi hiyo imefuatilia miradi 24 yenye thamani ya Sh27.1 na kati ya hiyo 11 imebainika kuwa na upungufu unaoweza kufifisha ubora wake.

Miongoni mwa upungufu walioubaini ni wa makandarasi kuchelewa kusaini mikataba ya kazi kwa zaidi ya siku 30, wazabuni kuchelewesha vifaa vya ujenzi, hali iliyochangia miradi kutokamilika kwa wakati na uelewa mdogo wa kamati ya ujenzi, hususani katika masuala ya manunuzi.

Changamoto nyingine ni fedha za kodi ya zuio kukatwa na kutowasilishwa kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), urasimu katika taratibu za manunuzi pamoja na sheria ya manunuzi kutofuatwa katika kumpata fundi.

Amesema kingine ni mafundi kupokea fedha na kutokomea bila kutekeleza mradi husika, jambo linalosababisha wananchi kukosa huduma.

Kufuatia changamoto hizo, Mtaita ameziagiza mamlaka husika ikiwemo Ruwasa wanaosimamia mradi wa uchimbaji kisima kirefu katika Kijiji cha Mwalo wilayani Bukombe, unaotekelezwa kwa gharama ya Sh34.5 milioni kumtafuta fundi aliyekimbia ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

“Mradi huu umesimama kwa miaka mitatu sasa na fundi alilipwa fedha, tumewaagiza waliompa kazi wamtafute kwa gharama yoyote maana amevunja mkataba  wamkamate ili hatua za kisheria zifuatwe dhidi yake,” amesema Mtaita.

“Mamlaka husika zinazoingia kwenye mikataba na mafundi wawe wananchukua hatua mapema badala ya kusubiri Takukuru kuja kuibua miradi hii wanaifahamu na fedha zimetumika,” amesema Mtaita.

Baadhi ya wananchi wa Mji wa Geita wakizungumzia kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wamesema shida kubwa inayochangia miradi isikamilike ni usimamizi mbovu wa wataalamu.

Joshua Maduka mkazi wa Msalala mjini Geita amesema ni vema wataalamu wakatekeleza miradi kwa awamu ili waweze kuisimamia ipasavyo.

Related Posts