Dodoma. Serikali imeahirisha utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa wa kidato cha tano kwa mwaka wa masomo 2024/25 kutokana na changamoto za kiufundi ikiwemo kuchelewa kuchapishwa kwa nakala ngumu za vitabu.
Akizungumza jana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya mwaka 2023 ilipitishwa Oktoba mwaka jana.
Amesema sera hiyo ni kama farasi anayevuta mtaala na kuwa mtaala umetengenezwa kukidhi matakwa ya sera na kuwa umekamilika na kuanza kutekelezwa tangu Januari mwaka huu.
Profesa Mkenda amesema mtalaa huo mpya unatekelezwa katika elimu ya awali, darasa la kwanza, la tatu, kidato cha kwanza na mwaka wa kwanza wa ualimu na kuwa unaenda vizuri.
Hata hivyo, Profesa Mkenda amesema sababu za kiufundi zimefanya kuahirishwa kwa utekelezaji wa mtaala huo kwa wanafunzi wa kidato cha tano.
“Mojawapo ya sababu za kiufundi, ni printing (uchapishaji) ya vitabu haijakamilika na bahati mbaya printing ya vitabu haifanyiki nchini lakini ni jambo ambalo tutakuja kulibadilisha,”amesema.
Profesa Mkenda amesema kuwa waliona vikija na zoezi la usambazaji watachelewa na hivyo walikaa na wadau na kuamua kwa pamoja kuahirisha utekelekelezaji huo.
Amesema vitabu vya mtalaa mpya vinaingia nchini mwezi huu, lakini mtaala wa zamani unaendelea kufundishwa shuleni.
“Vitabu vipo vimeshakamilika vipo katika vishikwambi vya walimu wote nchini na katika maktaba mtandao ukitaka unavipata. Lakini baada ya kujadiliana na wenzentu tukaamua kuahirisha. Hata mimi nikisoma vitabu katika mtandao havinogi,”amesema.
Profesa Mkenda amesema wapo baadhi ya wadau walitaka kuchapisha wenyewe vitabu lakini wakaona kuwa bila kwenda na msukumo mmoja utakuwa tabu kwa sababu mitihani inatungwa na Baraza la Mitihani la Taifa.
Amesema kuwa walikubaliana kwa pamoja kuahirisha hadi mwakani na hiyo maandalizi ya walimu yataendelea.
Profesa Mkenda amesema kuwa baadhi ya wanafunzi wameambiwa itabidi wabadilishe tahasusi walizochagua na kuwa baadhi ya tahasusi zilikuwepo tangu mwaka 2010.
“Hazikufundishwa kwa sababu hazikuwa na walimu lakini zilikuwepo. Shule itatoa tahasusi ikiwa na walimu sio lazima tahasusi zikiandikwa pale ziende zikatolewe. Kwa mfano tahasusi ambazo tumechanganya lugha nyingi huwezi kutoa hiyo elimu,”amesema.
Kauli hiyo ilifuatia barua iliyoandikwa na wizara hiyo Julai 24 mwaka huu na kusambaa katika mitandao ya jamii.
Barua hiyo iliyoonyesha kuwa wizara hiyo ilipokea barua kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Tawala za Mitaa (Tamisemi), kuhusu changamoto zilizopo katika utekelezaji wa mitalaa ulioboreshwa wa kidato cha tano ulioanza kutekelezwa Julai Mosi mwaka 2024.
Barua hiyo ilieleza katika kikao kazi cha pamoja kati ya wizara na Tamisemi kilibaini kuwa changamoto zilizopo ni ukosefu wa nakala ngumu za vitabu kwa matumizi ya walimu na utoaji wa mafunzo kabilishi kwa walimu.
“Kufuatia ombi hilo, WEST kupitia barua yenye kumbukumbu namna CA.128/191/01D/99 ya tarehe 22/7/2024 kwenda Ofisi ya Rais-Tamisemi iliridhia kuahirishwa kwa utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa wa kidato cha tano kwa mwaka 2024 ili uanze kutekelezwa mwaka 2025 baada ya chanagmoto hizo kutatuliwa,” ilisema barua hiyo.
Barua hiyo ilishauri utekelezaji wa mtaala husika kwa upande wa Zanzibar uahirishwe kwa sababu utahini wa wawanafunzi wa sekondari ya juu (A-level) kati ya Tanzania Bara na Zanzibar hutumia mtihani mmoja.