Mapya watoto wawili waliopotea Arusha, baba atajwa

Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamsaka mtu mmoja anayejulikana kwa jina moja la Maiko, ambaye ni baba wa watoto wawili wanaodaiwa kupotea wilayani Arumeru mkoani Arusha akituhumiwa kuhusika na tukio hilo.

Hayo yamebainika baada ya kusambaa kwa taarifa za kupotea kwa watoto wawili, Mordekai Maiko (7) na Masiai Maiko (9), wanafunzi wa Shule ya Msingi Olosiva iliyoko Arumeru mkoani Arusha.

Watoto hao walipotea Julai 24, 2024 na taarifa kusambaa jana baada ya kutoonekana ndani ya saa 24 kama ilivyoelekezwa na Jeshi la Polisi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo amesema leo Ijumaa Julai 26, 2024 kuwa katika upelelezi wa awali wamemshuku baba wa watoto hao kuwa huenda anahusika na tukio hilo.

“Bado upelelezi unaendelea wa kuwapata watoto hao lakini kwa hatua za awali, tunamtafuta baba yao kwanza kujiridhisha, baadaye tutatoa taarifa iliyokamilika,” amesema Kamanda Masejo.

Amesema sababu ya kumshuku baba huyo ni kutokana na kujirudia kwa tukio hilo kama ilivyowahi kutokea mwaka mmoja uliopita.

“Tunamshuku baba huyo, kwa sababu siomara ya kwanza watoto hawa kudaiwa kupotea,” amesema Masejo.

“Mwaka jana watoto hawa walidaiwa hivyo hivyo kupotea na katika kuwatafuta tukawakuta salama na baba yao wilayani Karatu, hivyo kwa sasa tunashuku huenda itakuwa hivyo hivyo,” amesema Masejo.

Endelea kufuatilia Mwananchi

Related Posts