Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu amesema nia yake ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano iko palepale na yuko tayari kuitikia wito wa Watanzania na chama chake.
Lissu ameyasema hayo leo Julai 26, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari alipokuwa akirejea kutoka nchini Ubelgiji alipokwenda kwenye mapumziko kwa zaidi ya wiki tatu.
Amesema mwaka 2020 akiwa na miaka 52 alimkabili hayati Rais John Magufuli na mwakani atakuwa na miaka 57.
Amesema japo nguvu za mwili zimepungua lakini nguvu ya hoja iko vilevile na ana uwezo wa kupambana.
“Mwaka ujao nitakuwa na miaka 57, kwa hiyo haiwezekani nikawa nina nguvu zilezile, lakini nguvu ya hoja na msimamo wa kisiasa na uaminifu kwa Watanzania bado iko pale pale,” amesema.
Kuhusu uchaguzi wa serikali za Mmtaa, Lissu ameonya vitendo vya wizi akisema hawatavumilia.
“Tunakwenda katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, sijui utakuwa Novemba, lakini utakuwa katika mazingira yale yale ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019, amesema na kuongeza:
“Sasa uchaguzi wa mwaka huu kuna kila dalili za kuonyesha kuwa wanaandaa mchezo mchafu tena.Mwaka huu kama watafanya kama ya mwaka 2019 watakuwa wamefanya makosa makubwa sana, watasababisha mambo ambayo hakuna anayetaka yatokee.’’
Amesema Chadema inajiandaa na uchaguzi katika mazingira hayo ya uwezekano wa mchezo mchafu kutokea.
“Tunajiandaa kuhakikisha tunatafuta wagombea katika kila nafasi inayogombaniwa, kuandaa utaratibu wa kampeni, kwa hiyo tunajiandaa kwa mapambano,” amesema.
Alipoulizwa kama wana mvutano kati yake na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, Lissu amesema mgogoro huo haupo na hana mpango wa kugombea uenyekiti.
“Mimi nimetangaza mara 100 na ushee ķwamba mimi sigombei uenyekiti wa chama, huo mvutano unatoka wapi? Ni wa kutengeneza tu na vyombo vya habari.
“Mwaka wa uchaguzi kama kawaida kunakuwa na kelele nyingi, kusipokuwa na kelele hicho ni chama mfu. Chama chetu kinaishi na kwa hiyo kwenye masuala ya kelele za uchaguzi hizo lazima ziwepo,” amesema.
Kuhusu maelezo ya aliyekuwa kada wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa,ambaye sasa amehamia CCM, Lissu amesema ni jambo la kawaida kwa aliyekuwa kiongozi kama huyo kuibua maneno mengi.
“Amekaa kwenye kamati kuu miaka 10, amekuwa mwenyekiti wa kanda karibu miaka 10, amekuwa mbunge vipindi viwili, kuondoka kwake kunakuwa na kelele kutokana na nafasi yake katika chama ni kawaida kuwa na kelele, ingekuwa ajabu kama zisingekuwepo.
“Ninavyokumbuka mimi miaka yote wakihama huwa wanatusema vibaya. Ya Msigwa hayatushangazi,” amesema.
Hata hivyo, amesema kuna umuhimu wa chama chake kumjibu ili kujenga imani kwa wananchi.
“Tuhuma hizo alizotoa katika mazingira haya si kitu kigeni, lakini zinatakiwa zijibiwe. Kama ni mali za chama, kama majengo, mashamba kutakuwa na nyaraka. Kama ni mali zinazohamishika, kama ni pesa kwenye akaunti, hizi vilevile zina nyaraka.
“Pamoja na kwamba tunatakiwa tuchukulie tahadhari huyu aliyeondoka, ni lazima yatolewe maelezo ambayo nafikiri yapo. Ofisi ya Katibu mkuu inashikilia nyaraka zote za chama,’’amesema na kukanusha kwamba Chadema kinaongozwa na mtu mmoja.