Mpina amshukuru Samia kumwondoa Makamba Nishati

Dodoma. Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwondoa aliyekuwa Waziri wa Nishati, January Makamba na kuibadilisha Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Mpina ameyasema hayo leo Alhamisi Aprili 25, 2024 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/25.

Amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kwa hatua alizochukua kuhakikisha hali ya upatikanaji wa umeme inaimarika tangu Januari 2024.

Pia, amesema alipoingia Dk Biteko kwenye wizara hiyo walianza kuziona jitihada za makusudi zilizofanyika ikiwemo usimamizi wa makini kuhakikisha Bwawa la Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere linakamilika na ziara za kutembelea vyanzo vya kuzalisha umeme na kufuta likizo za watumishi.

“Lakini kulikuwa na sarakasi nyingi sana pale Tanesco, kwa mfao waliajiriwa watumishi sita bila usahili wowote, bila ushindani wala kutangazwa na haijulikani kwamba waliletwa kutoka wapi, haijulikani waliletwa kwa ajili ya nini katika shirika lile.

Nao hasa ndio walikuja kuanza katakata ya umeme ambayo ilikuwa ikifanyika pale Tanesco,” amesema.

Amesema hata Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) haikutekeleza majukumu yake sawasawa katika kuhakikisha kwamba umeme unapatikana.

“Sarakasi zote hizo nichukue nafasi hii kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwondoa waziri aliyekuwepo hapo Nishati na kumwondoa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco na kuvunja bodi ya Tanesco.”

Na kuteua wewe Doto Biteko kuwa Waziri wa Nishati ambaye umeonyesha uadilifu mkubwa na unyenyekevu mkubwa kwa wananchi, kuwajibika kikamilifu. Na tunataka mawaziri wa aina yako,” amesema.

Agosti 30, 2023, Rais Samia alifanya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri kwa kumteua Dk Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Dk Biteko alikuwa Waziri wa Madini.

Katika mabadiliko hayo, January Makamba alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Wizara ya Nishati.

Pia, Septemba 2023, Rais Samia alimteua Gissima Nyamo-Hanga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco akichukua nafasi ya Maharage Chande ambaye wakati huo aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na baadaye kuteuliwa kuwa Postamasta Mkuu, Shirika la Posta Tanzania.

Katika mchango wake leo bungeni, Mpina aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi amemwambia Dk Biteko kuwa wanachotaka ni bei ya umeme ipungue kwa kuwa Bwawa la Mwalimu Nyerere limeshakamilika, kudhibiti hitilafu za umeme zinazojitokeza na kulipa fidia za wananchi pale hitilafu zinapojitokeza.

Pia, ametaka sababu nyingine ambazo zilizokuwa zikisababisha kukatika umeme nchini zidhibitiwe.

Mbunge ambaye kwa siku za karibuni amegeuka mwiba kwa baadhi ya mawaziri, amesema mkataba wa kufua umeme wa kampuni ya Songas umefika mwisho lakini waziri hawaeleza hatima ya mkataba huo, ingawa amedai wanajua kuwa kampuni hiyo ilikuwa ikiuza umeme kwa bei kubwa kwa Tanesco.

“Pia, hawa watu walianza kututoza wakifanya ukarabati kidogo tu wanatutoza. Hadi sasa wanatudai Sh107 bilioni za matengenezo, kazi ambayo haiko kwenye mkataba,” amesema.

Amesema wanataka waelezwe kwa kuwa mkataba huo umefika mwisho na isije ikafika umehuishwa tena wakati ulikuwa na migogoro kama hiyo.

Ametaka tathmini ya utekelezaji wa mkataba huo kupelekwa bungeni kabla ya uamuzi wowote wa Serikali.

Mpina ameshauri mkataba wa Tanesco na kampuni ya Ilo Link uvunjwe kwa sababu miito ya simu hasa wakati wananchi wanapopata dharura umekuwa na changamoto kubwa.

“Wananchi wetu wameonewa sana na huu mkataba, kwanza haifahamiki hiyo Ilo Link ilitoka wapi na maamuzi yakafanywa kutoa miito ya simu kwenye mikoa ikawa centralize pale Dar es Salaam halafu ndio wapokelewe na kisha kwenda kutatua changamoto zao,” amesema.

Amesema suala hilo limeunguza vifaa vya wananchi, nyumba zimeungua na uwezo wa kampuni hiyo kupokea simu ni asilimia 30 tu na hiyo inamaanisha asilimia 70 hawapati huduma hiyo.

“Wananchi hawapati huduma lakini unalazimika kulipia huduma kwa wateja. Kwanza watuambie fedha hizo anapewa nani?  Ukipiga kwenye huduma za dharura katika maeneo mengine hakuna malipo,” amesema.

Aidha, Mpina amesema mradi wa Mwalimu Julius Nyerere (JNPPP), unakaribia kufikia mwisho na malipo karibu yanaisha lakini Fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) Sh270 bilioni na fedha ya ucheleweshaji wa miaka miwili na nusu, Sh822 bilioni hazijalipwa.

“Mheshimiwa spika iwe jioni iwe asubuhi hizi fedha za Watanzania lazima zilipwe hata kama kuna sarakasi za nama gani. Waziri atuhakikishie leo hizi fedha zinalipwa, hatutakubali,” amesema Mpina.

Related Posts