Dodoma. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatarajia kufanya utafiti kuangalia uhusiano wa tatizo la utoro kwa wanafunzi na uwepo wa chakula shuleni.
Akizungumza leo Ijumaa Julai 26, 2014 katika kongamano la kitaifa la utoaji wa chakula na lishe shuleni, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema utafiti huo utahusisha kuangalia kiasi gani uwepo wa chakula mashuleni unachangia watoto kubaki shuleni.
“Utafiti mkubwa wa kuangalia utoro mashuleni utaanza hivi karibuni …Tunafanya utafiti katika masuala ya utoro kwa kuangalia kiasi gani uwepo wa chakula mashuleni unachangia watoto kubaki shuleni na kutotoroka,” amesema.
Alisema lengo lingine ni kupata takwimu sahihi za hali ya utoaji wa chakula shuleni na kuona afua zilizofanyika kwa kulinganisha ‘performance’ (matokeo) ya wanafunzi kabla utoaji wa chakula na baada ya afua hizo.
Profesa Mkenda amesema tayari ipo mikoa inayofanya vizuri katika utoaji wa chakula shuleni kwa kuhakikisha asilimia zaidi ya 80 ya shule zinatoa huduma za chakula.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa na asilimia kwenye mabano Njombe kwa asilimia (58.3), Kilimanjaro (54.03), Arusha (88.07), Pwani (87.85) na Manyara (82.93).
Kadhalika, Profesa Mkenda ametaka watoto ambao wazazi wao hawajachangia chakula wasiondolewe shuleni na badala yake itafutwe namna ya kuwabana wazazi.
Katika kuwezesha pamoja namna nyingine, Profesa Mkenda alizindua Mwongozo wa Utoaji wa Elimu ya Kujitegemea Shuleni ambao utawezesha shule kulima bustani za mboga na matunda kwa ajili ya chakula.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo amesema kufuatia umuhimu wa upatikanaji wa chakula shuleni wizara imetoa nyaraka na miongozo mbalimbali.
Amesema kongamano hilo linafanyika kwa lengo la kuwaweka pamoja wadau mbalimbali, mashirika ya kimataifa na kitaifa pamoja na makampuni mbalimbali ili kujadili kwa pamoja mada zinazohusu chakula na lishe shuleni.
Amesema kongamano hilo lilitoka na maazimio mbalimbali ikiwemo umuhimu wa wataalam wa kilimo na mifugo kushirikiana na shule katika kutoa utaalamu wao kwenye kilimo na mifugo.
Mengine ni jukumu la utoaji wa chakula na lishe lishirikishe wadau wote wa maendeleo, jukumu lianzie kwa familia na kuelimisha jamii kuhusu jukumu la utoaji na uchangiaji wa chakula
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Isabe iliyopo Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, Jacquline Richard amesema jamii ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ilielimishwa na kukubali kuchangia shuleni.
“Walipata elimu na kuanzisha bustani za mbogamboga na matunda na bustani viroba. Wanakula chakula, mbogamboga na matunda baadhi ya siku na wanafunzi wamekuwa wakivutiwa kuja shuleni,” amesema.
Aidha Profesa Mkenda amesema matokeo ya utafiti kuhusiana na mabinti waliopata ujauzito, ripoti yake itatoka hivi karibuni.