Kesi ya mauaji ya mtoto Asimwe yapigwa Kalenda

Bukoba. Kesi ya mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2), imeahirishwa hadi Agosti 9, 2024.

Kesi hiyo iliitwa leo Ijumaa, Julai 26, 2024, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wote tisa kwenye kesi hiyo ya mauaji namba 17740 ya mwaka 2024 walikuwepo.

Mshtakiwa hao ni Padri Elipidius Rwegoshora na Baba mzazi wa mtoto (Asimwe), Novath Venant, Nurdini Masudi, Ramadhani Selestine, Rwenyangira Alphonce, Dastan Bruchard, Faswiu Athuman, Gozbert Alikad na Desdery Everigist.

Wakili wa Serikali, Erick Mabagala, ameieleza Mahakama kuwa mchakato wa kuhamisha kesi hiyo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kagera haujakamilika, hivyo ameomba muda wa kukamilisha mchakato huo.

“Kutokana na taratibu za kuhamisha kesi hii kuipeleka Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba kutokamilika, tunaomba muda mwingine ili tukamilishe taratibu hizo,” amesema Mabagala.

Hatua ya kuhamisha kesi hiyo inatokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza shauri hilo.

 Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba anayesikiliza shauri hilo, Eliapokea Wilson, kabla ya kuahirisha kesi hiyo, ameuliza upande wa washtakiwa kama una changamoto yoyote ikiwa ataiahirisha kesi hiyo.

Wakili wa upande wa utetezi wa mshtakiwa wa kwanza, Mathias Rweyemamu, amejibu kwa niaba ya mteja wake Padri Rwegoshora kwamba hana pingamizi.

Baada ya hapo, Hakimu Eliapokea Wilson akakubali kuongeza muda wa kukamilisha taratibu hizo hadi Agosti 9, 2024, itakapotajwa tena.

“Tumeongeza muda hadi Agosti 9, 2024, shauri hili litakapoitwa tena na kutajwa,” amesema hakimu huyo.

Washtakiwa hao wamerudishwa rumande katika gereza la Bukoba hadi tarehe iliyotajwa itakapofika kwa kuwa shauri lao halina dhamana.

Related Posts